Tuesday, April 15, 2014

SERIKALI YAONDOA MZIZI WA FITINA - Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue aonyesha hati halisi ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Ikulu Dar es Salaam






Picha zote na Freddy Maro wa Ikulu.


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
TAMKO LA KATIBU MKUU KIONGOZI KWA VYOMBO VYA HABARI
KUHUSU HATI YA MUUNGANO WA TANGANYIKA NA ZANZIBAR IKULU,
DAR ES SALAAM, TAREHE 14 APRILI, 2014


Siku 12 zijazo tutasherehekea miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, na kuzaliwa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. wamezaliwa watu ndani ya Muungano huu na wengine wana wajukuu.

Inasikitisha sana kuwa leo, miaka 50 baadaye ipo dhana potofu inayojengwa kuwaMuungano huu si halali kwa vile hakuna  hati ya Muungano (Articles of the Union).

Waasisi wa Taifa letu ambao tarehe 22. Aprili 1964 kule Zanzibar walitia saini Hati hiyo, mbele ya mashuhuda, nao wameonekana kama walichokifanya kilikuwa kiini macho, na kwa hiyo kwamba waliongoza Taifa jipya la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa msingi wa kiini macho kwa miaka yote hadi Mwenyezi Mungu alipowaita.

Mambo yote mawili yametusononesha sana sisi Serikalini, na bila shakayamewasononesha wananchi wanaoipenda nchi yao, wanaowapenda  waasisi wa Taifa letu na kuuenzi Muungano wao.

Madai ya kuonyeshwa hati ya Muungano yalianza siku nyingi lakini hatukuweza kuamini hali itafikiwa ilipofikia, ambapo wapo watu wanathubutu kudai na kuapa kuwa hati hiyo haipo.

Ukweli ni kuwa hati hiyo ipo, ilikuwepo siku zote. Hata hivyo, lazima tukubaliane kuwa zipo hati fulani ambazo ni kiini cha uwepo wetu kama Taifa huru, Jamhuri huru na Muungano huru, ambazo tunazihifadhi kama mboni ya jicho. Hati hizo ni pamoja na hati ya Uhuru wa Tanganyika ya mwaka 1961, Hati ya Tanganyika kuwa Jamhuri mwaka 1962, na Hati yaMuungano wa Tanganyika na Zanzibar ya mwaka 1964.

Hati za aina hii zinahifadhiwa maeneo maalum ambayo ni salama ili zisipotee wala kuharibika. Kwa kawaida hatuzitoi, tunazifungua ilikuzihifadhi kwa namna yoyote ile.

Lakini sasa maneno yanakua mengi, tuhuma zimekuwa nyingi, dhihaka zimekuwa nyingi, kiasi cha wananchi kuanza kutiwa mashaka iwapo kweli Hati ya Muungano ipo au la.

Hivyo, kwa maagizo na ridhaa ya Mheshimiwa  Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais waJamhuri ya Muungano wa Tanzania, ninaleta mbele yenu Hati ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar iliyotiwa saini Zanzibar na waasisi wetu, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Mzee Abeid Aman Karume, ili muione na kuwahakikishia Watanzania kuwa yanayosemwa kuwahakuna Hati hiyo si kweli. Hati hiyo ipo tangu wakati huo, imetunzwa vizuri na waliotutangulia, tumeirithi, na tutaendelea kuihifadhi.

Na, tukiombwa kufanya hivyo na Mwenyekiti wa Bunge Maalum nina uhakika  Rais ataridhia ipelekwe huko ili kuondoa mjadala wa kama Hati ipo au la.

Isitoshe, tufanye utaratibu wa kuweka nakala kwenye Makumbusho ya Taifa ili kila atakayetaka kuiona katika miaka mingine 50 ijayo na kuzidi aione.

Mwisho, narejea kusema kuwa kwa upande wa Serikali tunasikitishwa na kufadhaishwa na na tuhuma nzito kwamba labda waasisi wetu hawakuwa makini au walitufanyia kiini macho. Hatukutarajia wawepo Watanzania wenzetu, wafikie hapo.

Ni jambo zito. Vile vile hatukutarajia kuwa Serikali itatuhumiwa kuwa haikuwa makini kuhifadhi waliosaini waasisi wetu.

Matumaini yetu ni kuwa baada ya leo tutaendelea na mambo ya msingi kwa mustakabali, umoja na uimara wa Taifa letu badala ya kuchochea hisia kuwa Muungano wetu hauna msingi imara wa kisheria.

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
Dar es Salaam
14. Aprili 2014

No comments: