Thursday, April 17, 2014

SEHEMU YA HOTUBA YA PROF. LIPUMBA LEO JIONI KWA NIABA YA WAJUMBE WANAOTETEA MAONI YALIYOWASILISHWA NA TUME YA KATIBA;


Profesa Ibrahim Lipumba




Mchango wa Mjadala wa Rasimu;

Mhe. Mwenyekiti gazeti la Mwananchi la tarehe 14 Aprili 2014 limeandika kuwa “Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Uratibu na Bunge), William Lukuvi ameanza kampeni kanisani kuwataka wananchi kupinga serikali tatu zilizopendekezwa na Tume ya Ma...badiliko ya Katiba, vinginevyo nchi itatawaliwa na jeshi kwa kuwa Serikali ya Muungano itashindwa kuwalipa mishahara wanajeshi.” 

Mhe. Lukuvi aliyasema haya katika Kanisa la Methodist, Jimbo la Dodoma alipokuwa mgeni rasmi akimwakilisha Waziri Mkuu, Mizengo Pinda katika ibada ya kumsimika Mchungaji Joseph Bundala kuwa askofu. Hoja kama hiyo pia ilizungumzwa na Rais Kikwete wakati akilihutubia bunge Maalum tarehe 21 Machi 2014.

Ni kweli katika Rasimu ya Katiba taratibu imara za Mapato ya Serikali ya Shirikisho hazijawekwa vizuri. Serikali hiyo haina Mamlaka ya Mapato. Baada ya Rasimu ya kwanza kutolewa tatizo hilo nililichambua kwa kina katika mada niliyowasilisha katika Baraza la Katiba la TCD. Makala hii imetumiwa sana na Wajumbe wa Bunge hili. Hata hivyo wajumbe hawa hawanukuu ufumbuzi uliopendekezwa katika mada hii. 

Baraza la Katiba la TCD chini ya Uenyekiti wa Augostin Lyatonga Mrema ulipendekeza muundo wa serikali tatu na utaratibu wa uchangiaji wa mapato toka serikali washirika kwa kadri mapato yanavyokusanywa na serikali washirika.

Zaidi ya asilimia 90 ya gharama za Shirikisho siyo mpya. Gharama za Rais wa Muungano za hivi sasa zitahamia kwa Rais wa Shirikisho. 

Ikiwa tutakuwa na uwazi na uwajibikaji gharama hizo zitakuwa ndogo kuliko za sasa. Gharama za JWTZ, Polisi, Uhamiaji, Mambo ya nje zitahamia Serikali ya Shirikisho. Zote hizi siyo gharama mpya. Kwa sababu ya uzoefu wa “Akaunti ya Fedha ya Pamoja” na Tume ya pamoja ya Fedha, Rasimu ya Katiba haina pendekezo la kuwepo kwa chombo kinachoshirikisha serikali tatu kujadili na kukubaliana mgao wa mapato ya serikali za washirika kugharamia serikali ya Muungano.

Tume imependekeza ushuru wa bidhaa kuwa chanzo cha mapato ya kodi ya serikali ya shirikisho.Ni vyema mapato ya kugharamia serikali ya Muungano yakachangiwa na mapato ya serikali mbili. 

Katiba itamke wazi serikali za washirika zitachangia sehemu ya mapato yao yote kwenye serikali ya Muungano. Kuzuia migongano ni vyema tukafikia muafaka wa asilimia ngapi ya mapato ya serikali yaende kwenye shughuli za Muungano. 

Kwa kutumia uchambuzi wa gharama za Muungano uliofanywa na Tume ya Pamoja ya Fedha, gharama za Muungano ni asilimia 20 ya mapato ya Muungano. Katiba inaweza kutamka kuwa kiasi kisichopungua asilimia 20 ya mapato yote ya serikali za Washirika yatawasilishwa katika mfuko wa serikali ya Muungano kwa kadri mapato hayo yanavyokusanywa. 

Izingatiwe kuwa kwa utaratibu huu bado mshirika mwenye uchumi mkubwa atakayechangia sehemu kubwa ya gharama za Muungano.
Katiba itamke kuwa Bunge la Shirikisho litatunga sheria ya kuweka utaratibu wa kuhakikisha kuwa sehemu yake ya mapato yanayokusanywa na serikali za Washirika yanawasilishwa kwenye mfuko wa Serikali ya Shirikisho.

Mamlaka ya kukusanya mapato inaweza kusimamiwa kwa pamoja kati ya serikali ya shirikisho na serikali za washirika ili kuhakikisha kuwa mapato yanayokusanywa na kuyawasilisha kwa serikali ya Washirika na serikali ya Muungano kwa uwiano uliokubaliwa. 

Miaka ya 1960 na 1970 Mamlaka ya kukusanya mapato ya Afrika Mashariki ilikusanya kodi za mapato, ushuru wa forodha na ushuru wa bidhaa Kenya, Tanganyika na Uganda na kuziwasilisha kwenye serikali husika. 

Sera za kodi zilitungwa na nchi husika lakini kodi za nchi hasa ushuru wa forodha zilifanana.

Kama CCM ingekuwa na nia njema utaratibu wa kukusanya kodi na kugawa kwenye serikali ya shirikisho na serikali za washirika siyo rocket science ni jambo ambalo linaweza kuwekwa vizuri ndani ya katiba. Katiba ya muungano kama katiba mama ijenge misingi mizuri ya usimamizi wa fedha za umma na ukusanyaji wa kodi.

Mhe. Mwenyekiti, Rasimu ya Katiba imeletwa na Tume ya Rais ili tuijadili na kuipitisha. Rasimu hii siyo ya CUF, siyo ya CHADEMA, siyo NCCR Mageuzi, siyo ya Wapemba.
Ni Rasimu ya Tume ya Rais Kikwete.

Katika hotuba yake katika kanisa la Methodist Mhe. Lukuvi pia alisema “Serikali tatu zikipita ni wazi kuwa hata makanisa yatafungwa kwani nchi haiwezi kuwa na amani tena.”

Lukuvi alisema Wazanzibari wanaotaka kuwa na nchi yao hawawezi kujitegemea, bali wanataka Serikali ili wapate nafasi ya kujitangaza kuwa ni nchi ya Kiislamu.

Baadaye alipotakiwa kufafanua kauli yake, Lukuvi alisema alichokizungumza kanisani hapo ni mawazo yake binafsi ambayo yanafanana na Watanzania wengi, akiwamo Rais Jakaya Kikwete.

Mhe. Mwenyekiti je lengo la serikali mbili ni kuwadhibiti Wazanzibari wasianzishe dola ya Kiislam kama alivyoeleza Mhe. Lukuvi? Baada ya hotuba ya Mhe. Lukuvi “Askofu Bundala alisema kanisani hapo kwamba ili kudumisha Muungano ni vyema Katiba ya Zanzibar ifutwe ili iwepo moja ya nchi moja ambayo inadumisha Muungano.”

Mchakato wa kupata katiba mpya unapaswa kuwa wa maridhiano, Vipi Waziri anayemuwakilisha Waziri Mkuu anaenda kanisani na kusema Wazanzibari wanaotaka kuwa na nchi yao hawawezi kujitegemea, bali wanataka Serikali ili wapate nafasi ya kujitangaza kuwa ni nchi ya Kiislamu.

Kama hamuitaki Rasimu ya Katiba ya Tume ya Rais kwa nini mmetuleta hapa kwa gharama kubwa. Tunaambiwa Bunge limekarabatiwa kwa shilingi bilioni 8.2. Je ni utaratibu wa 10 percent uliohamasisha kutumia fedha nyingi huku serikali ikiamini kuwa Rasimu ya Katiba haifai kabisa.

Mjadala umekuwa wa matusi na siyo wa kujenga hoja. Kauli za kibaguzi zimetolewa dhidi ya Wapemba, dhidi ya Waarabu, dhidi ya Wahindi. Wajumbe wa Bunge Maalum wanashangilia kauli za kibaguzi. Tunaanza kupanda mbegu ya intarahamwe wa Tanzania. Kauli za kibaguzi ni kinyume cha maadili na tunu za Watanzania.

Kwa utaratibu wa kanuni 33 (7), Baada ya taarifa ya kamati namba moja hadi namba kumi na mbili kuwasilishwa, taarifa hizo zitajadiliwa kwa kipindi kisichozidi siku tatu. Baada ya mjadala kamati ya uandishi inapaswa kuanda vifungu vya sura hizo mbili ili vipigiwe kura na wajumbe wa pande mbili za muungano. Hilo halitafanyika.

Kufuatana na Ratiba, Bunge Maalum litaendelea hadi tarehe 25 Aprili bila kupiga kura na kufanya maamuzi ya vifungu vya sura hizi mbili kinyume na kanuni. Bunge linaahirishwa hadi Agosti bila kufanya maamuzi ili kuwapa nafasi CCM watafute theluthi mbili ya pande zote za Muungano kwa njia yeyote ile. 

Tunaopigania katiba ya wananchi hatuwezi kubariki uchakachuaji wa maoni ya wananchi. Wakati umefika tuwaache CCM muendelee na vioja vyenu kwani hamtaki kuandika katiba inayotokana na mawazo ya wananchi badala yake mnahamasisha chuki dhidi ya Wapemba, Wahindi na Waarabu na kupandikiza uhasama wa kidini.

No comments: