Thursday, August 07, 2014

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI BUNGE MAALUMU LA KATIBA LIPEWE NAFASI YA KUFANYA KAZI YAKE-


Mwenyekiti wa Bunge Maalum, Mh.Sitta


Ofisi ya Bunge Maalum , imeshangazwa na kusikitishwa na baadhi ya vyombo vya habari na makundi ya jamii yanayoenezwa upotoshwaji mkubwa ambao umedakwa katika mitandao ya jamii kuhusu kauli aliyoitoa Mwenyekiti wa Bunge Maalum Mhe . Samuel Sitta (Mb) wakati wa mjadala wa kupitisha kanuni tarehe 5 Agosti , 2014 kuhusu midahalo ya Katiba inayoendelea katika baadhi ya televisheni hapa nchini.

Mwenyekiti wa Bunge Maalum , Mh.Sitta hapo tarehe 5 Agosti 2014 alitahadharisha kuhusu baadhi ya midahalo hiyo inayoendeshwa ikiwa na mapungufu makubwa.Wanapangwa washiriki wenye mawazo na malengo ya upande mmoja na kutumia fursa hiyo kushambulia kwa lugha chafu makundi yenye mawazo tofauti ambayo kimsingi yalitakiwa yashirikishwe kwenye midahalo hiyo.Tumeshuhudia upotoshwaji mkubwa kuhusu kauli ya Mwenyekiti .Hali hii inadhihirisha jinsi maadili ya upashanaji habari yanavyotumiwa vibaya na baadhi ya vyombo vya habari na baadhi ya makundi ya jamii.

Ifahamike wazi kuwa lengo la Mh.Mwenyekiti Sitta lilikuwa ni kuwakumbusha wahusika na waandaji wa midahalo hii pamoja na serikali kuwa utaratibu huu wa kualika kundi moja lenye mrengo mmoja na kuuita mkutano huo ni mdahalo si sahihi. Mdahalo tafsiri yake, hauna budi kuwa na pande mbili au zaidi.Utaratibu wa uaandaji wa midahalo kote ulimwenguni msingi wake ni kutoa fursa kwa wasikilizaji/watazamaji kusikiliza pande zote zenye mawazo tofauti na kuwaachia wananchi kuchambua mawazo hayo na kuona yepi wayakubali au kuyakataa.

Inasikitisha pale ambapo baadhi ya watu wameamua kuitumia kauli ya Mwenyekiti, Mh.Sitta kwa Kupotosha umma na kujikita katika kuzua malumbano yasiyo na tija kwa Taifa hususani katika kipindi hiki ambacho wananchi wangependa kufuatilia mijadala kuhusu Katiba.

Baadhi ya vyombo vya habari , kwa makusudi vimeamua kubeba agenda tofauti na kuangukia katika mtego wa kuchochea uhasama.Matoleo yao wamekuwa na Vichwa vya habari vilivyosomeka "Sitta Avaa Udikteta", Bunge lataka kina warioba wadhibitiwe", Sitta avunja nchi nk na hatimaye upotoshwaji wa aina hii kuenezwa katika mitandao ya Kijamii ili kuuchafua mchakato wa Bunge Maalumu la Katiba kutunga katiba na Kumchafua Mwenyekiti.

Ofisi ya Bunge Maalum inasisitiza na kuvikumbusha vyombo vya habari kuzingatia maadili ya upashanaji habari kwa uadilifu, hususani katika kipindi hiki ambacho Nchi ipo katika Mchakato ambao wananchi wangestahili kupata taarifa sahihi kuhusu utungaji wa Katiba. Bunge Maalum linakaribisha maoni ya wananchi yenye dhamira safi bila kuingiza chuki binafsi, uchochezi na upotoshaji habari kwa makusudi.

Bunge Maalum linatoa rai kwa wote kwamba liachwe litimize wajibu wake.
IMETOLEWA NA
OFISI YA KATIBU WA BUNGE MAALUMU 


6.Agosti 2014

No comments: