Tuesday, June 19, 2007
Kama wewe ni mpenzi wa muziki wenye midundo ya reggae au michanganyiko ya reggae na aina zingine za muziki kama zouk, african jazz nk uwezekano ni mkubwa sana kwamba umeshawahi kumsikia au kumuona jukwaani Ras Nas au kwa jina lingine Nasibu Mwanukuzi. Ras Nas ni mtanzania anayefanya kazi zake za muziki nchini Norway ndani ya jiji maarufu la Oslo. Jambo moja ambalo pengine wapenzi na mashabiki wake hawajui ni kwamba Ras Nas ni mwanasheria kitaaluma. Alisomea sheria katika chuo kikuu cha Dar-es-salaam. Pia ni mtunzi na mghani mzuri wa mashairi.
Kwa wapenzi wa muziki wa reggae hususani Kaskazini mwa Ulaya, ukitaja jina la Ras Nas hawatokuuliza maswali mengi. Muziki wake unaongea, mashairi yake yanazungumza lugha inayoeleweka.
Kwenye wasifu wake (Curriculum Vitae) anaonekana ameshiriki msururu wa matamasha kama vile Norwegian Wood – Oslo, Bergen International Music Festival – Bergen, Verden i Norden – Oslo, Oslo Mela Festival – Oslo, Zanzibar International Film Festival – Stone Town, Zanzibar, Festival of Performing Arts and Music – Lahore, Pakistan, Radio concert – Norwegian Broadcasting Corporation NRK P2 na mengineyo.
Mwaka huu anatarajiwa pia kushiriki tamasha maarufu la Oslo Mela Festival jijini Oslo. Lakini kabla ya kulipanda jukwaa mwaka huu Ras Nas atakuwa ameshatoa albamu mpya ambayo ameipa jina la Dar-es-salaam hivyo kuendelea kuwa “balozi” wetu mzuri nchi za Ulaya Kaskazini. Kama hujawahi kuzisikiliza baadhi ya nyimbo za Ras Nas basi unaweza kuanza sasa kwa kubonyeza hizo "links" hapo chini. Ukitaka kuona anapokuwa jukwaani anakuwa mtu wa aina gani bonyeza hapa.Ukitembelea tovuti yake utajifunza mambo kadhaa.
Sweet Rhythms
Guantanamo
River Nile
Kwanini aliamua kuachana na taaluma yake ya sheria na kujikita zaidi kwenye muziki? Nini kipya katika albamu yake mpya? Ana mipango ya kurejea Tanzania na kuendeleza kazi ya muziki? Ameshirikiana na wasanii gani kutoka Tanzania katika albamu yake hii? Hayo na mengineyo yatakujieni hivi karibuni BongoCelebrity itakapofanya mahojiano rasmi na Ras Nas. Kaa chonjo!
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment