Mambo kangaja, huenda yakaja!
MIONGONI mwa mambo mazuri yanayonogesha lugha ni methali. Methali huifanya lugha iwe tamu na yenye haiba masikioni mwa anayesikiliza. Methali humsaidia mtu kuelewa kwa upana na wepesi maana ya kinachokusudiwa kusemwa.
Methali hutumiwa na ‘wenye lugha yao’ kuwasilisha ujumbe au maana kwa haraka na wepesi zaidi. Humfanya anayeelezwa jambo kwa njia hiyo, ubongo wake unase haraka sana maana ya analoelezwa.
Kwa mfano mtu akiambiwa “mgaa mgaa na upwa hali wali mkavu”, moja kwa moja anaelewa anatakiwa afanye nini. Methali hii hutumiwa kuwaelimisha watu wasiopenda kujihangaisha kutafuta maisha yao. Watu wanaopenda kukaa bila kujihangaisha, wakidhani maisha yao yatakuwa mazuri kwa kutegemea fadhila tu.
Gaagaa ni kwenda huku na huko. Si mtu anayetulia mahala pamoja. Ni mtu anayejituma.Upwa ni ufukwe wa bahari. Hali ni kinyume cha kula. Hivyo methali hiyo ina maana anayehagaika hatakosa kitu. Lazima atakipata au hata kama hakupata alichokinuia, atapata kingine badala pake. Ndiyo maana ya kuwa hatakula wali mkavu, kwani hata dagaa ataambulia tu kwa kuhangaika ufukweni.
Hivyo methali hii inamfundisha mtu anayehangaika ufukweni kwamba hatakosa kitoweo. Anaweza asipate changu au nguru, lakini anaweza akaambulia japo chaza.
Karibu lugha zote duniani zina utaratibu wa kuwa na methali. Si Kihindi, si Kichina, si Kijerumani, Kihaya, Kinyakyusa au hata Kizaramo. Zote zina methali ambazo wakati mwingine bila mtu kusema analolikusudia, akiitamka tu, anayeambiwa anaelewa moja kwa moja anachoambiwa.
“Ukistaajabu ya Mussa, utayaona ya Firauni” ni moja ya methali lukuki za Kiswahili. Hii inatuelimisha kwamba mtu asipende kushangaa mambo, kwani dunia ni duara. Akishangaa hili, atakumbana na kubwa kuliko hilo ambalo hukulitarajia kama linawezekana. Inakuwaje?
Hali hiyo ndiyo iliyomkumba mwanasiasa mmoja mashuhuri nchini mwetu mwenye nasabu ya ‘Mtu wa Mungu’. Mwanasiasa huyu alimshangaa sana mwanasiasa mwenzake, alipokumbwa na masahaibu ya kidunia hivi karibuni.
Mwanasiasa mwenzake huyo, alikumbwa na mkasa wa ‘kuchomekewa’ na dereva wa daladala alipokuwa katika gari lake. Aligongwa. Kwa hasira mwanasiasa huyo alimfuata dereva aliyemchomekea na kubishana naye. Katika mabishano yao, mwanasiasa yule alikuwa na silaha ya moto ambayo inadaiwa ilifyatuka, na risasi kumpiga dereva ambaye alikata roho.
‘Mtu wa Mungu’ akalishabikia sana hilo. Alimshutumu mwenzake na kufikia hatua ya kumlaani! Hiyo tisa, lakini ni majuzi tu ametinga mahakamani kumfungulia mashitaka akipinga kwa nini ameachiwa kwa dhamana. Anataka arudishwe jela, akae rumande hadi kesi yake itakapomalizika.
Waswahili husema “Mungu si Athumani’ au ‘Mcheka kilema hafi hakijamkuta’. Juzi naye ‘Mtu wa Mungu’ kakumbwa na yale yale aliyomcheka na kumkebehi mwenzake. Akiwa katika gari lake la gharama kubwa, akitokea Mbagala kwenda katikati ya jiji la Darisalama, ‘Mtu wa Mungu’ alichomekewa.
Si unajua mambo ya jiji hili ambalo limezoeleka kuitwa ‘Jiji la Makamba’, ambalo sasa linapaswa kuitwa ‘Jiji la Kandoro’ katika nyakati za foleni zisizokwisha? Zinazowatoa jasho madereva na abiria wao? Mwenye daladala kakaa kwenye msururu kachoka. Kama kawaida yao, ‘katanua’.
Kufumba na kufumbua hamad, gari na ‘mheshimiwa’ mwanasiasa mwenye nasaba ya mchungaji, limeguswa kwenye kioo. Pazuri hapo! Mheshimiwa huyu kashuka, na moja kwa moja kwa dereva wa daladala. Walioshuhudia wanadai alimshusha na kuanza kumtandika makofi. Inakuwaje!
Je, kama angekuwa na ‘cha moto’ naye si angefuata nyayo za mwanaisasa mwenzake aliyemsubu na kumshutumu kujichukulia sheria mkononi? Yeye amefanya nini? Wee acha tu; mambo haya uyasikie hivi hivi. Wenye daladala wana mambo na vijambo barabarani vinavyoweza ‘kumlevya’ yeyote hata uwe jasiri kiasi gani.
Cha kuomba, mambo hayo yasikukute. Mungu apishe mbali, vinginevyo wengi tungejikuta mikononi mwa pilato kwa kuwajeruhi madereva wa daladala! Yale yale ya “usicheke kilema wakati unaendelea kuishi”.
Ni vyema basi, binadamu mwenzako anapokutwa na janga, usipende kulivalia njuga na kumwona mjinga. Utambue kuwa kuna mazingira yanayoweza kumkuta mtu yakamfanya awe nusu kichaa, akili ikashindwa kutafakari. Cha kufanya ni kumwombea Mungu ampe moyo wa subira. Usishangilie kwani Waswahili husema “mambo kangaja, huenda yakaja”.
Makala hii imechekuliwa toka kwenye gazeti la Uhuru, Jumatatu, Julai 2, 2007.
Baruapepe: hassanmwa@yahoo.com
Simu (Dar es Salaam): 0784-300715
No comments:
Post a Comment