Friday, August 10, 2007

Kiingereza siyo kigezo cha shule kuwa ya kimataifa


na Stella Nyemenobi
__________________

Wizara inazitambua shule 17 pekee za kimataifa.

"International School" ni maneno ya Kiingereza yamaanishayo "shule ya kimataifa" ambayo wanajamii wengi nchini Tanzania wamekuwa wakiyatumia kuelezea au kuiita shule zinazotumia lugha ya kigeni, hususan Kiingereza katika kuwafundisha wanafunzi. Wakati zipo shule nyingi ambazo Kiingereza hutumika kama lugha kuu ya mawasiliano kuanzia awali hadi sekondari, maarufu kama "English medium schools", lugha hiyo haimaanishi kuwa zinapaswa kuitwa shule za kimataifa. Wamiliki ambao hupitia mchakato wa aina mbalimbali na hatimaye kuanzisha shule hizo, ni wazi wanaelewa ukweli kuhusu tofauti kati ya shule za kimataifa na shule zao, ingawa wakati mwingine, baadhi hupotosha umma kwa kujiita kuwa shule zao ni za kimataifa.

Kubwa ambalo limekuwa likichanganya jamii na kuchukulia shule hizo za Kiingereza kuwa ni za kimataifa, ni pale shule inapoitwa jina kwa kuanzia na St. (kifupi cha Saint) kwa kumaanisha Mtakatifu.

Kaimu Ofisa Elimu Kiongozi, Leonard Musaroche anaelimisha juu jamii juu ya hilo na kusema, "Shule kutumia lugha ya kufundishia ya Kiingereza siyo kegezo cha kuwa shule ya kimataifa." Anasema Wizara ina orosha ya shule shule ambazo inazitambua kuwa ni za kimataifa na kwamba shule hizo zinatambulika kisheria. Zipo shule 17 pekee zilizosajiliwa nchini (Bara) za kimataifa. Shule za kimataifa zenye shule za awali ba msingi zinazotambuliwa na mikoa yake katika mabano ni Laureat, Haven of Peace, Essacs, St. Mary´s Academy Tabata, Kwanza (Dar es Salaam). Nyingine ni shle zao za msingi zilizopo Morogoro, Tanga na Iringa.

Kwa upande wa shule za kimataifa zenye Awali, Msingi na Sekondari zinazotambulika na mikoa husika katika mabano ni St. Constantine, Braeburn, St. Georges na Moshi (Arusha). Nyingine ni Shule ya Kimataifa ya Tanganyika na Academic, (za Dar es Salaam), Canon Andra Mwaka (Dodoma), Moshi (Kilimanjaro) na Isamilo ya Mjini Mwanza.

Katika kuzungumzia tofauti ya shule za kimataifa na nyinginezo, Ofisa huyo wa Wizara, haisajili shule zenye hadhi hiyo, bali usajili wake hufanywa na taasisi za kimataifa zenye jukumu hilo. Kisheria, kazi ya Wizara ni kuthibitisha na kutambua shule zilizosajiliwa na taasisi hizo. Miongoni mwa taasisi zinazohusika na usajili wa shule hizo ni kama vile "European Council for International Schools" (ECIS) na "Association of International Schools in Africa" (AISA).

Taasisi hizo zimeweka vigezo vya kusajili shule za kimataifa ambazo lazima mwenye lazima mwenye shule husika, avitimize kabla ya shule yake kutajwa kuwa ni ya kimataifa. Ili shule iwe ya kimataifa, Wizara imeweka maelekezo yanayotakiwa kuzingatiwa. Miongoni mwa maelekezo hayo ni kwamba, lazima shule isajiliwe kwanza na Wizara kama shule ya kawaida. Baada ya hapo, mwenye shule akitaka kuibadilisha iwe ya kimataifa, anatakiwa aiombe Wizara kwa maanndishi. Endapo Wizara itaridhika na maombi hayo, itatoa kibali cha maandishi na mwenye shule ataendelea na hatua za kutuma maombi kwenye taasisi zinazosajili shule hizo.

Musaroche anasema shule ikishasajiliwa kama ya kimataifa, mwenye shule ni lazima aijulishe Wizara kimaandishi na kuambatanisha na nakala ya usajili huo. Wakati katika hali ya kawaida, shule zinazotumia lugha ya Kiingereza katika kufundisha, baadhi zimekuwa zikijitambulisha kuwa ni za kimataifa, Kaimu Ofisa Elimu Kiongozi anashauri jamii kuepuka utata kwa kuhoji chombo kilichojisajili shule husika.

"Mwananchi anapaswa kumuuliza mwenye shule kama shule yake imesajiliwa na taasisi za kimataifa zinazotambulika na Wizara", anasema. Kwa mujibu wa Mtendaji huyo wa Wizara, mitaala inayotumika katika shule za kimtaifa ni kutoka Uingereza (British Curriculum) na Marekani (American Curriculum).

Hata hivyo anasema baadhi ya shule hutumia pamoja na mitaala ya Tanzania. Mathalan, shule ya St. Mary´s Academy Tabata na St. Mary´s Mbezi Beach (zote za Dar es Salaam), ndizo zinazotumia mitaala hiyo ya nje mchanganyiko na mtaala wa Tanzania. Tofauti na shule hizo 17 za kimataifa, shule zilizobaki, husajiliwa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi. Aina ya shule zinazosajiliwa ni pamoja na shule za serikali na zisizo za serikali.

Akielezea mchakato wa uanzishaji wa shule hizo, Musaroche anasema hilo ni mojawapo ya majukumu yanayofanywa na Wizara hiyo kwa shule kama hizo ili kuhakikisha kuwa elimu inayotolewa kwa wadau inazingatia Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 1995, Sheria ya Elimu namba 25 ya mwaka 1978 na marekebisho yake, namba 10 ya mwaka 1995.

Ili kuanzisha na kusajili shule zenye ubora unaostahili, wadau hawana budi kufuata hatua mbalimbali kama zilivyoainishwa kwa kina katika Mwongozo wa Usajili wa Shule wa mwaka 1982.

Hatua ya kwanza ni kupata kibali cha kujenga shule. Mwenye nia na uwezo wa kuanzisha shule, anatakiwa kutuma maombi ya kutaka kujenga shule kwa maandishi kwa Ofisa Elimu Kiongozi. Maombi haya ni lazima yapitishwe kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya na Katibu Tawala wa Mkoa ambako shule husika itajengwa. Anayehitaji kujenga shule hutakiwa awe ni viambatanisho mbalimbali ikiwamo andiko la mradi, nakala ya ramani ya majengo ya shule na hati au uthibitisho wa kumiliki ardhi kisheria. Ofisa Elimu Kiongozi akisharidhika na maombi hayo, atatoa kibali cha kujenga shule kimaandishi na ndipo ujenzi utaanza.

Mwongozo wa usajili unaeleza hatua ya pili kuwa mwombaji anapaswa kujaza fomu nyingine ya kuomba kuthibitisha kuwa Meneja wa Shule. Lakini pia, hatua hii itafanywa baada ya mwombaji kuwa amekamilisha mahitaji muhimu kama vile majengo na samani muhimu, vifaa vya kufundishia na kujifunzia, kuwa na walimu na wafanyakazi wenye sifa. Matayarisho yawe yamekaguliwa na mamlaka za Wilaya ambao ni Mhandisi wa Majengo, Ofisa Afya na Mkaguzi Mkuu wa Shule. Wizara ikiridhia, hutoa kibali cha maandishi cha kumthibitisha mwenye shule na meneja wa shule.

Baada ya mwenye shule kukamilisha mahitaji yote yanayotakiwa na shule kukaguliwa, hupewa taarifa ya shule kusajiliwa kwa maandishi. Vile vile hupewa cheti cha usajili chenye namba ya usajili wa shule.

Ingawa Wizara inaunga mkono na kuwa tayari kuwasaidia watu wenye nia ya kuwekeza katika elimu, lakini inasisitiza kuwa umuhimu wa kusajili shule uko pale pale. Usajili huo, unawezesha wizara kubaini ubora wa shule husika ikizingatiwa kwamba cheti cha usajili hakiwezi kutolewa kabla ya shule kukaguliwa. Lengo la ukaguzi ni kuhakikisha kuwa elimu itakayotolewa inakidhi vigezo.

Makala hii ilichapishwa kwenye Jarida Maarifa la Habari Leo, Alhamisi Julai 26, 2007. Viungo vya tovuti vimewekwa na mtumaji wa makala kwenye blogu hii, Bw. Omari Guy Agallo Chichi.
omyguyagallochichi@yahoo.co.uk

No comments: