Saturday, September 22, 2007

Helga Gabriel Tarimo-Richa Adhia alituzidi kwa mambo mengi



KAMA ilivyo ada ya Face 2 Face, kutuliza ‘mtima’ wa wasomaji wetu, Mwandishi FATMA AMRI wiki hii amejibu maombi ya wadau wetu waliyoomba kujua machache kutoka kwa Mrembo wa Vodacom, Miss Popularity 2007, Helga Gabriel Tarimo ambaye pia ni Mlimbwende wa Shinyanga na Kanda ya Ziwa.....
_______________________________________

FACE 2 FACE: Habari yako Miss Popularity

HELGA: Nzuri Sister, namshukuru Mungu kwa kuniwezesha kuiona siku hii ya leo.

FACE 2 FACE: Nimelazimika kukutafuta kutokana na msukumo wa wadau wa safu hii. Hivyo kabla ya kusonga mbele ni vema tuanze kupata historia yako kwa ufupi.


HELGA: Jina langu kamili ni Helga Gabriel Tarimo, nimezaliwa mwaka 1986, mimi ni kifungua mimba katika familia ya watoto sita ya Mzee Gabriel.

Harakati za kumkataa adui ujinga, nilianza mwaka 1992 ambapo nilihitimu shule ya msingi 1998, niliendelea na masomo ya sekondari katika Shule ya St. Theresia na kuhitimu mwaka 2002.

Kwa sababu lengo langu ni kupata elimu zaidi, kwa sasa naendelea na masomo nchini Kenya, nikisomea mambo ya uhusiano wa jamii katika Chuo cha Graffins (Graffins College), jijini Nairobi.

FACE 2 FACE: Nani alikushawishi kujiingiza katika urembo

HELGA: Ok, ni Dotto Nsurupia, ndiye aliyenishawishi kuingia kwenye mambo ya urembo baada ya kuona nina vigezo vyote vinavyohitajika, alinitaka niingie kwenye kinyang’anyiro cha Miss Shinyanga ambapo nilishinda.

FACE 2 FACE: Wewe unatokea Mkoa wa Arusha kwa nini ukashiriki Miss Shinyanga?

HELGA: Mimi ni Mtanzania, naruhusiwa kushiriki sehemu yoyote ndani ya nchi hii, haijalishi nimezaliwa Mkoa gani.

FACE 2 FACE: Ulikuwa katika hali gani mara baada ya kutangazwa Miss Shinyanga?

HELGA: Kwanza nilimshukuru Mungu na kujiona mrembo ambaye nina sifa za kutosha kuiwakilisha hata nchi, ari hiyo ndiyo iliyoniwezesha kushika nafasi ya tatu Miss Kanda ya Ziwa na hatimaye kuingia katika kinyang’anyiro cha Ulimbwende wa Tanzania ambapo nilitawazwa Miss Popularity.

FACE 2 FACE: Ulipokuwa katika Kambi ya Miss Tanzania ni kitu gani ulikuwa hufurahishwi nacho na kipi kilikuwa kikikufurahisha.

HELGA: Nilikuwa sifurahii mikwaruzano ya warembo wenzangu na majigambo. Kitu ambacho kilinifurahisha sana kambini ni kitendo cha mimi kuwemo kwani jambo kama hilo lilinitokea mara moja katika maisha na halijirudii.

FACE 2 FACE: Utaratibu gani uliotumika kumpata Miss Popularity?

HELGA: Miss Vodacom Popularity alipatikana kwa kupiga kura kwa njia ya kutuma ujumbe mfupi wa maneno (SMS) ambapo watu walimchagua mrembo wanayemtaka.

FACE 2 FACE: Zawadi gani ulipata baada ya kushinda taji hilo?

HELGA: Nilipata zawadi ya shillingi 5,000,000, nimepanga kuzitumia kwa kujilipia ada.

FACE 2 FACE: Baada ya kuvishwa taji hilo nini majukumu yako kwa cheo ulichotunukiwa?

HELGA: Majukumu yangu kama Miss Popularity ni kufanya shuguli za jamii kama kutembelea watoto yatima, kuwatia moyo waathirika wa ukimwi na kupambana na janga hilo.

FACE 2 FACE: Wengi wanampinga Miss Tanzania 2007, Richa Adhia kuwa hakustahili kuvikwa taji hilo nini maoni yako?

HELGA: Mimi kama mshiriki niliyekuwa kwenye kinyang’anyiro hicho, ninamkubali kwa sababu alikuwa na vigezo vilivyohitajika na kati yetu wengi hatukumfikia, kweli alistahili kuukwaa umalkia huo.

FACE 2 FACE: Nini matarajio yako ya baadaye?

HELGA: Natamani kuwa Mwana uhusiano bora, kutetea haki za wanawake na watoto.

FACE 2 FACE: Safu hii inakupata fursa ya kuwashukuru baadhi ya watu ambao wamekuwezesha kufika hapo ulipo.

HELGA: Kwanza kabisa, Dotto Nusurupia ambaye alinishawisi kuingia katika fani ya urembo, pia nawashukuru wananchi kwa kunipigia kura na kuniwezesha kushinda Miss Popularity, kwa sababu huo ni mwanzo mzuri wa maisha yangu ya baadaye.

FACE 2 FACE: Nashururu kwa ushirikiano wako.

HELGA: Ok, nami nakutakia kazi njema.

Chanzo: Global Publishers Tanzania.

No comments: