Sunday, October 14, 2007

Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Leo Jumapili tarehe 14 Oktoba 2007 ni miaka minane toka baba wa taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alipofariki dunia.

Alhamisi tarehe 14 Oktoba 1999 Tanzania, bara la Afrika na wapenda maendeleo ya binadamu duniani kote, tulimpoteza shujaa mkuu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Tanzania imeihalalisha siku ya tarehe 14 Octoba kila mwaka, kuwa siku ya Mwalimu Nyerere. Madhumuni ya siku hii ni kumkumbuka au kukumbushana juu ya yale ambayo Nyerere aliyaamini, kuyakemea n.k. misingi ya uongozi bora huchimbuliwa tena kwenye siku hii.

Mnara wa kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere mjini Dodoma.

Tukumbuke baadhi ya nukuhu hizi chache za Mwalimu Nyerere.

"Hatuna haja ya kusoma vitabu vya Karl Marx au Adam Smith kugundua kwamba jembe au ardhi pekee haiwezi kuleta mali. Wala hatuna haja ya kupata shahada ya Uchumi kufahamu kwamba ardhi haiundwi na mfanya kazi wala kabaila. Ardhi ni zawadi ya Mwenyezi Mungu kwa mwanadamu, ipo siku zote"
(Kijitabu cha TANU 1962)

Mnara wa kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere mjini Dodoma.

"Watanzania ni watu maskini. Kuwabebesha watu maskini mikopo ambayo inawazidi kimo si kuwasaidia bali ni kuwaumiza. Na hasa inapokuwa, mikopo hiyo ambayo wanatakiwa walipe haiwafaidii wao, bali inawafaidia wachache tu.."
(Ujamaa, uk. 23)


"..tunapotaja unyonyaji hufikiria mabepari, tusisahau kuwa bahari ina samaki wengi. Nao hutafunana. Mkubwa hutafuna mdogo na mdogo naye humtafuta mdogo zaidi..." (Ujamaa, uk. 27)



"Nyawabiso bisoburuweri, akerero kerembura (ni Kizanaki...Wazanaki mtusahihishe hapa) maana yake: Mficha ficha maradhi, kilio kitamfichua.."



"Hakuna msahafu wa siasa, wala hautashuka msahafu, utakaotoa majawabu ya matatizo yote ya siasa ya uchumi yatakayotokea katika nchi hii katika siku za mbele."
(Ujamaa, uk. 51)



"Mtu akitoka Dar es Salaam kuja Kairo ataelekea Kaskazini; lakini mtu akitoka Moscow kuja Kairo ataelekea Kusini. Jambo lililo muhimu ni kwamba kila mmoja wetu aelekee lengo, kutoka mahali panapofaa kuanzia"
(Ujamaa, uk. 85)


"Hakuna jibu rahisi...nchi yetu ina umoja mkubwa, watu wake wanazo tofauti mbalimbali. Kwa hiyo haiwezekani mtu kukaa Dar es Salaam na kuandika msahafu wa jinsi ya kuishi na kufanya kazi katika kila kijiji na kitongoji cha Tanzania...(Ujamaa, uk. 118)


"...maneno matupu, yangawa matamu, hayavunji msitu..." (Ujamaa, uk.129)


"Azimio la Arusha halikuleta miujiza. Halikutuongzea mazao, wala halikusaidia mvua kunyesha. Halikuwatajirisha watu wala kuwafanya wawe na elimu zaidi. Halikubadilisha mawazo yetu tuliyolelewa nayo wala kutubadili hali yetu kwa miujiza............
(Hotuba ya Rais kuhusu utekelezaji wa Azimio la Arusha, ktk. Mkutano Mkuu wa TANU Mwanza 17 Oktoba 1967)


Namkumbuka Nyerere

Tusifunike uwazi, na ukweli tuuseme,
Kukumbuka sio kazi, hakuhitaji umeme,
Kwenye kuenzi malezi, wote tupeane shime,
Namkumbuka Nyerere, Baba wa Taifa letu.

Kafanya mengi hakika, hauyapati kwa namba,
Machache tumeyashika, na tuyafunge kwa kamba,
Yasije kutuponyoka, tukakosa cha kutamba,
Namkumbuka Nyerere, Baba wa Taifa letu.

Kwa lugha alituunga, tusiwe na ukabila,
Udini aliupinga, ubaguzi nao utatula,
Umoja tumeujenga, nchini kila mahala,
Namkumbuka Nyerere, Baba wa Taifa letu.

Ndiye aliyeongoza, tukayang’oa magugu,
Kazi tuliimaliza, bila kuleta vurugu,
Na amani imekoza, tunaishi kama ndugu,
Namkumbuka Nyerere, Baba wa Taifa letu.

Humchoki hotubani, asimamapo kunena,
Na mambo uchambuzini, alichambua kwa kina,
Ulimjaa kinywani, ucheshi wenye maana,
Namkumbuka Nyerere, Baba wa Taifa letu.

Mpenzi wa Kiswahili, muandishi wa vitabu,
Si kwa haya mawili, yawe ya sifa sababu,
Mwalimu mwenye akili, mwenye swali na jawabu,
Namkumbuka Mwalimu, Baba wa Taifa letu.

Nimpendelea haki, wanyonge wamkumbuka,
Kati ya waliobaki, ni nani atawashika?
Na kwao hawabebeki, imani zimewashuka,
Namkumbuka Nyerere, Baba wa Taifa letu.

Ni mchukiaji rushwa, walaji walimjua,
Heshimani utashushwa, mara akikugundua,
Kicheo hautovushwa, madaraka kuchukua,
Namkumbuka Nyerere, Baba wa Taifa letu.

Leo wanakula rushwa, waziwazi bila haya,
Taifa linayumbishwa, kwa zao tamaa mbaya,
Hawawezi wajibishwa, kwa fimbo wala kwa waya,
Namkumbuka Nyerere, Baba wa Taifa letu.

Nani kashika wasia, baba aliouacha?
Yupi anajivunia, aseme bila kuficha,
Wote aliowalea, sasa wameota kucha,
Namkumbuka Nyerere, Baba wa Taifa letu.

Miiko ya uongozi, wametupa jalalani,
Sera nzuri za uwazi, wamezifukia chini,
Wamekuwa mabazazi, utawajua nyusoni,
Namkumbuka Nyerere, Baba wa Taifa letu.

Hali mbaya ya maisha, kooni inatukaba,
Wao wamesababisha, lawama watazibeba,
Mwenye njaa nakumbusha, mjuzi aliyeshiba,
Namkumbuka Nyerere, Baba wa Taifa letu.

Katuachia urithi, uongozi ni hekima,
Wala katu si mirathi, inayoachwa na mama,
Kama mtamba hadithi, katufunza kuwa wema,
Namkumbuka Nyerere, Baba wa Taifa letu.

Mwandishi ni Ngonyani, mkono wangu wa chuma,
Kofi langu la shavuni, maumivu yatahama,
Usithubutu mtani, nitakutia kilema,
Namkumbuka Nyerere, Baba wa Taifa letu.

Shairi hili limetungwa na Mathew Ngonyani ‘Mkono wa Chuma’ anayepatikana kwa simu; 0713 974 828 au baruapepe: ngomathew80@yahoo.com.

Kutoka Tanzania Daima


Nyerere asimulia imani ya wazee kwa vijana

Katika kumuenzi Baba wa Taifa, leo tunawachapishia moja ya hotiba zake zilizowakuna wengi. Hii ni sehemu ya hotuba ya Julius Nyerere alipokutana na Baraza la Wazee wa Dar es Salaam, kuagana nao kabla hajastaafu urais. Ilichapishwa kwa mara ya kwanza katika gazeti la Radi, Toleo Na. 2 la mwaka 1986 lililokuwa likimilikiwa na Ndimara Tegambwage. Gazeti hili lilifutwa na serikali kwa madai kuwa lilikuwa halitoki kwa muda mrefu – Mhariri.

“MIMI nimeanza siasa na wazee wa Dar es Salaam; na wazee wa Tanzania. Nimeanza nao mapema sana; mapema kweli. Nilirudi kutoka masomoni, Uingereza Oktoba 1952 – miaka 33 nyuma. Wakati huo nikiwa kijana mdogo wa miaka thelathini na kidogo hivi.

Niliporudi nikakubaliana na wamisionari hapo Pugu (sekondari), nifundishe shuleni kwao. Lakini nikiwa shuleni – Chuo Kikuu – nilijua. Niliishaamua kwamba maisha yangu yatakuwa ya siasa. Niliamua hivyo: Nitafundisha kwa muda wa miaka mitatu, nione hali inavyokwenda na kuzoeana na wenzangu kabla ya kuanza maisha ya siasa.

Niliporejea nchini hapo Oktoba, nikaenda Butiama. Januari nikarudi Dar es Salaam. Nikaanza kazi. Nikataka kujua habari za African Association. Mzee Mwangosi anakumbuka. Yeye ndiye aliniambia habari za African Association. Aliisha niambia habari hizo tangu nikiwa Makerere – Chuo Kikuu – nikiwa mwanafunzi.

Pale, mimi na wanafunzi wenzangu tulikuwa tumeanzisha chama kinachoitwa Tanganyika African Welfare Association (TAWA) cha wanafunzi wa Tanganyika; mimi nikiwa katibu wao. Hapa tukaona mambo yanakwenda vizuri kidogo.

Tukaona kwanini TAWA iwe ya wanafunzi peke yao na siyo Tanganyika nzima. Kwa hiyo nikawaandikia baadhi ya watu Tanganyika. Nikasema, jamani ee, tumeanzisha chama, kwanini msianzishe huko matawi ya chama hicho?

Ndugu Mwangosi akapata barua hiyo. Alikuwa miongoni mwa waliopata barua hiyo. Akaniandikia – nikiwa Makerere – akasema: Wewe kwanini unataka kuanzisha chama kipya? Kipo chama. Kipo Chama cha TAA (Tanganyika African Association).

Kwa hiyo la maana si kuanzisha matawi, maana chama kipo na matawi yameenea; la maana ni kwamba hicho chama chenu mfute, na muanzishe tawi la Tanganyika African Association.

KUVUNJWA KWA TAA

Hivyo ndivyo tulivyofanya. Kwa hiyo mimi nikawa katibu wa katawi ka TAA hapo Makerere. Niliporudi Tabora na kuanza kufundisha pale St. Mary’s (sasa inaitwa Sekondari ya Milambo), nikachaguliwa katibu wa TAA wa jimbo ambalo makao yake makuu yalikuwa Tabora. Ulipofanyika mkutano wa TAA mjini Dar es Salaam, nilihudhuria nikiwa mjumbe kutoka Tabora.

Kwa hiyo nilikuwa naijua Tanganyika African Association. Nilipokuwa ninaondoka kwenda Ulaya kusoma, nilikuwa nimeishaonja shughuli za TAA. Sasa niliporudi, baada ya kukaa Pugu siku chache, nikaja mjini Dar es Salaam. Nikauliza nani wanaongoza TAA? Nikaambiwa kuna jamaa mmoja anaitwa Abdul Sykes. Sasa ni marehemu. Abdul ndiye alikuwa katibu wakati huo.

Nilipelekwa na Kasela Bantu - ambaye naye aliteleza-teleza na hatunaye hapa (kwenye mkutano). Kasela Bantu alikuwa mwalimu mwenzangu. Tulifundisha pamoja Milambo. Nilipokuja Dar es Salaam, nikakuta anafanya kazi Radio (Tanganyika Broadcasting Corporation). Ni Kasela Bantu aliyenipeleka kwa Sykes.

Wakati huo mambo yalikuwa yanasinzia kidogo. Kwa muda mfupi mwaka ule, tukafufua-fufua, hasa kutoka Januari. Kufika Aprili, TAA ikafufuka. Tukafanya mkutano hapo Anautouglou. Kwenye mkutano huu wakanichagua kuwa rais wao – wa TAA.

Ninasema yote haya kwa shukrani kwa wazee. Jamaa hawa walikuwa watu wazima wa Dar es Salaam, na mimi kijana mdogo Mzanaki, na Kiswahili changu si kizuri sana – cha matatizo.

Nimekuja, natoka Ulaya, tena masomoni. Muda mfupi tu jamaa hawa wakaniamini haraka sana – katika muda wa miezi mitatu. Wakanichagua Rais wa TAA. Hapo ndipo nilianza shughuli mpya ya kuandika katiba ya TAA na kuipa madhumuni hasa ya shabaha ya kuleta uhuru.

Baada ya miezi 13, hapo 1954, tukaanzisha TANU. Jina hili lilipendekezwa na kina Abdul Sykes. Walikuwa wamelifikiria tangu zamani, walipokuwa askari vitani huko Burma (Vita vya Pili).

WAZEE NA MSIMAMO

Miezi minne baada ya kuanza kazi Pugu nikawa ninakuja Dar es Salaam, kwa mguu; kila Jumamosi. Baadaye wazee wakanipa baiskeli nikawa ninakuja mjini kukutana na wenzangu; kufanya mikutano.

Hivyo ndivyo tulivyofanya. Wazee wakaniamini upesi sana. Tukawa na uhusiano mkubwa sana. Wadogo wenzangu wengine walikuwa Abdul Sykes, Abass Sykes (mdogo wake), Dosa Aziz – waliokuwa wengi ni wazee.

Katika kuhutubia mikutano yangu, nilikuwa nikisema: Wazee na ndugu zangu! Wazee hasa ndio walikuwa na mikutano ya awali ya TAA na TANU. Walikuwa na msimamo wa hali ya juu kabisa! Hawakuyumba hata kidogo! Vijana walikuwa na mashaka. Wengine walikuwa na vikazi vyao, waliogopa kuvipoteza.

Nalo jambo lenyewe ni la hatari – la kuzungumzia uhuru! Unaweza ukakosa kazi; na wapo waliopoteza kazi; wengine wakaacha kazi. Kina Rashid (Kawawa) waliona watoke kwenye shughuli hizo tuje tuungane katika chama.

Wazee wa Dar es Salaam, na baadaye wa nchi nzima, wakatuunga mkono, na kila nilipokwenda, watu wa kwanza walionielewa, walikuwa wazee.

Nilikwenda Songea mwaka 1955 mara baada ya kujiuzulu. Huko wazee walinipokea na kunielewa. Nilianza safari za kuitembelea Tanganyika nzima. Nilikwenda Mbeya. Mkutano wangu niliufanya na wazee; kikundi kidogo cha wazee, ndani ya nyumba ya mtu.

Kwa mkutano huu wa Mbeya, wazee wakauliza: Unatafuta nini? Nikawaambia natafuta uhuru. Wale wazee, kwa sababu ya vita vya Maji Maji, na wanakumbuka, kabisa, wakaona mimi ninatafuta jambo la hatari. Tulifanya mkutano wa makini kweli. Wakauliza: Wewe unawezaje kuleta uhuru? Wewe una njia gani kudai uhuru na usitiwe kitanzi na Waingereza?

WAINGEREZA WAONGO

Tulielezana. Nikawaambia ninyi wazee, Waingereza wanawadanganya, Waingereza wametumwa na ule Umoja wa Mataifa uliokufa (League of Nations), waje kuishika Tanganyika kwa muda tu; watusaidie, na wakati tutakapokuwa tayari, watuachie tukajitawale.

Waingereza wanafanya ujanja; hawasemi. Vita vimekwisha (vya Pili) na Umoja wa Mataifa mwingine – mpya (United Nations Organisation – UNO) umewakabidhi Tanganyika kwa shabaha ileile. Sisi siyo koloni lao. Wamepewa dhamana tu.

Kwa hiyo nikawaambia wazee, hakuna haja ya kumwaga damu. Tuwaseme tu! Tuwashitaki kwa waliowaleta hapa kwamba hawafanyi kazi yao; wamesahau kabisa!

Wazee wakauliza: Eh, inawezekana? Nikasema inawezekana. Kazi yetu ya kwanza ilikuwa kuwaambia watu kwamba uwezekano wa kujitawala upo. Hilo lilikuwa la kwanza. Wazee walijua maana ya kujitawala. Walitamani kujitawala, lakini hawakujua waanzie wapi.

Vijana hawakuwa na habari kwamba kujitawala kunawezekana. Kwa hiyo kwa wazee sikuwa na matatizo. Wao hawakuwa na kazi; hawakumwogopa Mwingereza. Hawakuogopa kufukuzwa kazi. Baadhi walikuwa wafanyabiashara.

Mzee John Rupia (marehemu) alikuwa mfanyabiashara na kaidi (mkaidi) kidogo. Aliwahi kutishwa na kunyang’anywa leseni yake ya biashara. Akaambiwa akiendelea kushirikiana na kijana mwenda wazimu (Julius Nyerere), atanyang’anywa leseni moja kwa moja. Rupia aliwajibu: Potelea mbali!

Nasema yote haya ikiwa njia ya kutoa shukrani kwa wazee na imani yao kwa vijana wakati huo.

Imani hujenga imani. Na mambo haya makubwa ya nchi, kama hayana baraka za wazee hayaendi. Magumu sana. Wanasema ngoma ya watoto haikeshi! Mimi nilipata baraka za wazee tangu zamani. Tangu awali kabisa.

TWINING AMEKWISHA

Siku moja, Dosa akanifuata Magomeni (Dar es Salaam). Akasema: Leo wazee wanakutaka. Wapi? Kwa Mzee Jumbe Tambaza. Wanakutaka usiku. Nikasema haya, nitakuja. Nikaenda. Nikakuta wazee wameshakaa; wameniita kijana wao kuniombea dua. Mimi Mkristo, wao Waislamu watupu. Wakaniombea dua za ubani. Tukamaliza.

Tulipomaliza wakasema kuna dua pia za wazee wao. Basi wakanitoa nje. Tukatoka. Zilipomalizika zilikuwa za Kurani; sasa zikaja dua za wazee – za jadi.

Walikuwa na beberu la mbuzi. Wamechimba shimo. Wakaniambia simama. Nikasimama. Beberu akachinjwa, huku anaambiwa, “Twining (Twainingi) umekwisha!” (Edward Twining alikuwa gavana wakati huo). Ndipo nikaambiwa: Tambuka! Nikavuka lile shimo. Hapo nikaambiwa na wazee: Basi nenda zako; tangu leo Twining amekwisha!

Sasa mimi Mkristo; hao Waislamu. Na mimi mkorofi-korofi katika mambo haya (ya kutambika). Lakini tulikuwa tunaelewana na wazee wangu hao. Kwa hiyo nilitambuka pale na kuambiwa: Nenda nyumbani salama. Twining hawezi tena!

Wazee wangu wengine wanakumbuka tulikuwa tunakwenda Bagamoyo. Kwenye makaburi kule! Tunapiga dua huko kwenye makaburi na wazee wangu.

Baadhi yetu mtakumbuka safari moja jamaa wa Kenya, hawa kina Tom Mboya (marehemu) walishitakiwa. Tukasema tuwasaidie. Tuwasaidie vipi? Tukasema tufunge. Tukaomba nchi nzima kufunga siku hiyo. Tufunge! Tukafunga. Hakuna kula. Na siku ya kufunga tulikuwa na mkutano Bagamoyo. Tukaenda huko. Tukafanya mkutano hadi saa 12 jioni.

Baada ya mkutano tukaenda nyumbani kwa mzee Mohammed Ramia (marehemu). Hapa ndipo tulikuwa tumefikia. Mimi nikamuuliza mzee: Sheikh, una Aspro? Akajibu: Kwa nini unataka Aspro? Nikajibu kuwa kichwa kinaniuma kwelikweli. Akasema subiri.

Tulisubiri hadi saa ya kufuturu. Tukafuturu vizuri. Mzee Ramia akaniuliza: Bado unataka Aspro? Nikajibu kichwa sasa hakiumi. Kumbe ilikuwa njaa.

Nawaelezeni haya kwa sababu huko tulikotoka, tulishikamana sana. Tulishirikiana sana na wazee.

Kutoka: Tanzania Daima



Angalia viungo hivyo hapo chini, ilikuwa ni baada tu ya Mwalimu kufariki.

http://www.anc.org.za/ancdocs/history/people/
nyerere/newsart.html

http://www.utamaduni.dk/news/nyerere.htm#profil

http://www.sardc.net/nyerere/comm-stmt.html

http://news.bbc.co.uk/1/hi/world/africa/474637.stm

http://news.bbc.co.uk/2/hi/africa/463136.stm

http://www.cnn.com/interactive/specials/9912/
yearinreview.passages/content/politics/nyerere.html

http://www.kwenu.com/profile/nyerere.htm

http://www.utamaduni.dk/news/nyerere.htm

http://african.lss.wisc.edu/swahili/swahili_4/news/
nyrere_letters1/html/pages/kifo_cha_nyerere.htm

http://african.lss.wisc.edu/swahili/swahili_4/news/
nyrere_letters1/html/pages/mungu_amlaze_nyerere.htm

http://african.lss.wisc.edu/swahili/swahili_4/news/
nyrere_letters1/html/pages/namilia_nyerere.htm

http://www.anc.org.za/ancdocs/history/people/
nyerere/cosatupr991014.html

http://www.anc.org.za/ancdocs/history/
mbeki/1999/tm1018.html

http://www.tanemb.se/funeraarr.htm


No comments: