Binti wa Karume sasa auanika mtandao wa rushwa Kisutu.
*Adai haki inauzwa, wanyonge wanaonewa
*Akiri anajua ni msalaba mzito, lakini ataubeba
*Asema hana tatizo na Mahakimu, bali rushwa
*Asema mteja wake alitishiwa kwa kesi ya Babu Seya
Na Hassan Abbas
SIKU chache baada ya kutokea hali ya sintofahamu kati yake na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Kisutu, Bibi Addy Lyamuya, Wakili wa Kujitegemea ambaye pia ni binti wa Rais Amani Karume wa Zanzibar jana amefanya mahojiano maalum na gazeti hili na kusisitiza kuwa hana ugomvi na hakimu yeyote bali anapigania haki za wanyonge, wanaolazimika kununua haki kwenye mahakama hiyo.
Fatuma katika mahojiano hayo, amewabainishia Watanzania kuwa yeye kama wakili aliyefundishwa vyema maadili ya kazi yake na pia anayeenzi wosia wa babu yake, hayati Mzee Abeid Amani Karume, siku zote amefundishwa kupigania haki inapotaka kuchafuliwa na ubatili.
"Nilipoanza kulishughulikia suala hili, nilijua utakuwa msalaba mkubwa kwangu, lakini kama babu yangu alivyokuwa jasiri kiasi cha kuwaongoza Wazanzibar kupata haki zao, nami nimejifunza kutonyamazia uovu," alisema wakili huyo ambaye jana aliuweka hadharani mtandao wa rushwa ulioenea katika mfumo wa mahakama hasa kwa baadhi ya Mahakimu wa Mahakama ya Kisutu, Dar es Salaam na kuitaka jamii ilijadili tatizo hilo.
Chanzo cha yote
Anasema yeye kimsingi anaifanya kazi ya uwakili ikiwa ni sehemu ya wito wake binafsi aliokua nao tangu mdogo wa kutotaka kuona wanyonmge wanaonewa.
"Nilipoanza kazi hii nilikuwa natetea sana wanyonge hasa katika hizi kesi za madai na mambo ya ndoa, lakini nikaziacha na kujihusisha zaidi na masuala mengine," alianza kusema.
Akaongeza kuwa hata hivyo kutokana na kuwa na moyo wa huruma akajikuta akishindwa kukwepa kuwatetea wanyonge hao kila walipomfuata awasaidie.
"Hata hii kesi ilipokuja, kimsingi mteja wantu ni mtu wa kawaida, lakini nikajitoa kama sehemu ya wito wangu nimsaidie apate haki yake ya kuonana na mtoto wake mpendwa," aliongeza.
Wakili Fatuma akieleza msingi wa kesi hiyo, aliliambia gazeti hili kuwa inahusu baba na mama waliotengana ambapo mume ambaye ndiye mteja wake, aliiomba mahakama awe na fursa ya walau kuonana na mwanae kwa siku chache katika wiki.
"Nilimtetea katika kesi hiyo na Agosti 2, mwaka huu tukashinda. Hukumu ilimpa haki mteja wangu ya kuwa na mwanawe kuanzia kila Ijumaa kisha Jumapili awe anamrudisha kwa mama yake," alifafanua.
'Kansa' yaanza
Wakili Fatuma akiwa anaonekana mwenye huzuni, alisema wakati mteja wake akifuatilia hukumu hiyo ndipo alipoanza kuombwa rushwa ili hati ya hukumu yake isainiwe na akalazimika kutoa.
Anasema katika tukio la pili, baada ya kupewa hukumu yeye akiwa wakili alibaini kuwa mteja wake hakuwa amepewa hati ya amri ya mahakama na akamshauri aende tena Mahakama ya Kisutu kuiomba ili aweze sasa kuanza kupata haki yake ya kuwa na mwanawe.
"Alipofika kwa Hakimu akaambiwa alichotoa siku ya kwanza kilikuwa hakitoshi. Akajipapasa na kutoa alichokuwa nacho lakini bado akaambiwa hakitoshi.
"Hii ni aibu kwa taifa hili kwa msimamizi wa haki kufikia hatua anauza haki namna hii," alisema wakili Fatuma na kuongeza: "Yule mteja wangu akawa ameishiowa hela hivyo akamwomba rafiki yake aliyekuwa akisubiri nje ya mahakama amsaidie."
Akaongeza kuwa jamaa huyo alilazimika kwenda benki ya Barclays na kutoa dola 100 ambazo walimkabidhi Hakimu huyo.
"Huyu jamaa aliyekwenda kutoa fedha zake benki ili amsaidie mteja wangu, yupo na yuko tayari kutoa ushahidi," alisema.
Wakili Karume akieleza jinsi Mahakamu walivyofikia hatua ya kuwa na mtandao wa aina yake wa kudai rushwa na ambao unawakera wananchi wengi, anasema baadaye kesi hiyo ilichukua taswira nyingine tena kufuatia mawakili wa upande wa mke kuwasilisha maombi ya kutaka kesi hiyo ifanyiwe marejeo kwa kuangaliwa upya.
Anasema Hakimu huyo (jina tunalo), alimpigia tena simu mteja wake na kumtaka waonane kwenye hoteli ya Sea Cliff.
"Mteja wangu alisita kwenda kwa sababu alikuwa akijua huko angeendelea kuombwa hela zaidi. Hakimu yule akatuma hata sms (ujumbe mfupi wa maandishi) ambao tunao kama ushahidi akimsisitiza mteja wangu waonane," aliongeza.
Sea Cliff-Agosti 26, 2007
Wakili Fatuma anasema kuwa kabla ya kwenda kuonana na Hakimu huyo kwenye Hoteli ya Sea Cliff iliyoko pembezoni mwa Bahari ya Hindi jijini Dar es Salaam, mteja wake alimpigia simu na kueleza nia ya kutaka kumrekodi Hakimu huyo.
"Aliponieleza nia yake nikamwambia sawa, fanya hivyo kwa sababu hali ile iliendelea kumchosha mteja wangu," alisema wakili Fatuma.
Kitisho cha Babu Seya
Anasema wakiwa hotelini hapo bila Hakimu huyo kufahamu kuwa alikuwa akirekodiwa, alianza kwa kumrubuni mteja wa wakili Fatuma kwa kumshangaa anavyowalipa hela kwa watu wengine (mawakili) ambao alidai hawezi kumsaidia.
Katika kanda hiyo yenye urefu wa takribani dakika 12, Hakimu huyo pia katika mazingira mengine yenye utata, alisikika akimshawishi jamaa huyo aachane na suala la kutaka akae na mtoto wake kwani kuna athari siku atakazokuwa akikaa naye, anaweza kusingiziwa mambo kama yaliyomkuta Babu Seya.
"Hakimu yule anasikika mbali ya kudai hela akimtishia pia mteja wangu kuwa yanaweza kumkuta ya Babu Seya kama ataendelea kung'ang'ania kukaa na yule mtoto," alisema kwa uchungu wakili Fatma.
Hoi kwa wiki moja
Akizungumzia jinsi alivyostushwa na yaliyokuwa yakiendelea mara baada ya kupelekewa rekodi ile, wakili Fatuma ameliambia gazeti hili kuwa alipatwa na mshituko mkubwa.
" Nilipata 'broken heart' (jakamoyo), sijui unaweza kueleza vipi katika Kiswahili, lakini niliumwa sana na niliumia kiasi cha kushindwa hata kwenda ofisini kwa muda wa wiki moja.
"Nikajiuliza nafasi yangu ni ipi katika kusaidia suala hili?Nilijua pia kuwa hilo linaweza kunigharimu na ni msalaba mkubwa kwangu?Nikafikiria niliache,lakini nikajiuliza ni wanyonge wangapi wanalazimika kuinunua haki na nani ataibadili hali hii?
"Mimi nimefundishwa vyema sheria kule Uingereza, nayajua maadili yangu kama mwanasheria, nina moyo wa uchungu kama mwanajamii mwingine na pia hii kazi siifanyi kwa shida, ningeweza kukaa nyumbani, mume wangu akanilisha, lakini naifanya kazi hii kwa wito.
"Nilipoisikiliza ile sauti ya yule Hakimu anavyoomba rushwa kwa kujiamini, nilijua pia moyoni mwangu kuwa huu ni mtihani katika maisha yangu na haya yaliyotokea niliyawaza kabla," alisema.
Anasema rafiki yake mmoja ambaye kwa sasa ni wakili nchini Uingereza aliyekuwa hapa nchini ndiye aliyempa moyo kulisimamia kidete suala hilo na kutolinyamazia.
Kazi yaanza
Wakili Fatuma anasema baada ya kuamua kulisimamua suala hilo, alimpigia simu Hakimu husika na kumuuliza ni kwa nini alikuwa anachukua rushwa kwa mteja wake.
"Nilipoongea naye kwa simu awali tuliongea vizuri lakini nilipomgusia suala la kwa nini anachukua rushwa kutoka kwa mteja wangu na kumueleza ushahidi nilionao, alijifanya yeye si Hakimu wa Kisutu na akakata simu.
"Mteja wangu aliwasilisha malalamiko yake TAKUKURU. Nami sikukata tamaa nililifikisha suala lile tena kwa kumwekea rekodi ile aisikilize Hakimu Mkuu Mfawidhi wa Kisutu, Bw. Sivangilwa Mwangesi lakini nikashangaa Hakimu yule aliendelea kusikiliza kesi yangu na nyingine za wananchi wakati uadilifu wake ulishakuwa shakani.
"Mimi tulipokutana naye Hakimu huyo (anayetuhumiwa) mahakamani nikamwomba ajitoe katika kesi yangu kwa sababu tayari uadilifu wake ulikuwa shakani na kimaadili hakupaswa kuendelea kusikiliza kesi za wananchi. Alisita lakini nikasimamia hoja yangu na hatimaye akajitoa," alisema.
Mtandao wa njama
Wakili Karume anawahakikishia watanzania kuwa hakuwa na ugomvi na Hakimu Addy Lyamuya wala Hakimu mwingine wa mahakama hiyo, lakini anasema tangu kesi hiyo ilipohamishwa kutoka Hakimu mmoja hadi mwingine alikuwa akihisi maofisa hao wa mahakama kama vile wamechukizwa na vitendo vyake vya kufuatilia mambo kwa kina.
"Sijui nini kilitokea. Sikuwahi kugombana na Mahakimu awali kwa sababu uwakili sijaanza mwaka huu wala mwaka jana. Nahisi baada ya kuona ninasimamia haki ipasavyo, walikuwa na hali fulani tofauti dhidi ya kesi yangu," alisema.
'Tume' ya Kisutu
Akizungumzia ripoti iliyotolewa juzi na Mahakama ya Kisutu kuhusu sintofahamu iliyotokea, wakili Fatuma anashangaa kuona jinsi misingi ya asili ya haki yake ya kusikilizwa ilivyokiukwa.
"Sikuitwa kujieleza na hili linashangaza, kwani hata maelezo yangu ya maandishi niliyawasilisha jana (juzi) mchana wakati ambapo kumbe tayari Hakimu Mwangesi alikuwa akiongea na waandishi akitoa ripoti ya uchunguzi wake,sidhani hata kama alisoma maelezo yangu wala kuwaita mashahidi wangu.
Juzi Hakimu Mwangesi alisema hajapokea tuhuma za rushwa dhidi ya mmoja wa mahakimu wake na jana alipoulizwa kwa njia ya simu kuhusu suala la kutomsikilia wakili Fatuma Karume katika uchunguzi wake, alikiri kutofanya hivyo lakini akasema alitumia maelezo ya awali ya malalamiko ya wakili huyo.
Akizungumzia hilo Fatuma ansema: "Misingi ya haki za asili inaeleza bayana kuwa lazima uitwe na kujitetea dhidi ya tuhuma zako. Hili halikufanyika lakini pia nashangaa kwa nini hata nilipotoa tuhuma za rushwa, haukufanyika uchunguzi na wala sikuitwa kutoa ushahidi zaidi."
Anasema kwa uzoefu wake akiwa wakili, sehemu kubwa ya haki za wananchi inauzwa na kuitaka jamii isimame kidete kuibua maovu zaidi yaliyoko katika idara ya mahakama kwa sababu kama haki itauzwa hakuna thamani tena ya maisha ya mwanadamu.
"Wazee wetu, Mwalimu Nyerere na babu yangu, Mzee Abeid Karume walituasa sana kuhusu rushwa. Ni heri mtu ale rushwa sehemu nyingine lakini si katika sehemu ya utoaji wa haki kama mahakamani.
"Rushwa ikishamiri katika mahakama kuna haja gani ya watu kusomea taaluma kama sheria, Ni bora kesi zikasikilizwe Jangwani ambako watu watakuwa wakiweka dau kwa kutumia fedha ili wenye nazo washinde.
"Lakini kama kuna taaluma na misingi ya sheria inayopaswa kufuatwa, basi wananchi na vyombo husika viamke. Kuna mtandao mbaya sana wa rushwa katika mahakama hasa kwa baadhi ya Mahakimu wa Kisutu," alisisitiza.
Tuhuma za wakili Fatuma Karume kuhusu rushwa katika mahakama, zimekuja wakati pia ikiwa ni miaka takribani 11 sasa tangu ripoti mashuhuri ya Jaji Warioba, ilipobainisha kuwepo kwa vitendo viongi vya rushwa katika sehemu mbalimbali ikiwemo Idara ya Mahakama.
Wananchi mbalimbali pia wamekuwa wakilalamikia vitendo vya kukithiri kwa rushwa katika mahakama mbalimbali hapa nchini.
Katika mahojiano yake na gazeti hili hivi karibuni, Jaji Warioba alionesha kutilia shaka kama muongo mmoja sasa, ripoti yake imefanyiwa kazi katika kuwabana wala rushwa.
4 comments:
Wala hajaua professional yake popote, sana sana waaandishi wamempa jina na kumtangazia business, safi sana, nimempenda huyu dada yuko fit!!
Mwenye kulia na alie, binti kajitaidi kajiimarisha na kajitoa kimasomaso ili kutetea haki!!! sisi kama wazazi tunamuunga mkono, fikiria usiweze kumuona mwanao kwa muda mrefu halafu eti hakimu kwa sababu zake tu anasema haiwezekani mpaka tarehe anayotaka yeye, ingekuwa yeye ndo mwenye kutamani kumuona mwanae angeweza?
Hovyoooo!!!
JAMANI MBONA HAPA MNAMUONGELEA FATMA TU? TENA MBONA AMEKUWA NA SUBRA SANA? ME MTU AKINIONYESHA KIDOLE KUWA SINA AKILI NAMTIA KIBAO ILI ATIE AKILI, NA MBONA HAMUONGELEI HIZO RUSHWA ALIZOKUWA AKIZICHUKUA KWA MTEJA WA FATMA?
ME NINA MIKASA MINGI YA MAHAKAMANI JAMANI, SIMLAUMU HUYU DADA, KUNA ULASIMU SANA, YANI USIKUTE NA YEYE ALISHACHOSHWA NA MAMBO YA MAJAJI, FATMA KAZA BUTI, ONGEA HATA UKITAKA WEKA MHADHALA JANGWANI UTANGAZE, HAYA MAZEE YAMECHELEWA KUJENGA NYUMBA HUKO ZAMANI SIKU HIZI YANATATUFA KUJENGA KWA NGUVU KAZI KULA HELA TU ZA WATU..KUDADADEKI!!!
NA MSIMTAJE BABAKE HAPO, WALA HAKUWEPO MZEE WA WATU, NYIE MTAJENI FATMA TU, MAMBO YA MTOTO WA RAISI ONDOENI!! HAYO YOTE MADONGE TU, NA NYIE BABA ZENU WAWE MARAISI BASI
MKELEKETWA!!!
Fatma Karume is one of the best we have in our country and it is an honour to have her fight for our citizens' rights!
It is quite obvious the magistrates who are corrupt and sell the law / rights of people want to destroy her but some of us, the CITIZENS of our beloved country are there to back her up.
GO FATMA KARUME GO, let us fight the corruption and make sure people get their RIGHTS!
Tatizo sisi watanzania tumezoea sana mteremko, ata rushwa ni vile vile kama ugali wa kila siku tu. Ukishikwa na askari, si kwa ajili ya makosa kwenye gari yako lakini ni njaa zake tuu, vile vile system yote hapo tanzania. Hii kesi ni sawasawa na ukiwa na askari wa kulinda nyumbani, ungependa huyo askari alinde nyumba yako na ulale kwa usalama au askari mpumbavu anaye lala tu na akipewa hela na wezi aanze kuwa saidia wezi namna ya kuvunja nyumba yako. Huyo dada Fatma ndiyo kiboko yao, Fatma wachape viboko hawa sawasawa na tuwaondoe ugonjwa wa cancer mahakamani.
Post a Comment