Monday, November 26, 2007

Mjukuu wa Shaaban Robert Aendeleza Kiswahili London…

Wiki hii inayoanza leo Jumatatu 26.11.2007, hapa London, Dada Amina ataanza masomo rasmi kufundisha Kiswahili. Madarasa hayo yatakayokuwa ya bure halafu baadaye yaanze kuwa ya malipo kwa wananchi wa hapa Uingereza.

Amina Waziri.

Hadi juzi Jumamosi tunaelezwa wanafunzi ishirini tayari walishajisajili kwa uchu na mate. Madarasa haya yatafundishwa kila siku katika Kituo cha Waafrika kilichopo New Cross, kusini ya London. Mtanzania Amina Waziri ni mtu wa kujituma sana…

Toka utotoni maisha yake yamekuwa yakusafiri safiri, kuhama hama, kutembelea sehemu kadhaa nchini Tanzania na dunia. Ukizungumza naye ni mtu anayejieleza vizuri, anayejua anasema nini, mwanamawasiliano. Hii ni kwanza kutokana na kazi ya baba yake mzazi, Mzee Waziri Juma aliyekuwa Waziri na Balozi wetu nchi mbalimbali. Mama yake Amina alikuwa binti yake mwandishi maarufu wa Kiswahili, Shaaban Robert. Kwa hiyo da Amina ana damu ya mwanafasihi na mmoja wa viongozi wetu mahsusi.Alizaliwa Tanga, tarehe 14 Februari, 1960 na kuanza shule ya vidudu Mbeya, darasa la kwanza Kaloleni Arusha. Toka hapo ikaanza sasa safari ya kusoma shule kadhaa (Tanga, Tabora, Dar es Salaam) akiongozana na wazazi waliokuwa katika wadhifa wa kiserikali. Akasoma China, Sudan hadi alipoingia kidato cha kwanza Shule ya Kisutu, Dar es Salaam, mwaka 1973. Baada ya kusoma shule kadhaa za sekondari (Korogwe, Sudan Sisters mjini Kahrtoum) alimalizia kidato cha nne shule ya Ifakara mwaka 1978. Miaka kumi na tatu iliyofuata alifanya kazi ya mhudumu wa ndege (air hostess) shirika la Air Tanzania na kusafiri kila mahali Bongo na Afrika Mashariki. Aliishi pia Bujumbura, Burundi. Toka mwaka 1991 anaishi London, mzazi wa watoto tisa (walio hai watano) na wajukuu wawili. Keshafanya kazi za mhudumu wa mahoteli, dereva wa teksi, mwangalizi wa wazee na watoto na kufuzu diploma ya Theolojia na Nasaha (counselling) na kuchapa kitabu chake cha kwanza mwaka jana kiitwacho : “Oneness.” Kitabu hicho chenye picha ya marehemu binti yake Comfort (aliyefariki mwaka 2002) kinaelezea harakati za mwanamke wa Kiafrika kupambana na maisha na kuyamudu.Nilimhoji Amina karibuni baada ya moja ya safari zake nyingi kwenda nyumbani. Haya hapa mazungumzo yetu.

FM : Ulikuwa nyumbani karibuni. Je, ulikwenda kufanya nini?

Amina: Hususan na lengo la safari yangu ya nyumbani hivi karibuni ni mshawasha na mwamko wa kufanya kazi za Mungu, na pia kwenda kufanya utafiti nitaweza kufanya nini ili nitoe mchango wangu katika kuwasaidia wapendwa wananchi, na vile vile kwenda kuwaona ndugu wazazi na marafiki .

FM: Mwaka jana ulikwenda nyumbani pia. Tueleze tofauti ya uliyoyaona mwaka jana na mwaka huu.

Amina: Naam, mwaka jana mwezi wa Agosti nilienda kwa mara ya kwanza baada ya miaka 16 tangu nilipoondoka tarehe 13 Machi 1991, tofauti niliiyoiona hapo na safari hii ,ni kubwa. (kicheko) Mwaka huu nimeona kuna mwamko mpya wa kimawazo, nadharia, na pia kimaendeleo, labda pengine ni kwasababu wakati huu nilikuwa katikati ya mji, ambako niliweza kuonana na watu wa tabaka mbalimbali, wengi walikuwa na ari ya kimapinduzi, ya kimaendeleo, na wala hawakuwa na mcheche wa kutaka kutika nchini, zaidi walisisitiza ushirikiana kati ya waliopo nje ya nchi na wao ili kuleta sura mpya ya maendeleo.

FM: Kuna ugumu gani wa maisha kwa Wabongo kwa jumla?

Amina: Watanzania , kama , watu katika nchi yeyote changa bado wapo kwenye hali ya kuvuta hatamu, hali hii ni ngumu na ya utata, hasa wakijilinganisha na mataifa makubwa, hivyo bado sana , katika sera nyingi bado watu wana sita sita, hii ni hali ya kawaida kabisa katika hatua za maendeleo, bado watu wanashindwa kutoa mawazo yao bila woga, hii inasababisha masahihisho kushindwa kufanyika, na maendeleo kuzorota, laiti , wananchi wengepewa mwanya wa kidemokrasia , kutoa mawazo yao , bila kuvunja sheria wala heshima, nina hakika tungekuwa mbali. Kiuchumi, kiafya, kisiasa,kinadharia, kimawazo nk.

FM: Kuna urahisi gani wa maisha kwa jumla kwa Wabongo?

Amina: Watanzania , ni miongoni mwa mataifa machache ulimwenguni yenye sifa ya uadilifu na utulivu, sifa ambazo ni ngumu kuzikuta kwingi duniani. Kuna amani ya pekee, muda wote nilipokuwa nyimbani, sikusikia lugha chafu, sikusika mikimiki ya mwizi kukimbizwa, hata kwenye sehemu ya kuuza pombe sikuona maajabu yeyote, ya kushangaza, nidhamu ya vijana na watoto, ndio usiseme, ukweli ni kwamba Tanzania tunastahili hongera. Pia watu ni wakarimu na waaminifu na vyakula ni vingi na bei zake ni safi kabisa, nilishangazwa na ubora wa mbao na ujuzi wa maseremala , hasa magereza, na ujenzi wa nyumba bora na nzuri.

FM: Nini mustakbala wa maisha? Je, kuna matumaini gani?

Amina: Watanzania wakipewa sauti ya kusema wanataka nini wafanyiwe, kama nyumba bora, maji safi, umeme bila mikato, kazi za kudumu, mashule mengi ya fani mbalimbali, mahospitali na zahanati, barabara nzuri, sehemu za bustani wazi, maduka yenye bidhaa zetu wenyewe za ubora na bei nafuu, teknolojia mbalimbali,Tanzania itashinda na itakuwa taifa la mfano bora kama mengi duniani sababu tunao watu wenye sifa za kiutu na uaminifu na bidii ya kazi.

FM: Wewe unataka kufanya nini kusaidia nchi yetu na watu wetu?

Amina: Freddy, nataka kufanya kila kitu kuisaidia nchi yangu, na watu wangu, nipo katika harakati za kukusanya nguvu hapa na pale, nataraji kuanzisha vituo vya mafunzo hasa kwa wale ambao wamekumbwa na maafa ya maisha , kama, wajane, wafungwa, wazee, vilema, tayari nimeona kuna mashule mengi ya watu binafsi, lakini akina kabwela hawana namna ya kuzigusa, na wafungwa ndio wannanisumbua sana roho yangu, maana wengi wakitoka jela ndio hivyo tena, hawana chao; washaathirika, kila wanapokwenda hawana msaada wowote,majina yao tayari yameshaingia dosari, na wajane pia, wana tabu kubwa, hivyo nataka kufanya kitu kwa wasiojiweza..

FM: Suala la wanawake. Unaonaje maendeleo yao ukilinganisha enzi zile ulipokuwa ukiishi Bongo na sasa?

Amina: Kina mama Bongo wanastahili sifa na hongera, kote vijijini na mijini, wao ndio wameshika hatamu, wengine wachuuzi, wengine wafanya kazi, na hata wale kina mama wanaopiga uasharati ,ili wapate riziki, pia wanaangalia familia zao vizuri sana, naomba usinielewe vibaya, si kama naunga mkono zoezi hilo, la hasha, lakini, kama ukiwakuta makwao , kamwe huwezi kujua kama wana tabia hii, maana wana beba majukumu ya familia yote. Enzi zetu bongo, wanawake walikuwa na woga na waliachia waume wawafanyie mambo mengi. Lakini sasa hata kina mama vijijini wanataka kwenda shule kupata ujuzi.

FM: Umeanza kufundisha Kiswahili hapa London. Nani wanafunzi wako na unaionaje kazi hiyo?

Amina: Wanafunzi wangu wengi ni kutoka visiwa vya Karibi: Jamaika, Trinadad- Tobago, St Lucia, St Vincent, Guyana, Kyuba, Grenada, St Kitts, na hata Waingereza ambao wanataka kuja kufanya kazi Tanzania. Pia baadhi ya Waafrika ambao wanapenda kujua lugha yetu.Naipenda sana kazi hii maana inanipa amani na kuona kwamba ninaweza kutoa mchango wangu kwa wengi , hasa , Wakaribi ambao wana kiu cha kutaka kujua lugha ya asili ya mtu Mweusi. Suala la utumwa limewatia pengo, wanaona wameibiwa silaha ya lugha, kwani lugha ni amana kubwa.

FM:Je, Kiswahili kinapendwa na watu wa aina gani ughaibuni, hususan Uingereza?

Amina: Cha kufurahisha sana ni jinsi ambavyo lugha yetu inapendwa sana, hasa na Waingereza, labda kwa vile hawa ni watu ambao kwao kitu chochote kina thamani kubwa, na kama nilivyosema awali wenzetu Wakaribi, wako radhi kulipa chochote wajue Kiswahili, na hasa jamii hii ya watoto waliozaliwa huku, ambao hawajui lugha nyingine zaidi ya Kiingereza, wanapenda sana nao wajidai eti tu waaongee Kiswahili , mradi tu wawakoge wenzao.

FM:Je, unaonaje maendeleo ya lugha ya Kiswahili hii leo nyumbani?

Amina: Nilichogundua , ni kwamba lugha yetu imechuja, imejaa maneno duni, wala siyo katika msamiati wa fasihi, hata kule kwetu Tanga , nilishangaa kuwaona watu wamekitia Kiswahili maji, sio tena kile Kiswahili cha awali, enzi za mababu na mabibi zetu.

FM: Vijana kwa wazee wengi wanaanza kutumia lugha ya mseto “usio na mguu wala kichwa.” Kuna desturi hii leo ya kuchanganya sana Kiswahili na Kiingereza. Lugha haileweki kama ni Kiswahili au Kiingereza. Vijana hawajui Kiingereza wala Kiingereza. Je, nini maoni yako?

Amina:Twaweza kupiga msasa, lakini tuzingatie kuwa ligha za miji mkikubwa huwa ni za barabarani, hata Kiingereza, Kiarabu, Kihindi nk, lakini, ile lugha ya mashuleni, vyuoni, serekalini, isitiwe dosari, huo ni urithi wetu, lazima tuuhifadhi kwa udi na uvumba.

FM:Unatukuza sana dini ya Kikristo. Nini nafasi yake kwa watu wetu duniani?

Amina: Kweli namtukuza sana Yesu Kristo, na kweli nampenda mno maana, aliuacha mbiguni ufalme wake uliotukuka , akaja duniani kudhalilika kwa kila mtu, ili afungue lango kuu la pepo, alicholeta Yesu. Hakuna mwingine yeyote awezaye kuleta ni kusameheana au msahamaha. Hakuna, katu katu, binadamu awezaye kusamehe, ila yeye tu, wote tuna magutu, japo tunadai tumesamehe na tumesahau, lakini ukiguswa tu yote yanarudi kama wimbi, na kisasi juu, ndio maana namfuata Yesu, ili nami niweze kusamehe, nimwangalie yeye tu, maana yeye ndie njia, ukweli na maisha ya milele.

FM:Kumekuwa na kukosoa Waafrika kuwa tumeacha dini zetu na kuiga dini za kigeni (Uislamu na Ukristo). Wasanii kama Fela Kuti wa Naijeria, walidai Waafrika tunajidunisha kwa kuabudu dini zilizoletwa na watu wa tamaduni nyingine. Tunajidunisha na kukopi nje. Nini maoni yako.

Amina: Kumkana Yesu ni kujikana wenyewe, nani aliezaliwa bila najisi isipokuwa Yesu? Na nani aliekufa akafufuka ila Yesu? Tena kabla ya kufufuka aliekwenda jehanamu kuhubiri Injili, ili kutoa nafasi nyingine, daima!

Kutoka: Freddy Macha´s Kitoto wordpress dot com

No comments: