WAINGEREZA wana msemo maarufu: You cannot eat your cake and have it.
Kwa tafsiri isiyo rasmi, msemo huu unaweza pia kuwa na maana ya ile hali ambayo, mitaani kwetu, huelezwa vizuri na maneno: “Huku wataka na kule wataka”. Yaani, hali ya kibinadamu kabisa, ya mtu kutaka kupata kila kitu, ama kufaidi pande zote.
Katika siku za karibuni tumeshuhudia maneno, na hasa minong’ono ambayo imekuwa ikidaiwa kuendelea ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ya kile ambacho unaweza kukieleza katika lugha ya kisasa: Nani zaidi.
Tumesikia huko nyuma kwamba yawezekana hata Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, mara kadhaa, amepata mawazo kwamba nafasi yake sasa inatishiwa. Zimekuwapo pia habari kwamba kuna mbio za kuwania nafasi ya ukatibu mkuu kati ya Katibu Mkuu wa sasa, Wilbroad Slaa na Naibu wake, Zitto Kabwe.
Kama ilivyo kawaida, hakuna ambaye amejitokeza kusema nini kinachoendelea kuhusiana na suala hili la wenye madaraka ndani ya CHADEMA. Hakika nitakuwa wa mwisho kuamini kuwa kutakuwa na mvutano wa kuwania madaraka ndani ya CHADEMA, na hasa wakati huu chama hicho kinapoonekana kuwa kinapanda chati.
Lakini pengine kinachozungumzwa sasa ndicho cha muhimu zaidi. Baadhi ya wana CHADEMA, tena wengine wabunge, wamejitokeza hadharani wakisema kwamba uteuzi wa hivi karibuni uliofanywa na Rais Jakaya Kikwete wa Zitto Kabwe kuingia katika Kamati ya Madini, hauna nia nzuri. Wanataka mbunge huyo asijiunge katika kamati hiyo.
Sasa hilo linashangaza kidogo. Na ndilo linalotufikisha kwenye hadithi ya keki ya Waingereza. Ni kweli CHADEMA na Zitto Kabwe ndio walioibua suala la mgodi wa Buzwagi bungeni. Ni kweli kwamba Buzwagi imekuwa ni biashara nzuri kisiasa kwa CHADEMA. Ni kweli kwamba chama hicho kimekuwa kikishinda pointi kutokana na hoja za Buzwagi, Richmond na Benki Kuu (BoT). Wananchi wamewaelewa kina CHADEMA na wanawashukuru kwa kuibua mijadala juu ya maeneo hayo. Wengi tumefunguka macho.
Sasa kwa nini wasisherehekee na kupongezana kwa ushindi huo mkubwa wa kisiasa, na badala yake waanze kunyoosheana vidole?
Inawezekana CHADEMA hawakulitarajia hili, kwamba baada ya mambo kukwama bungeni, basi, ingeundwa kamati, tena ya Rais, ya kutazama mikataba ya madini. Inawezekana CHADEMA walikuwa na mikakati mingine ya kuweza kung’ang’ania hoja ya Buzwagi ambayo sasa baada ya kamati kuundwa, imejifia - angalau mpaka ripoti itakapotoka.
Je, yawezekana labda CHADEMA inaona imepokonywa keki mdomoni?
Lakini hata kama ndivyo, si kuna bado mambo mengine lukuki ya uozo ndani ya Serikali yanayostahili kuibuliwa? Busara gani baadhi ya wana –CHADEMA kuanza, sasa, kumwandama Zitto ajitoe katika kamati hiyo katika kipindi ambacho CHADEMA nzima inapaswa kusherehekea ‘ushindi’ kwa kufanikiwa kumshinikiza Rais kuunda kamati hiyo?
Kwani wao walitaka nini hasa? Kwamba waendelee kupigia kelele suala hilo, na Rais akae kimya asifanye lolote? Na kama akifanya lolote, kama hili la kuunda kamati ya kuchunguza, basi, aliyewasilisha hoja binafsi bungeni kuhusu suala hilo (Zitto) asiingizwe kwenye hiyo kamati?
Na katika busara ya kawaida ni nani hasa anayeweza kunufaika na hatua ya namna hiyo? Ni CHADEMA kama chama? Ni Kikwete kama Rais wa nchi? Ni Bunge kama Bunge! Au ni umma wa mamilioni ya Watanzania wanaotaka kuujua ukweli kuhusu maliasili zao zinazomegwa kwa kasi na wageni kwa kushirikiana na watawala?
Lakini hata kwa busara ndogo tu; si kweli kwamba CHADEMA ndiyo itakayonufaika kwa kuwa na mtu wao mahiri (Zitto) ndani ya kamati hiyo atakayewaeleza ukweli wote wa kile kinachoendelea? Au wanataka kazi hiyo aifanye “Bwana Mapesa” wa UDP kwa niaba yao? Maana, na yeye yumo ndani ya kamati hiyo; japo chama chake hakikupata kulishikia bango suala hilo la Buzwagi.
Kama CHADEMA ni chama cha upinzani kinachotaka kukamata dola, basi, ni vyema kikaonyesha ukomavu katika kushughulikia masuala yanayogusa maslahi ya Taifa. Na maslahi ya Taifa si maslahi ya CHADEMA au CCM peke yake. Ni maslahi yetu sote.
Hata kama Buzwagi ilikuwa ni keki ya kisiasa kwa baadhi ya vigogo wa CHADEMA, ukweli ni kwamba imeshamegwa; na hivyo hawawezi kubakia nayo kwa ukubwa ule ule!Toka Raia Mwema.
No comments:
Post a Comment