Ayub Rioba.
TUNAFURAHIA mno vitu vya nje. Chochote kigeni tunakipokea na kukitukuza. Tunalamba miguu na nyayo za wageni. Tunaishi kwa mila zao, imani zao, lugha zao, tamaduni zao, majina yao na vitu vitu vyao. Hatujui chetu ni kipi. Tumeacha vya kwetu vya msingi. Ndivyo nilivyojaribu kuhitimisha safu hii juma lililopita.
Maelezo ya tabia hii yanaweza kupatikana katika matukio muhimu ya kihistoria yaliyoanza karne ya nane hivi. Zipo kumbukumbu zinazoonyesha kwamba Waarabu na Wachina walikwisha kuanza biashara na Afrika Mashariki mapema katika karne ya nane.
Katika mwaka 1415 Wachina wakiwa na majahazi yao walitia nanga pwani ya Afrika Mashariki na kuondoka na mnyama, twiga, ambaye walimshusha Beijing.
Kwa mfano, mwaka 1436, majahazi yaliyoongozwa na Mreno Affonso Goncalvez Baldaya yalitia nanga Afrika Magharibi. Affonso aliwaamuru vijana wake wawili (wenye umri usiozidi miaka 17) kupanda farasi na kuelekea nyikani ili wavumbue kulikuwa na nini au watu wa aina gani kule.
Vijana wale wa Kireno walipanda farasi kila mmoja na wakaanza kuingia nchi kavu wakifuata ukingo wa mto, ambao Wareno waliamini ulikuwa na dhahabu tele.
Baada ya kutembea kilometa kama 35 hivi ndani ya nchi kavu, vijana wale wa Kireno walikutana na kundi la vijana 19 wa Kiafrika. Vijana wawili wa Kireno, inaelezwa, waliwashambulia wale Waswahili ambao walikuwa na vimikuki vyao hafifu na kuwasambaratisha.
Waswahili wale, inaelezwa, walitimka mbio na kutokomea katika mapango waliyokuwa wakiyatumia kujihifadhi.
Mfano huu unadhihirisha kwamba Waswahili walipomuona Mzungu akiwa juu ya farasi akiwafuata kwa ujasiri akiwa na jambia lake linalong’aa waligwaya. Jinsi vijana wale wa Kireno walivyowaelezea Waafrika wale, utadhani walikuwa wanamzungumzia ngochiro au ngiri.
Lakini cha muhimu kuliko vyote katika mahusiano ya awali kati ya Afrika na wageni ni jinsi wenzetu walivyokuwa wakituelezea tulivyo. Wapelelezi wengi toka Ulaya walirejesha nyumbani kwao ripoti za ajabu kuhusu jinsi walivyotuona sisi Waafrika. Kwa mfano, msafiri na ‘mgunduzi’ mmoja Pliny katika machapisho yake aliyoyaita Summary of the Antiquities and Wonders of the World aliwaelezea Waafrika aliowaona kama ifuatavyo:
“...Wengine (watu weusi) hawana pua wala matundu ya kupumulia; uso mzima umejaa kama papai. Wengine hawana midomo ya juu; wengine hawana ulimi wanaongea kwa ishara; na wana kitundu kimoja usoni cha kupumulia na ambacho pia hukitumia kunyewa maji;...
Wapo pia Waarimaspi (Watu weusi) ambao huwa na jicho moja katikati ya paji la uso; Waagriphagi wao hula nyama ya simba na Waanthropomphagi ambao huishi kwa kula nyama ya binadamu; Wengine wanaitwa Wagamphasante na hutembea uchi kama wanyama.
Wapo pia Wacinamolgi ambao vichwa vyao ni kama vya mbwa vile; wapo pia Wablemys ambao wao hawana vichwa kabisa, ila macho na midomo vipo kifuani. Wapo pia Waswahili ambao hutembea kwa kutumia mikono na mguu kwa pamoja...”
Hivyo basi kwa kipindi chote ambacho wapelelezi, wafanyabiashara (ikiwemo ya Utumwa), wamissionari na hata wakoloni waliendeleza mahusiano na Waafrika, waliendelea kututazama kwa mantiki ya sura iliyojadiliwa hapo juu. Juma lililopita niligusia suala la sura ya Waafrika inayoonyeshwa katika chaneli za vituo vikubwa vya televisheni duniani. Ni ile ile ya karne ya 15 ya wale vijana wawili wa Kireno.
Wakati Wareno wanaanza biashara katika sehemu kadhaa za Afrika walikuwa wanatafuta dhahabu na vito vingine vya thamani; malighafi za biashara na baadaye watumwa. Walipoanza kukamata watumwa, kumbukumbu zinaonyesha kuwa wapo Waafrika waliopinga.
Waliopigana kufa na kupona wasichukuliwe na wageni. Wareno wakagundua njia rahisi ya kuwakamata Waafrika bila vurugu wala makeke. Dawa, kwa kuanzia, ilikuwa ni zawadi. Zawadi kama shanga, kioo cha kujitizama, mvinyo wa kwenye chupa, nguo za kutoka ulaya na vitu vingine vya urembo. Hili linaweza pia kusaidia kuelezea ni kwa nini ufisadi ni sehemu kubwa ya maisha yetu hadi leo.
Zawadi hizi zilitolewa kwa watawala wa makabila ya kule ambako walizifurahia sana . Kwa zawadi ambazo mathalan leo hii zisingekuwa na thamani ya shilingi laki tano za Tanzania , watawala (Watemi) wa Kiafrika walichekelea hadi magego yote yakaonekana. Kwa vijizawadi hivyo, walikuwa radhi kuachia kiasi kikubwa cha dhahabu, vito vingine vya thamani na hata watumwa kwa wafanyabiashara wa Ulaya.
Mara mzungu alipotambua tu kwamba Mswahili alichohitaji ni vijizawadi zawadi - hasa vidude dude vya kutoka Ulaya – na kwamba akishapewa vitu hivyo tu yu radhi afanywe chochote; basi walihitimisha nadharia muhimu katika historia ya mahusiano kati yao na sisi hadi hii leo.
Wareno wa kwanza kwanza kufanya biashara ya utumwa Afrika Magharibi walianza kwa kuvizia na kushambulia kisha kuchukua watumwa wa Kiafrika. Lakini mara tu walipojenga kituo cha biashara hiyo katika kisiwa cha Arguim, Afrika Magharibi, Waafrika wenyewe walianza kufanya kazi ya kusaka, kuvizia na kukamata Waafrika wenzao ili wawauze kwa Wafanyabiashara wa Kireno.
Farasi, ambaye kwa wakati huo alikuwa ni chombo muhimu cha usafiri, akatumika kama fedha ya kununulia watumwa.
Alvise da Ca’ da Mosto mfanyabiashara wa Venice aliyesafiri na mabaharia wa Kireno kwenda Afrika Magharibi aliandika hivi: “Watawala katika nchi ya watu Weusi wako tayari kukupa watumwa kati ya 10 na 15 ukiwapa farasi mmoja tu.”
Inasemekana watawala wa kabila la Jolof na watu wa tabaka la juu ambao walimiliki Savannah na maeneo makubwa ya kilimo kusini mwa Mto Senegali walipenda sana kumiliki farasi kama njia ya kuwakoga wengine kwamba wao wako matawi ya juu. Wiki ijayo tunaendelea na mjadala wa chanzo cha matatizo ya Waafrika.
ayubrioba@hotmail.comKutoka Raia Mwema
No comments:
Post a Comment