Thursday, November 22, 2007

Chetu Chao na Chao Chao!

NAAMINI katika dhana kwamba sisi ni viumbe wa Mola aliyetuumba. Napinga pia mfumo kandamizi unaowatukuza na kuwabagua watu kwa misingi ya rangi, dini, umri, uwezo, mali, elimu na umbile.

Naamini nia ya Mwenyezi Mungu kutuumba mataifa mbalimbali ilikuwa ni nzuri. Akiwa huko aliko, anafurahi kuiona bustani nzuri ya watu wa kila rangi, kama rangi za upinde wa mvua. Kwa hiyo napinga kabisa taifa moja kujiona ni bora zaidi katika kila kitu kuliko mengine.

Wanasema maendeleo katika habari, mawasiliano, sayansi na teknolojia yamefanya dunia iwe kijiji kidogo. Kwa kiasi fulani, hayo ni kweli. Lakini ukichunguza kwa makini, utabaini kwamba katika kijiji hicho kidogo kuna kiranja au kaka mkubwa ambaye wakati wowote anatuangalia. Yeye ndiye anayedhibiti ulinzi na usalama wetu, anatuamulia sera zetu za kilimo, afya, elimu, anatuchagulia marafiki, kwa jumla tumemwachia kazi ya kufikiri yeye.

Ndiyo maana leo popote utakakoenda, utakuta vijana wanafurahia mambo yanayofanana iwe muziki, chakula, mavazi au kukaa kijiweni bila kazi, na kuwaza namna ya kushinda bahati nasibu na kuwa na jumba kubwa au gari.

Hali hii haikutokea kwa bahati mbaya, ni programu ya makusudi iliyopangwa katika kipindi cha muda mrefu kwa kupitia matangazo ya biashara, filamu, michezo na sasa mashindano ya ulimbwende. Ndiyo maana vijana ni kizazi kipya kinachokwenda na wakati.

Wanaposema biashara imechanganya wanamaanisha wameliteka soko la vijana. Ni kijana gani hataki kuvuta sigara naye awe mtanashati? Hata kama hataki, lakini kila kona anakuta mabango yanayomhamasiha na kumshawishi awe teja wa sigara tangu mdogo ili awe mteja wa kudumu wa bidhaa hiyo.

Kijana gani hatamani kunywa pombe, kula chips na kuku kila siku, aendeshe gari, avae mitindo mipya ya kimataifa na kuwa kizazi kipya? Sasa tunashangaa na kulalama nini vijana wetu wanapopotea, hawaeleweki, ni kama vile si watoto tuliowazaa.

Hebu fikiria, Serikali iamue kusitisha uagizaji wa bidhaa za anasa kutoka nje, au iwekee kodi kubwa katika nguo zinazotoka nje ili tununue zetu, itakuwaje? Naamini nchi haitakalika si vijijini wala mijini, kwa vile tumekwisha kuwa mateja wa bidhaa na mtindo wa maisha wa wengine.

Tumekwisha kulambishwa utamaduni wa nje na kuwa watumwa kiasi cha kusifu bidhaa za nje, na kuchukua maadili na vionjo vya wengine kuwa ndio kigezo cha mafanikio. Kwa kufanya hivyo tunawatengenezea ajira watoto wa wenzetu, kisha tunalalama, sisi ni fukara, hatuna ajira!

Katika miaka karibu 15 ya mashindano ya ulimbwende Tanzania, tumeshuhudia changamoto nyingi zikijitokeza. Kwa muda mrefu Watanzania wengi hawakuona faida yoyote katika mashindano haya.

Baadhi tuliunga mkono au kuyapinga kwa sababu mbalimbali, lakini fahamu ndiyo zinatujia sasa kwamba utandawizi ndio umekamilika na umefika nyumbani sasa. Wanaume wetu ndio wamekwisha kukombwa; hujawa nadhifu, kama hujavaa suti hata kama jua kali kiasi gani!

Kwa miaka mingi wazalishaji wa nguo wameshindwa kuingia kwenye soko letu la nguo hasa la wanawake kwa sababu hatuna vipimo vinavyotabirika au kufanana. Jambo hili ni tatizo kwa sababu ama utakuta mwanamke wa Kiafrika ana matiti makubwa, au tumbo kubwa, au matako makubwa! Pia wanawake hao wengi hawana uwezo wa kuagiza nguo maalum kwa ajili yao.

Lakini sasa mashindano haya ya ulimbwende yamefanya wasichana wengi wawanie kuwa na inayojulikana kama “English figure”; yaani uwe mwembamba, mrefu, mweupe, miguu mirefu na nywele ndefu hata zikiwa za bandia. Ukiwa na umbile hilo basi angalau unakuwa na matumaini kuwa unaweza ukaukwaa u miss, au ukatokea kwenye magazeti ya mitindo.

Sasa hivi Afrika iko tayari kupokea mitindo ya nguo kutoka kokote duniani. Nguo hizo zitakuwa katika mitindo ya khanga, vitenge, batiki na vikoi.

Kwa hiyo mambo ya kutafuta fundi wa kushona nguo ndio kwa heri, ni majimama manene wachache tu labda ndio wataenda kwa fundi.

Si bahati mbaya kwamba Shirika la Biashara duniani limekazania kwamba ifikapo tarehe 31 Desemba 2007, ndio mwisho wa sera za kulinda soko la ndani dhidi ya biashara ya kimataifa.

Yaani kuanzia 1 Januari 2008, Afrika itaingia katika ushindani wa masoko kwa bidhaa zake sawasawa na wale waliotuchukua katika biashara ya kuuza na kununua watu, kisha wakatutawala na wanaendelea kutunyonya. Ukweli ni kwamba hii ni kashfa ya karne!

Kwa muda mrefu ukiwa mtu Mweusi na unakipaji kitakacho iletea sifa nchi yeyote, Ulaya na Marekani, hasa katika michezo au sanaa unaweza ukapata “uraia” wa nchi hizo kwa urahisi. Michezo na muziki sasa hivi ni tasnia zinazotengeneza pesa, na ndizo zinaongoza katika kutumiwa kueneza utandawazi na kutufanya Waafrika tujihisi kuwa tunatendewa sawa na watu wengine.

Si siri, kama ningekuwa nimezaliwa na kulelewa Ulaya, China au India, na nikazungumza lugha zao kwa ufasaha, na kufuata mila na desturi zao, hayo yasingenifanya niwe Mzungu, Mchina au Mhindi. Kwanza watu wangeniangalia mimi kama mtu Mweusi, mpaka niwaeleze kuwa mimi ni mwenzao.

Tunapowaona wacheza soka Weusi katika timu ya Ufaransa, hawawezi kutulazimisha tuamini kuwa wao ni Wafaransa kwa kuwaangalia tu. Tunajua wengi wao ni biashara.

Wafuasi wa Marcus Garvey wanatafsiri utamaduni kuwa ni “ Njama, au mbinu inayotumiwa na kundi la watu kujiundia namna ya kufikiri, kutenda, kuamini na kuungalia ulimwengu ili waweze kuunda mwamko ambao utawasaidia kufanikisha mambo yao, ili waweze kusaidiana na kufaidika kama kundi, kwa vile hawawezi kufaidika wakienda mmoja mmoja. Kwa hiyo utamaduni ni chombo chenye nguvu na uwezo” Njama hizi unazikuta katika hali nyingi kama vile katika dini, kabila,itikadi za kisiasi, NGOs, sera za uchumi, NATO, hata Umoja wa Mataifa.

Kwa hiyo utamaduni na historia viko katika akili na miili yetu kama watoto mapacha. Swali kubwa kwetu ni tuna utamaduni wa Kiafrika au wa Kitanzania? Tuna utamaduni ambao unaangalia maslahi yetu kama Wafrika au Watanzania? Je, tuna taifa la Afrika na kwamba tunaamini kuwa sisi ni wamoja? Nini haiba ya Mwafrika leo hii, je imemezwa na ya Kizungu au Kihindi?

Wenzetu, kama Wazungu maslahi yao yanapotishiwa wanakuwa taifa, kwa hiyo wanakuwa na uwezo wa kutuweka pembezoni kwenye matukio au siasa za kimataifa.Wanauwezo wa kutufanya tuachane na haiba zetu tuwafuate wao kwa vile tayari ni taifa. Vipi tunashangaa kuwa tumechanganyikiwa? Tunashindwa kuukwepa utumwa.

Kwa hiyo Miss Tanzania anapokwenda China, macho ya wengi yatamwona msichana mrembo wa Kihindi, mpaka pale atakapojitambulisha. Lakini kwa macho ya walioandaa, watamnadi Miss Tanzania kama ushahidi kwamba, Tanzania ni nchi ya amani haina ubaguzi wa rangi. Wote karibuni, mje mjichukulie cho chote, ingieni katika ushindani wowote.

Huu ni mchezo wa kibepari, una sheria zake, kama hukubaliani nazo basi usicheze, hata kama uwanja wa mchezo uko sawa. Tulipokubali kubadili sera zetu za uchumi, chini ya maelekezo ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha (WB/IMF) katikati ya miaka ya 1980, tulikubali kufundishwa ubepari, na kuishi kwa sheria zake, chetu chao, chao chao! Mashindano ya Ulimbwende hayana uhusiano na Waafrika, ushiriki wetu unawafaidisha watu wengine.

Nani anafadhili mashindano hayo, kwa nini na anafaidika vipi? Kama ungekuwa nje ya nchi na unaangalia mashindano hayo bila shaka usingetambua kuwa ni ya Kitanzania. Kama unamfahamu mzee Rashidi Kawawa na mkewe, na vigogo wengine, ungesema labda walikwenda nchi fulani kuangalia mashindano hayo.

Kiongozi wa sherehe siku hiyo alikuwa mtangazaji nimpendae Taji Liundi ambaye alitabiri vizuri “..mwaka huu tutaona tofauti… tuwaachie majaji wafanye kazi yao.. mtashangaa zaidi Miss World mwaka huu akitoka Tanzania.”

Natumaini baadhi ya watu hawatachanganya mambo, na kudhani kuwa Tanzania ni India, si unajua viwanda vingi vya Tanzanite viko India pia. Afrika mkae tayari kumkubali Richa Adhia kama malkia mpya wa Afrika na dunia kutoka Tanzania. Big Brother Afrika katoka Tanzania, huu mwaka wetu, sijui inakuwaje!


Kutoka Raia Mwema.


No comments: