Sunday, November 25, 2007

Kamati ya Madini yaanza kumeguka


*Mjumbe ajiondoa ni iliyoundwa na Kikwete
*Aitupia lawama CHADEMA kwa maneno maneno

Na Mwandishi Wetu

MMOJA wa wajumbe 12 wa Kamati ya Kupitia Upya Mikataba ya Madini ametangaza kujitoa.

Akizungumza na gazeti hili Dar es Salaam jana, mjumbe huyo Bw. Peter Machunde, kutoka Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), alisema tayari amewasilisha barua yake kwa Rais.

Bw. Machunde alisema alifikia uamuzi huo kwa masikitiko makubwa na moyo mzito na kuomba ridhaa ya Rais amkubalie ingawa alimteua kwa heshima kubwa kuwa mmoja wa wajumbe.

Alisema uamuzi wake huo umetokana na kusikia maoni na wasiwasi wa baadhi ya watu, ambao alisema walionesha shaka na au kutoridhishwa na uteuzi wake na hivyo kumfanya atafakari kwa kina, kama kuwapo kwake katika Kamati kusingeipunguzia uwezo na uhalali wake miongoni mwa wanajamii.

Bw. Machunde alisema kilichomsikitisha sana ni maoni na wasiwasi wa baadhi ya watu wakishabikiwa na CHADEMA, waliopinga ushiriki wake kwenye Kamati.

"Binafsi nisingependa kuona kuwapo kwangu ndani ya Kamati kunawapa watu hao na chama chao kisingizio cha kumzuia mwanachama mwenzao ashiriki," alisema akimaanisha Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Bw. Zitto Kabwe.

Alisema hata hivyo kimsingi, Kamati ya Rais ilipokewa vizuri na Watanzania walio wengi kwa kuwa kuundwa kwake kulizingatia maslahi ya Taifa na ni Kamati iliyojumuisha watu wenye uwezo mkubwa na wanaotoa uwakilishi mpana wa jamii.


"Ni kwa sababu hii nimesikitishwa sana na ninashindwa kuelewa, pale baadhi ya viongozi wa CHADEMA wanapoingiza ajenda za kisiasa na kuhusisha chama chao katika suala zito na muhimu kwa maslahi ya nchi yetu.

"Huu ni upungufu kwa chama ambacho kimetumnia suala hilo kwa muda sasa hapa nchini, kuelezea upungufu wa sera na sheria na iweje sasa Rais anapounda Tume kwa maslahi ya Taifa, wao tena ndio wawe kipingamizi cha suala hilo," alisema.

Akizungumza kwa masikitiko, Bw. Machunde alielezea kusikitishwa kwake na mwelekeo wa mtizamo wa baadhi ya Watanzania kushutumiana na kutoaminiana na kujenga mazingira ya wao kujionesha kwenye jamii kwamba wana uchungu na nchi hii, ikiwa ni pamoja na raslimali zake, kuliko wengine.

"Ni imani yangu, kwamba wote tunaipenda nchi yetu kwa kiwango kinacholingana...nimeumizwa na kufadhaishwa sana na dhana inayojengwa na kuenezwa na viongozi wa CHADEMA, kwamba katika ushiriki wangu kama mjumbe wa Kamati hii, nisingeweka maslahi ya nchi yetu mbele.

"Hakuna tusi kubwa kama kudhaniwa kwamba unaweza kuisaliti nchi yako na kuitambua heshima na imani uliyopewa na Rais," alisema na kuwafananisha CHADEMA na genge la wababaishaji.

Alieleza kusikitishwa kwake na kuwapo hila za makusudi za kutaka kuidhoofisha Kamati hiyo kimamlaka, kwa kutumia mbinu chafu za kutumia majina ya watu kukidhi matakwa yao kisiasa.

Alisema huko ni kutojiamini na kutoamini mtu mwingine, licha ya kuwa wana mwakilishi wao Katika Kamati na tena ni kiongozi wa ngazi za juu kabisa.

Bw. Machunde ni mtaalamu wa masuala ya fedha, uwekezaji miradi na masoko ya mitaji mwenye Shahada ya Juu ya Uhasibu (CPA) na ambaye amekuwa mjumbe wa Bodi ya Taifa ya Uhasibu (NBAA) kwa miaka sita mfululizo.

Alimalizia akisema yeye si mwanasiasa na wala hana jukwaa la kisiasa, la kuelezea na kutetea rekodi yake ya mapenzi, uzalendo na utumishi kwa nchi yake.

"Rais aliponiteua kuingia Kamati hii, niliamini kwamba Kamati ina jukumu kubwa na muhimu kuliko sifa na heshima ya mtu mmoja au chama chochote cha siasa na bado nitaendelea kuamini hivyo, hata nikiwa nje ya Kamati," alisema.

Wajumbe waliosalia kwenye Kamati hiyo ni Mwenyekiti wake, Mwanasheria Mkuu wa Serikali mstaafu, Jaji Mark Bomani, Bw. Zitto, Mbunge wa Bariadi Mashariki, Bw. John Cheyo na Mbunge wa Kyela, Dkt. Harrison Mwakyembe.

Wengine ni Mbunge wa Msalala, Bw. Ezekiel Maige, Bw. David Tarimo wa Kampuni ya PriceWater Coopers na Bibi Maria Kejo ambaye ni Mkurugenzi wa Madai na Sheria za Kimataifa katika Wizara ya Katiba na Sheria.

Wajumbe wengine ni Mwanasheria wa Wizara ya Nishati na Madini, Bibi Salome Makange, Kamishina wa Sera wa Wizara ya Fedha, Bw. Mugisha Kamugisha, Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Makazi katika Wizara ya Ardhi, Bw. Edward Kihundwa na Mbunge wa zamani wa Ilala, Bw. Iddi Simba.

No comments: