Tuesday, November 13, 2007


Mrema amshangaa Jakaya Kikwete.

na Mwandishi Wetu .

MWENYEKITI wa Chama cha Tanzania Labour (TLP), Augustine Mrema, amesema Rais Jakaya Kikwete amefanya makosa yanayoweza kuleta chuki na machafuko nchini kwa kuzungumzia suala la Mahakama ya Kadhi kanisani.

Mrema alisema kitendo hicho cha Rais kimelenga kumchonganisha yeye (Mrema) kwa wananchi, hasa Wakristo ambao wamembatiza, na kusema kuwa ataonekana amefanya jambo kubwa na baya nchini.

Alisema jana alipozungumza na waandishi wa habari katika ofisi za makao makuu ya chama hicho, Magomeni, Dar es Salaam.

Juzi, Rais Kikwete akiwa katika ibada ya kumsikika Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Alex Malasusa, alisema hakuhusika kuliweka katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM suala la Mahakama ya Kadhi.

Rais Kikwete aliwaambia waumini wa kanisa hilo kuwa suala hilo kwa mara ya kwanza liliibuliwa bungeni na Mrema, wakati huo akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani.

"Mimi sikatai kuwa hoja hiyo niliiibua bungeni, lakini kitendo cha Rais Kikwete kutumia jukwaa la dini kueleza suala hilo kunalenga kunichonganisha kwa wananchi hasa Wakristo, ambako mimi nimebatizwa," alisema Mrema.

Mrema alisema, yapo mambo mengi mazuri aliyoyafanya wakati huo, lakini hayatajwi, na kutoa mfano kuwa aliwahi kuzima mgogoro wa Kanisa la KKT Dayosisi ya Arumeru ambao ungeweza kuleta maafa.

Pia alisema aliwahi kuzima mgogoro ndani ya Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA) kwa kuchangisha fedha za kufanya mkutano uliokuwa umeshindikana kutokana na ukata, lakini cha kushangaza, hayo yote hayasemwi.

Amemtuhumu Rais Kikwete kuzungumzia suala hilo kanisani, hali akijua ni kosa kuyapeleka mambo ya Waislamu kwa Wakristo, kwani linaweza kuibua mgogoro mkubwa au hata machafuko nchini.

Kutokana na hali hiyo, alisema hivi sasa ameshabaini sababu za kura zake kupungua wakati wa uchaguzi, na kusema kuwa hali hiyo inatokana na watu kuiba hoja zake.

"Hivi Rais Kikwete leo anaporuka na kusema suala la Mahakama ya Kadhi si ilani ya CCM na imewekwa na watu wengine… kama alikuwa halitaki kwanini hakulitoa?" alihoji Mrema.

Akieleza kilichomsukuma kuwasilisha hoja ya kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi bungeni, Mrema alisema akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani alikuwa akishughulikia migogoro ya ndoa na mirathi ya Waislamu, hivyo aliamua kufanya utafiti wa kuirejesha mahakama hiyo, ili iwasaidie.

Alisema katika uchunguzi wake alikwenda nchini Kenya ambako alijifunza jinsi mahakama hiyo inavyoweza kuendeshwa bila kuleta mifarakano katika nchi.

"….Baada ya kuhamia NCCR-Mageuzi nikiwa mgombea ubunge Jimbo la Temeke niliwaahidi wananchi nikishinda nitashughulikia siala hilo, ili mahakama hiyo irejeshwe.

"Kwa kuwa nilikuwa nimeliweka wazi kwa kila mwananchi, hakuna hata Mkristo aliyelipinga, kwani nilikuwa nimelifanyia utafiti wa kutosha na kila mmoja aliyelisikia aliridhika nalo, ndiyo maana mwaka 1996 nikalipeleka bungeni na likaungwa mkoni na wabunge wengi," alisema Mrema.

Alisema hata alipohamia TLP alimtuma mbunge wake (Thomas Ngawaiya) kulikumbusha suala hilo bungeni ambapo tangu wakati huo tume iliundwa kwa ajili ya kulifanyia kazi, ingawa hawakumshirikisha kama muasisi wa jambo hilo.

Katika mkutano huo, Mrema alionyesha kitabu alichodai alikiandaa mwaka 1996 kikionyesha muundo wa mahakama hiyo utakavyokuwa bila kuathiri maisha ya Wakristo.

Hata hivyo, Mrema alimuonya Rais Kikwete kulipeleka suala hilo kwa wananchi, kwani linaweza kuleta machafuko na kusema kama ameapa kwa Msahafu kutafuta maoni kwa wananchi, kutakuwa ni kwenda kinyume na maagizo ya mtume, kujadili au kuyatolea maoni masuala ya Mwenyezi Mungu.

"Rais Kikwete anasema kuwa atalipeleka suala hilo kwa wananchi wakalitolee maoni, wananchi gani? Yaani unaweza kwenda kumuuliza Mkristo kuwa unaitaka Mahakama ya Kadhi….hii si ni sawa na kwenda kumuuliza Mwislamu akubali kuwa Yesu ni mwana wa Mungu wakati wao wanaamini kuwa Mungu hakuzaa," alionya Mrema.

Alisema kuwa hata huu unaoitwa mgogoro uliopo ni ufisadi unaochochewa na viongozi waliopo madarakani na jinsi viongozi wa CCM wanavyoitumia kwa kueneza propaganda kuwa italeta vurugu, kwani wakati anaiandaa hiyo mahakama hakukurupuka kama CCM walivyoirukia, sasa wanaonyesha kuwa wameshindwa kuitekeleza.


Wakati huohuo, Kaimu Meneja Elimu wa Shirikisho la Vyama vya Ushirika, Gloria Mazoko, alisema anafurahishwa na kitendo cha Rais kuzungumzia suala hilo, kwani limetoa mwanga hasa kwa watu waliokuwa hawafahamu suala hilo lilikotokea.

Akizungumza na Tanzania Daima , Gloria alisema awali alidhani hoja ya kuwepo kwa mahakama hiyo kuliwekwa, ili kuwavutia wapiga kura hasa wa madhehebu ya Kiislamu.

"Awali nilikuwa na mtazamo tofauti kuhusu kuwepo kwa mahakama hiyo ya kadhi, kwa kweli kitendo cha rais kulizungumzia suala hilo kumenipa mwanga mkubwa na sasa nimeondokana na mtazamo wa awali niliokuwa nao juu ya kuwepo kwa kadhi," alisema Gloria.

Aliongeza kuwa pamoja na suala hilo kuzua mjadala mkubwa, haoni tatizo la kuwepo kwake. Hata hivyo, alishauri kuwa ikiwa kuwepo kwa suala hilo ni utaratibu na haliathiri, haoni sababu ya kutokuwepo.

Katika maoni yake mengine, kaimu meneja huyo alisema kutokana na suala hilo kuzungumzwa kwa kina na watu mbalimbali, kwa sasa limeanza kuleta mtafaruku katika madhehebu ya dini.

Alishauri taasisi za kidini kutofika mahali kusababisha mgawanyiko baina ya Wakristo na Waislamu, kwani inaweza kusababisha mshikamano na muungano uliopo nchini kupotea.

Naye Jerry Tillya, alisema kwa sasa wananchi wamechoshwa na uundwaji wa tume za kufuatilia masuala mbalimbali, akisema badala yake serikali ingetumia fedha hizo katika shughuli nyingine za maendeleo.

"Kila siku tume zinaundwa bila mpango huku wananchi wanataabika, hivi sasa kuna mfumuko wa bei ya vitu mbalimbali vikiwemo vyakula, kwa nini serikali isiunde tume kuchunguza suala hili ambalo lina masilahi makubwa kwa taifa?" alihoji Tillya.

Ofisa Ugavi wa Shirikisho la Vyama vya Ushirika, Mteme Kungwe, alikubaliana na tamko la Rais Kikwete, alizishauri taasisi za kidini kuendesha mambo yake bila kuwepo kwa mkono (mchango) kutoka serikalini.

Naye Emmanuel Richard, alisema ili kuondoa mvutano ulipo kati ya serikali na Waislamu kuhusu kuanzishwa kwa mahakam hiyo, ni bora pande zote mbili zikakaa pamoja na kujadili suala hilo, kuliko kukaa kimya, jambo ambalo amesema linaweza kuhatarisha amani ya nchi.

Juzi, Rais Kikwete alikaririwa akisema chimbuko kuhusu Mahakama ya Kadhi ni bungeni, na muasisi wake ni Mrema alipokuwa mbunge wa Temeke.

Alisema baadaye hoja hiyo iliwasilishwa na Ngawaiya kwa nguvu ya hoja binafsi na kwamba kwa busara za Spika wa kipindi hicho, Pius Msekwa na kiongozi wa shughuli za serikali bungeni, Frederick Sumaye, alikataa hoja hiyo kujadiliwa bungeni moja kwa moja kutokana na kile alichokitaja kuwa ni unyeti wake na kuamua kuipeleka katika Kamati ya Katiba na Sheria.

Rais Kikwete alisema baada ya kamati hiyo kukamilisha utafiti na kukabidhi ripoti kwa Spika, alikabidhi serikalini ambako inafanyiwa kazi, ili kutoa ushauri unaofaa.


Taarifa hii imeandaliwa na Mobin Sarya, Hellen Ngoromera, Dauson Harold na Happiness Katabazi.

Toka: Tanzania Daima.


No comments: