
Tujivunie Kiswahili, tuache kukinyanyapaa.
Mhariri
HabariLeo; Tuesday,November 13, 2007 @00:01
MAKAMU wa Rais, Dk. Ali Mohamed Shein alikaririwa akieleza kushangazwa kwake na jinsi baadhi ya Watanzania wanavyokidhalilisha Kiswahili.
Dk. Shein ambaye alikuwa akizindua kongamano la siku nne la Kimataifa la Idhaa za Kiswahili Duniani alieleza kusikitishwa na Watanzania hao kutumia kupendelea kutumia Kiingereza katika mikutano, warsha na semina badala ya Kiswahili, hali inayochangia kuididimiza lugha hiyo.
Tunaungana na Makamu wa Rais katika wasiwasi huo wa Watanzania kuchangia kukididimiza Kiswahili badala ya kukiendeleza.
Ni hali ya kusikitisha ikizingatiwa kwamba baadhi ya Watanznaia badala ya kujivunia Kiswahili nao wameanza kukinyanyapaa kwa kuwa na kasumba kwamba eti mtu akizungumza Kiswahili eti hajaendelea, hajasoma, na kadhalika!
Hivi kwa nini Watanzania tusione mfano wa baadhi ya nchi zenye lugha zao ambazo zinapigana kufa na kupona katika kuzitumia lugha hizo katika ngazi zote?
Hatuoni mfano wa Wafaransa, Wataliano, Wajerumani, Warusi, Wachina, Wajapan na kadhalika?
Ile hali iliyokuwapo katika miaka ya 1970 na 1980 ya kukifanya Kiswahili kiweze kutumika katika ngazi zote za shule imeishia/imefia wapi?
Ni kweli Tanzania ni kitovu cha Kiswahili, lakini hivi sasa kutokana na hali ya kukinyanyapaa, hivi sasa ziko baadhi ya nchi zinakaribia kuchukua nafasi hiyo.
Hivi kweli Watanzania tuko tayari kuiachia nafasi hiyo ichukuliwe na nchi nyingine?
Kwa nini uwepo ulegevu katika kukiimarisha Kiswahili wakati lugha hiyo hivi sasa imeanza kutumia hata katika Umoja wa Afrika na kutambulika katika nchi na taasisi nyingi duniani?
Sisi hatudhani kwamba hiyo ni barabara. Tutakuwa tunaliua taifa letu wenyewe.
Kwa maana hiyo basi, matamshi ya Makamu wa Rais yawe ni changamoto kwa kila mmoja nchini kuhakikisha Kiswahili kinakamata umuhimu wake kama ilivyokuwa katika kiaka ya 1970 na 1980 na hata kupita kiwango hicho.
Kiswahili ni lugha ya asili yetu Watanzania. Tujivunie Kiswahili, tukiimarishe na tukikuze.
No comments:
Post a Comment