Sunday, November 18, 2007


Msekwa: Enzi za kulindana,

kubebana CCM zimekwisha

Basil Msongo

HabariLeo; Sunday, November 18, 2007 @00:03

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Pius Msekwa amesema enzi za kulindana, ‘mwenzetu’ na kubebana katika chama hicho zimekwisha.


Akifungua na kuwasilisha mada katika kongamano la wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu Dar es Salaam jana, Msekwa alisema awamu ya sasa ya uongozi wa chama hicho haitatetea wakosaji au kuwalinda na itafanya kazi kwa uwazi kujiimarisha.

Msekwa alisema CCM ipo tayari kukosolewa na kwamba baada ya kumalizika kwa Mkutano Mkuu wa chama hicho uliofanyika Dodoma hivi karibuni, uongozi wa chama hicho umeanza kusimamia utekelezaji wa kanuni ya CCM kwa nguvu mpya.

Kongamano alilolihutubia Msekwa liliandaliwa na Umoja wa Vijana wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya kimataifa ya wanafunzi yanayofanywa Novemba 17 kila mwaka.

Maadhimisho kama hayo yalifanyika pia Mjini Magharibi, Zanzibar, Morogoro, Iringa, Dodoma, Mwanza, Arusha na Moshi ili kuwapatia wanafunzi fursa ya kujadili na kutoa maoni kuhusu hali ya chama hicho kwa ujumla, kutoa ushauri na kueleza upungufu.

“Suala la kukosoa, kujikosoa na kukosoana katika chama ni njia ya kukijenga na kukiimarisha chama chetu. Lakini ni kweli pia kuwa hatujajenga tabia hii ipasavyo. Mara nyingi tumependelea kuteteana na kufichiana makosa, awamu hii itaondokana nayo,” alisema Msekwa.

Alisema dhana ya utawala bora ndani ya chama itatekelezwa kwa ukamilifu na kwamba, CCM itatekeleza shughuli zake kwa kuzingatia Katiba, sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa.

“Suala la utawala bora ndani ya chama chetu linapaswa kutekelezwa kwa nguvu mpya katika kusimamia kanuni cha chama zinazoweka nidhamu kwa wanachama na viongozi wa chama,” alisema Msekwa.

Sambamba na kukiri kulindana, Msekwa pia alikiri kuwa rushwa imetawala katika uchaguzi ndani ya chama hicho na kubainisha kwamba CCM haikumbatii rushwa ila utekelezaji na usimamizi wa sera ya chama hicho kupambana na rushwa umekwama.

“Wote tunajua wazi kwamba chama chetu kimeingiliwa vibaya sana na tatizo kubwa la rushwa katika uchaguzi wake, hilo hatuwezi kulificha, lazima tuwe wakweli,” alisema na kueleza kuwa rushwa wakati wa uchaguzi wa chama hicho inakera.

“Hata Mwenyekiti wetu alisema kule Kizota, rushwa ni ajenda ya CCM, sisi hatukumbatii rushwa” aliwaeleza wajumbe wa kongamano hilo wakiwamo wanafunzi wa vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu, wabunge, mawaziri, viongozi wa CCM mkoa na wilaya za Dar es Salaam.

Aliwataka wanachama wa CCM kutobweteka kwa kuwa mazingira ya siasa yamebadilika hivyo hata kama wanalinda ada za uanachama wao hawatakuwa na thamani katika chama hicho endapo hawatakisaidia chama kushinda chaguzi mbalimbali.

Msekwa alisema sambamba na juhudi za wanachama, uimara wa chama hicho utatokana na ubora wa dira, ubora wa malengo yake, na ubora wa mipango ya utekelezaji wa malengo hayo.

Kwa mujibu wa Msekwa, hotuba ya Mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete katika Mkutano Mkuu wa chama hicho uliofanyika Dodoma itakuwa dira ya utekelezaji wa sera za CCM.

Alisema bila juhudi za wanachama, CCM haiwezi kuendelea kuwa chama tawala hivyo mwanachama hai wa chama hicho si yule anayelipa ada ya uanachama, ni anayeshughulika ipasavyo kukiletea chama ushindi katika chaguzi.

“Ndiyo kusema kwamba hata kama mwanachama amelipa ada zake zote, hata mpaka mwaka 2050, lakini siku ya uchaguzi akizembea kwenda kukipigia chama chetu kura yake, uanachama wake hauna thamani, huyo si mwanachama hai wa CCM,” alisema Msekwa.

Katika kongamano hilo kiongozi huyo mkongwe katika chama na serikali alieleza umuhimu wa kuwapo kwa viongozi wa zamani kwa kuwa uzoefu wao ni muhimu kwenye kufanya maamuzi kwa kuchanganya na fikra za viongozi wapya.


No comments: