Innocent Mwesiga
NILIPATA kusoma mahala kwamba "kujua Kiingereza si kujua au kuwa mtaalamu katika eneo lako la kazi".
Ingawa dhana hii ina utata, lakini hakuna ubishi kuwa kujua Kiingereza si sifa ya ubora. Kama zilivyo lugha nyingine, Kinyamwezi, Kihaya, au Kisukuma; Kiingereza ni chombo cha mawasiliano kwa wanajamii.
Ikiwa Kiingereza ni lugha yako ya kwanza au jamii uishimo ndiyo lugha inayotumika, huna budi kukiongea na kukiandika bila matatizo yoyote hata kama si kwa ufasaha. Kwa mantiki hiyo, haimaanishi wewe ni bora au mtaalamu wa fani yoyote.
Hata hivyo, nadharia ya kudhani kwamba lugha na fani ya mtu vinaweza kutenganishwa inahitaji uchanganuzi kidogo. Lugha ya fani yako ni sharti uijue.
Aghlabu, moja kati ya mihimili mikubwa katika fani ya uandishi wa habari ni umahiri wa kucheza na lugha.
Kama wewe ni mwandishi wa habari, na Kiingereza ndiyo lugha ya mawasiliano katika jamii yako, yakupasa kukiongea na kukiandika kwa ufasaha.
Haipendezi kuona mwandishi wa habari wa gazeti la Kiingereza amebeba bango la msisitizo kuwa hajuhi Kiingereza lakini anaijua fani yake.
Ingawa ubora wa vielelezo vya ushaidi na uelewa wa sheria katika jamii husika ni nyenzo muhimu kwa mwanasheria, pia, uwezo wa kutumia lugha ya mawasiliano kwa maandishi au kujieleza ni nguzo kubwa katika fani ya sheria.
Mwanasheria anajua ni wakati gani atumie lugha ya mafumbo na ni wakati gani atumie lugha inayoeleweka ili kumnusuru mteja wake. Mawasiliano ya moja kwa moja kati ya mwanasheria, wazee wa mahakama na mahakimu yana athari zaidi ya kumtumia mkalimani.
Lugha ni rafiki mkubwa wa mwanasheria. Kama Kiingereza ndiyo lugha ya mawasiliano ndani ya jamii husika, ni vema kutokuitenganisha na fani ya sheria.
Historia ya mwanadamu na maendeleo ya jamii aishimo, vina mahusiano ya moja kwa moja na matumizi ya lugha kama chombo cha mawasiliano baina ya wanajamii.
Watu wa mataifa kama ya China, Ujerumani, Urusi, Uajemi, Japan, Marekani, na mengine mengi, wanatumia lugha zao kama chombo cha mawasiliano, na ndizo hizohizo wanazotumia kupata utaalamu katika fani zao.
Binafsi, sidhani kama mjadala wa matumizi ya Kiingereza ndani ya mfumo wetu wa elimu unapewa uzito unaostahili. Si vema kuendelea kuukwepa mjadala huu, kwa sababu Kiingereza ndio lugha ya mawasiliano itumikayo kutupatia utaalamu katika fani zetu.
Kuna nyenzo mbili za kutilia maanani. Mosi, utaalamu katika fani yoyote, na pili, lugha, ambacho ni chombo kinachotumika kuingiza huo utaalamu kwenye ubongo wa mtu.
Kwa mfano, Mchina anajifunza utaalamu katika fani yoyote ile ambao haujuhi, kwa kurahisishiwa na lugha yake ya msingi ambayo ni Kichina, ambayo tayari imeimarika ndani ya ubongo wake.
Si nadra kumkuta Mchina mahala ambapo lugha ya mawasiliano si Kichina bali ni Kiingereza kama ilivyo Marekani, akitafuta neno la Kiingereza kwa dakika kumi au ziadi kuelezea ujuzi anaoujua tayari kwa lugha yake.
Kinyume, Watanzania tunajifunza vitu vyote viwili ambavyo ni vigeni kwetu kwa wakati mmoja. Tunatakiwa kuelewa utaalamu ambao ni kitu kipya. Hata Kiingereza ambacho ni chombo kinachotumika kuingiza utaalamu huo katika bongo zetu, ni lugha mpya, yaani sio lugha yetu ya kwanza na wala si ya msingi.
Tukiondoa kasumba ya kupima fukuto la joto la Dar es Salaam na kuvitumia vipimo kama kigezo cha uwakilishi wa joto la nchi nzima, tutakubaliana kwamba asilimia kubwa ya Watanzania, lugha zao za kwanza si Kiswahili wala Kiingereza bali ni zile za asilia.
Njia ya kufikiri na kutafakari, mawazo, ubunifu, majina ya vitu, hadithi, simulizi, utamaduni, na vitu vingine vinavotumika kukuza ubongo wa mtoto toka azaliwe mpaka umri wa kwenda shule, vinapokewa na mtoto kwa Kichagga, Kisukuma, Kihehe, Kimakonde, Kizalamo, na lugha nyingine za asili.
Mtoto anapoanza shule, mambo yote yanabadilika ghafla na sasa lugha ya msingi inakuwa Kiswahili. Lugha inayojenga msingi wa kuingiza utaalamu katika ubongo wa mtoto wa Kitanzania inaanza kuwa Kiswahili, ambayo si mpya, bali haitumiki majumbani mwa familia nyingi za Kitanzania.
Huo ndio unakuwa msingi wa fani ya mtoto. Habari njema ni kwamba ubongo wa mtoto mdogo, una sifa na umaridadi wa kuzinasa lugha zote zinazokatiza mbele yake, na kuziongea bila matatizo yoyote.
Habari mbaya ni kuwa uwezo wa mtoto kuzinasa lugha unafifia kadiri umri wake unavyozidi kukua. Umri wa kuanza shule kwa Watanzania walio wengi unakinzana na umaridadi wa kuzinasa lugha.
Kadiri mtoto anavyopanda kimadarasa, ndivyo uwezo wa kuelewa lugha mpya unavyozidi kufifia, na ndivyo anavyozidi kujiimarisha katika lugha ya msingi. Sifa ya lugha ni matumizi yake. Ili uweze kuimiliki lugha yoyote ile duniani, yakulazimu kuiongea, kuisoma, na kuiandika.
Pamoja na ukweli kuwa ukali wa kunasa lugha unakinzana na umri wa mtu, ubongo wa mtoto anayeanza darasa la kwanza kwa wastani wa umri wa miaka saba, bado ni mchanga, kwa vyovyote vile, tunaufungua ubongo mchanga na kuupa msingi wa lishe ya Kiswahili kwa miaka saba mfululizo mpaka ukomavu wake, yaani anapomaliza darasa la saba akiwa na umri wa miaka 14.
Lugha ya mawasiliano na kufundishia katika shule za msingi ni Kiswahili. Kiingereza kinafundishwa kama somo, na wala si lugha ya mawasiliano au kufundishia. Kibaya zaidi, shule zetu nyingi za msingi zina baadhi ya walimu wa Kiingereza wanaoamini kwamba hawajuhi Kiingereza, lakini wanazimudu vizuri fani zao. Mara nyingi somo la Kiingereza linafundishwa kwa kuchanganywa na Kiswahili.
Matamshi ya sentensi kama past tense ya go ni went si mageni kwa wanafunzi wa shule zetu za msingi. Kumwagia kidonda tindikali, sasa tumekuwa kama mtambo wa butua butua, kwa maana ya kufyatua walimu kama matofali ya mchanga bila kuchanganya na simenti.
Mtoto anapoingia sekondari anakuwa ameweka msingi wa fani yake kwa Kiswahili. Tunatarajia aanze kuimarika na kuongeza misamiati. Ghafla, Kiingereza kinakuwa lugha mpya ya mawasiliano na ya kufundishia. Kiswahili ambacho ni lugha ya msingi, kinafundishwa kama somo.
Mkinzano huo wa lugha na uelewa wa fani zetu, unaleta ugonjwa wa mkanganyano katika asilimia kubwa ya bongo za Watanzania. Mabadiliko ya ghafla ya lishe ya lugha kwa ubongo bila kuwa na shibe ya stamina ya lugha ya msingi yanaleta utapia mlo wa akili.
Si bongo zote zinaweza kula kila aina ya lugha kwa wakati wowote bila ya kucheuwa. Kinga ya kucheuwa ni kukariri na sifa moja kubwa ya kukariri ni kutokufikiri au kutokuwa mbunifu.
Usahaulifu ni rafiki mkubwa wa haya majinamizi. Yeyote aliyetembelewa na sifa hizo, hata mvua zikamnyeshea na akajificha mpaka darini, ni nadra kumkuta ameelimika, ikizingatiwa kuwa elimu ni kitu kinachobaki kichwani baada ya kusahau yale uliyojifunza.
Kila nchi duniani ina mfumo wake wa elimu na hakuna mzani unaoweza kutumika kupima uzuri au ubaya wa mfumo wa elimu wa nchi moja kulinganisha na nchi nyingine. Ugumu au urahisi wa maswali, kufaulu au kushindwa kwa waliowengi haviwezi kutumika kama kipimo cha ubora wa elimu.
Kipimo cha maana cha mfumo wowote wa elimu duniani, ni jinsi unavyowasaidia watu wake kuyabadili mazingira yao yanayowazunguka. Kama wahitimu wa mfumo huo hawawezi kubadili mazingira yao binafsi na ya jamii waishimo, basi mfumo huo haufai.
Binafsi, si mshabiki wa kupendelea lugha moja zaidi ya nyingine kati ya Kiswahili na Kiingereza. Pendekezo langu ni kwamba lugha ya msingi iwe ndiyo lugha ya sekondari na vyuo vikuu. Msingi wa nyumba, lazima ufanane na nyumba unayotaka kujenga. Haiwezekani kuporomosha hekalu la ghorofa 30 katika msingi uliokusudiwa kujenga nyumba ya chumba kimoja na sebure.
Msingi wa mawasiliano unaompa kijana kutoka darasa la kwanza mpaka la saba, lazima uendelezwe sekondari na vyuoni. Msingi maana yake ni kujenga kitu juu yake; sekondari unayoijenga lazima ifanane na msingi wenyewe. Kiingereza hakifanani na Kiswahili ambacho ni msingi tunaojengewa.
Nakumbuka kuwa miongoni mwa makusudio ya kutumia Kiswahili katika shule za msingi yalikuwa kuhakikisha tunaimarika katika lugha iliyotukomboa, na kuondoa makombo yaliyosalia vichwani mwetu baada ya kumung'oa mkoloni.
Pia, kuiunganisha jamii yetu, kwani maneno mengi ya Kiswahili yanatumika katika lugha zetu za asili. Suala jingine ambalo ilibidi liende sambamba na makusudio hayo, lakini halikutiliwa maanani ni kukifanya Kiswahili kuwa lugha ya ukombozi wa fikra, ili kuleta mageuzi ya kiuchumi na kuneemesha hali za Watanzania.
Mojawapo ya kasumba alizotuachia mkoloni ni kumwabudu pamoja na mambo yake yote. Kitu chochote kizuri mpaka sasa kinaitwa cha Kizungu. Kiingereza tukawaachia wasomi wetu wachache waliobahatika kuchaguliwa kuendelea na elimu ya juu.
Kwa kufanya hivyo, Kiswahili kimebaki na sura ya kuiunganisha jamii, na tukategemea Kiingereza kichukue nafasi ya kuleta ukombozi wa fikra na kuiendeleza jamii. Binafsi, nafikiri jukumu la kuleta ukombozi wa fikra linawahusu wanajamii wote.
Ni vema kuwapo uelewa wa lugha ya mawasiliano baina ya wataalamu (wahandisi), mafundi wa kati (technicians), na wanajamii waliowengi ambao hawana ujuzi wowote. Kiingereza kimekosa nafasi miongoni mwa haya matabaka.
Ukiacha wazee wetu ambao walisoma shule za msingi na sekondari zilizofundisha Kiingereza, au walifunzwa na walimu wanaozungumza Kiingereza bila matatizo yoyote, na matokeo yake wamejaliwa kuzungumza na kuandika lugha zote mbili kwa ufasaha yaani Kiswahili na kiingereza, wahitimu wengi ambao hasa ni matokeo ya mfumo huu wa sasa ni msalaba kwa jamii.
Idadi ya watu wanaotaka kutenganisha lugha na taaluma inaongezeka kwa kasi kubwa. Mfumo wetu unaendelea kuzaa vijana wa kisasa, wasioweza kuandika kwa ufasaha au kuongea si tu Kiingereza peke yake, bali hata Kiswahili.
Bahati mbaya, kipindi hiki cha mageuzi katika jamii yetu kinahitaji waandishi kuliko kipindi chochote katika historia ya nchi yetu. Tumefungua milango; tunatoka nje ya nchi na wageni wanaingia nchini kwetu kwa kasi. Nani atawaandikia wanajamii wetu dhamiri iliyofichika ya hawa wageni?
Nani ataweka katika kumbukumbu tamaduni zetu ili wageni wasiziharibu tena? Na nani atawaandikia wajukuu zetu uhalisi wa maisha ya huku ughaibuni?
Historia ya mwanadamu inatuasa kuwa tunasoma ili kujitegemea kifikra, kuwa wabunifu na la muhimu hasa ni kuyabadili mazingira yetu. Zamani Watanzania tulikuwa na majigambo kuwa elimu yetu ni bora kulinganisha na nchi nyingi duniani.
Walioamini hivyo sasa wanaachwa kwenye mataa. Mienendo ya makampuni ya kigeni si ya kufurahisha na haileti matumaini kwa jamii yetu. Hawa wageni wanakataa wasomi wetu eti kwa sababu hawajuhi lugha waliopatia usomi wao, yaani Kiingereza.
Benjamin Mkapa aliwahi kuulizwa akiwa rais, lakini majibu yake yalionyesha kuwa tatizo hili bado halina ufumbuzi. Kinyume na imani yetu ya zamani, makampuni ya kigeni yanaonekana kuvutiwa na watu waliosomea nje kuliko wale waliomalizia nyumbani.
Kwa nini tusifanye kama Cameroon ambao wanatumia lugha zote mbili bila matatizo. Kuna shule za Kifaransa peke yake kuanzia msingi mpaka vyuoni na kuna shule za Kiingereza peke yake kuanzia msingi mpaka vyuoni.
Au mfumo wa aina hii utaligawa Taifa? Basi tuwaige majirani zetu wa Kenya kwa kufundisha Kiingereza shule za msingi na sekondari na Kiswahili kibaki kutumika majumbani na mitaani.
Je, kwa kufanya hivyo tutaibua ukabila? Kwa nini tusiwe na mfumo wetu wa kipekee wa kufundisha Kiswahili toka msingi mpaka vyuoni.
Inawezekana pia kukihalalisha Kiswahili peke yake, tukawa tumejifunga kitanzi na kijiwekea mipaka ya mawasiliano na baadaye tukashindwa kupumua kwa sababu ya umasikini wetu, na uduni wa teknolojia yetu. Inawezekana pia kuwa mfumo wa sasa unafaa labda tatizo ni sisi wenyewe! Hatuwezi kufikia majibu kirahisi zaidi ya kuchanga bongo kwa pamoja.
inno@comcast.netKutoka: Raia Mwema
No comments:
Post a Comment