Friday, November 16, 2007

Kama tumeushinda ukabila, nini dini?

John Bwire

SUALA la kuunda Mahakama ya Kadhi nchini limekuwa mdomoni mwa watu na kuchukua sura mpya kila wakati.

Tayari suala hilo limefikishwa mahakamani na Mchungaji Christopher Mtikila akipinga kuanzishwa kwake.

Baraza Kuu la Waislamu la Tanzania (BAKWATA) limemjia juu likidai kwamba aliukashifu Uislamu wakati yuko katika mchakato wa kulifikisha suala hilo mahakamani.

Jumapili iliyopita Rais Jakaya Kikwete alitumia mwanya wa sherehe za kumsimika Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Alex Malasusa, kujiweka mbali na suala hilo ambalo lilikuwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya chama chake (CCM) wakati anagombea Urais mwaka 2005.

Kikwete aliwarudisha miaka ya nyuma Watanzania kueleza kwamba suala la Mahakama ya Kadhi ni ‘mtoto’ wa Augustine Mrema, Rais wa chama cha TLP, kwani ni yeye aliyekuwa ameliibua wakati akiwa mbunge wa Temeke.

Mrema naye amemlaumu Rais Kikwete kwamba alifanya kosa kulizungumzia suala hilo kanisani kueleza kwamba ni yeye aliyeliibua. Alidai kwamba kwa kufanya hivyo amemchonganisha na Wakristo wenzake.

Hayo yote yaliyotokea kuhusiana na suala hilo ni ushahidi tosha kwamba suala hilo linalogusa imani za watu linahitaji kupatiwa ufumbuzi kwa kutumia busara.

Hatutaki kuingia kwa undani kusema ni yupi alikuwa sahihi na yupi alikuwa amekosea katika suala zima la kuwapo kwa Mahakama ya Kadhi nchini.

Lakini, tunaamini kwamba kuendeleza malumbano ya suala hilo kunaweza kulifikisha taifa letu mahali pabaya.

Kubwa zaidi ni suala ambalo linaweza likafifisha umoja wa kitaifa ambao mwasisi wa taifa hili, Mwalimu Julius Nyerere aliujenga wakati wote wa utawala wake.

Ni ule umoja ambao unawafanya Watanzania leo kutotilia maanani dini ya mtu wala kabila lake katika masuala yote ya ujenzi wa taifa hili.

Baada ya kufanikiwa kupiga vita ukabila, tusifike mahali ambapo sasa ikawa ni sifa kwa mtu kuwa muumini wa dini fulani.

Ni kutokana na sababu hiyo ndiyo maana tunadhani kuna haja kubwa ya kutumia busara katika kupata ufumbuzi wa suala hilo tena haraka.


Kutoka: Raia Mwema

No comments: