Wednesday, November 28, 2007

Wasichana Dar es Salaam wauzwa Kongo



*Wachukuliwa mikoani kama wafanyakazi wa ndani
*Wafikia kwenye majumba Masaki, Kunduchi, Zanzibar


Na Rashid Mkwinda, Tunduma

BIASHARA haramu ya kuuza binadamu nchi za nje imezuka sehemu mbalimbali mpakani mwa Tanzania na nchi jirani, kwa wasichana wenye umri wa kati ya miaka 13 na 14.

Wasichana hao wamekuwa wakikusanywa na kusafirishwa katika nchi hizo ambako hulazimishwa kupigwa picha za uchi na kufanya biashara ya ngono.

Kwa mujibu wa taarifa za siri zilizotolewa na wasichana watatu waliozungumza na gazeti hili mjini hapa juzi, walichukuliwa nchini na kusafirishwa hadi Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) katika mji wa Lubumbashi ambako awali waliambiwa wanakwenda kufanya kazi za ndani.

Wasichana hao, Paulina Samwel (14), Happiness Jonathan (14) na Zuhura Majige (15), walidai kuwa walichukuliwa Mbeya Agosti 29 mwaka huu na mwanamke waliyemtaja kwa jina (linahifadhiwa) ambaye alidai anahitaji watu wa kufanya kazi za nyumbani kwake, Dar es Salaam.

Waliendelea kudai kuwa walichukuliwa na mwanamke huyo hadi nyumba moja Mbezi Beach ambako waliwakuta wasichana wa rika lao wasiopungua 55 kutoka mikoa mbalimbali ya Bara wakiwa wamefungiwa ndani na kupewa mahitaji yote muhimu ikiwa ni pamoja na chakula kizuri, mafuta mazuri ya kulainisha ngozi na nguo za kubadilisha.

"Walikuwa wakituhamisha kutoka jumba moja hadi jingine…kuna majumba matano sehemu za Mbagala, Mikocheni B, karibu na Kanisa la Assemblies of God, Masaki, Kunduchi, Mbezi Beach na Unguja karibu na soko la samaki," alidai Paulina.

Walidai kuwa pamoja nao walikuwapo wanawake wenye umri mkubwa sawa na mama zao, ambao walikuwa wakiwafundisha mambo ya ngono, huku wakitumia muda mrefu kuangalia picha za ngono kupitia mikanda ya Video na kwamba usiku walichukuliwa baadhi ya wasichana na kurejeshwa alfajiri.

"Huko tunakutanishwa na wanaume ambao tunafanya nao vitendo vya ngono kwa malipo, ambayo huchukuliwa na wanawake hao na siku nyingine huchukuliwa wasichana wengine kwa ajili ya kupelekwa katika majumba ya starehe na kurejeshwa alfajiri na gari maalumu lenye vioo vya giza," alidai Happiness.

Waliendelea kudai kuwa wasichana wengi wanatoka Mbeya, Kigoma, Morogoro, Shinyanga na wilaya za Kisii na Kakamega, Kenya na kwamba Oktoba 12 mwaka huu, wasichana 17 wakiwamo wao, walichukuliwa na kusafirishwa kwa njia ya magari makubwa hadi DRC.

Walidai kuwa siku moja kabla ya kuanza safari, waliletewa hati za kusafiria zikiwa na picha ambazo walipigwa siku waliyofika na kwamba kila mmoja anapofika katika jumba hilo, hupigwa picha nne za pasipoti kwa kutumia kamera ndogo ya 'Digital'.

"Tulichukuliwa ndani ya malori yanayosafirisha mizigo kutoka bandari ya Dar es Salaam na kila lori tulipanda wasichana watatu…yalikuwa malori yapatayo sita. Kiongozi wetu ambaye alikuwa ni mama wa makamo, alipanda lori la mbele," alidai Zuhura.

Aliongeza kusema walipitia katika njia ya mpaka wa Tunduma na kwa siku nne waliingia Lubumbashi na kupelekwa moja kwa moja katika jumba la kifahari ambako waliwakuta wasichana wenye umri kama wao kutoka sehemu mbalimbali za Afrika Mashariki, wakiwamo wa kitanzania, ambao walifahamiana kutokana na Kiswahili.

Wakiwa katika jumba hilo, walidai walishangaa kuona makundi ya watu kutoka mataifa mbalimbali ambao wakidaiwa kutoka Paris, Ufaransa na Arabuni ambao walifanya mazungumzo na wenyeji wao na baadaye kuchaguliwa baadhi yao na kisha kuondoka nao.

Walidai kuwa utaratibu huo ni wa kila wiki na kila siku makundi ya wasichana walikuwa wanaletwa katika jumba hilo.

"Hali hii ilianza kututia hofu mimi na wenzangu, tukatafuta mbinu za kutoroka…tukaondoka alfajiri ndani ya jumba hilo na kufika katika mtaa mmoja, tukakutana na mama akiwa anatoka msikitini, tukamwomba atusaidie baada ya kumweleza matatizo yetu," alidai Zuhura.

Aliongeza kuwa mama huyo aliyemtaja kwa jina (linahifadhiwa) aliwachukua hadi nyumbani kwake na kuwauliza jinsi walivyofika humo na kuwatahadharisha, kuwa watu wale hufanya biashara za kuuza wasichana Ulaya na Arabuni, hivyo walikuwa wamejiingiza katika matatizo.

Alidai kuwa mama huyo aliwatafutia usafiri wa kurudi nchini kupitia magari makubwa yanayofika Tanzania na kuingia kupitia mpaka wa Tanzania na Zambia kitongoji cha Tunduma Novemba 15 mwaka huu.

Walipoulizwa sababu za kudanganyika hadi kufika huko, wasichana hao walidai kuwa wao wanatoka katika familia duni na kwamba mara baada ya kumaliza shule ya msingi na kushindwa kuendelea na masomo, waliamua kutafuta kazi yoyote ya kufanya na kwamba kazi pekee waliyoiona ni kufanya kazi za uyaya.

"Mimi naishi na bibi yangu Mbozi, mama yangu alifariki dunia siku nyingi, niliposikia kuna mtu anatafuta msichana wa kazi, nilifurahi na hasa niliposikia kuwa ninakwenda Dar es Salaam, kwani sikuwahi kufika hata siku moja nikajiona mwenye bahati kufika Dar es Salaam, lakini yaliyonikuta siwezi hata kusimulia," alisema Paulina kwa uchungu.

Mmoja wa watoa taarifa hizi ambaye hakupenda kutajwa jina lake gazetini alidai kuwa biashara hiyo ni maarufu nchini katika sehemu za mipaka ya nchi za Kasumulu mpakani mwa Malawi, Kigoma, Holili na bandari ya Isaka Kahama na kueleza (bila kufafanua) kwamba biashara hiyo inahusisha watu wakubwa.

No comments: