WAZIRI wa Uingereza anayeshughulikia Masuala ya Maendeleo ya Kimataifa, Douglas Alexander, ametaja rushwa na ufisadi kuwa baadhi ya changamoto zinazoikabili Tanzania katika kufikia maendeleo ya kweli.
Alexander alisema hayo juzi katika hafla ya kukaribishwa nyumbani kwa Balozi wa Uingereza nchini, katika kwa ziara yake siku mbili.
Alisema Tanzania inapaswa kuitia moyo Uingereza kwa kuhakikisha misaada inayotolewa na nchi hiyo, inasaidia nyanja mbalimbali za maendeleo na inawafikia walengwa badala ya kupotea kwa njia ya rushwa.
Alisema katika siku za hivi karibuni kumekuwa na vichwa vya habari katika magazeti vilivyokuwa na maswali magumu kuhusu Benki Kuu ya Tanzania (BoT) au mambo yanayohusiana na fedha, ambazo zilianza kuzua mjadala katika Bunge la Uingereza hivi karibuni huku baadhi ya wabunge wakihoji mambo kadhaa juu ya suala hilo.
Kwa mujibu wa Alexander, Bunge hilo, limeanza kujenga hofu juu ya misaada ya nchi hiyo kwa Tanzania na kubainisha kuwa, baadhi ya wabunge walimweka katika wakati mgumu kwa kumtaka kujibu baadhi ya maswali kuhusu misaada ya nchi hiyo kwa Tanzania.
Kwa hakika katika miaka ya hivi karibuni baada ya serikali yetu kuongeza fedha katika sekta ya afya na elimu, huku Tanzania, moja ya changamoto kubwa ambazo tumezipata ni juu ya kuhakikisha fedha hizi za walipa kodi wetu zinatumika ipasavyo, alisema Alexander.
Alisema changamoto hizo ni pamoja na matumizi katika sekta ya afya na elimu, kutoa elimu bora, kutoa huduma za jamii kulingana na mahitaji, matumizi ya serikali yanayoendana na kuzingatia uwekezaji bila kusahau umuhimu wa misaada ya kimataifa na kodi za wananchi.
Kwa hiyo nachukua fursa hii kuwatia moyo katika safari yenu ya maendeleo iliyoanza sasa kwa maana ya kuhakikisha pesa inayotolewa inatumika vizuri na kuhakikisha kuna maono thabiti ya malengo na kwamba siku za mbele tutashangilia sio tu mafanikio tutakayoyashuhudia bali pia maendeleo yatakayoweza kufikiwa, aliendelea kusema.
Waziri huyo ametaja changamoto zingine zinazoikabili Tanzania katika kufikia maendeleo ya kweli kuwa ni kukabiliana na vifo vya watoto wadogo, utapiamlo, vifo vya wajawazito na uboreshaji mazingira ya elimu ya sekondari.
Katika hatua nyingine Serikali ya Uingereza itaongeza maradufu msaada wake katika Benki ya Maendeleo ya Afrika. Zaidi ya pauni 400milioni zimekwisha kutolewa.
No comments:
Post a Comment