Wednesday, November 21, 2007


Watanzania tukithamini, tukipe hadhi yake Kiswahili.

Angela Semaya
HabariLeo; Tuesday,November 20, 2007 @00:01

BARAZA la Kiswahili la Taifa (BAKITA) mwanzoni mwa wiki iliyopita liliadhimisha miaka 40 tangu kuanzishwa kwa baraza hilo, sambamba na kuendesha kongamano la siku nne la Kimataifa la Idhaa za Kiswahili Duniani.

Mbali na kuadhimisha kuanzishwa kwa BAKITA, lakini pia ilikuwa nafasi ya kukipa thamani Kiswahili ambacho ndicho lugha ya taifa hapa nchini, na ni lugha ambayo pia imekuwa ikithaminiwa katika nchini nyingine barani Afrika na Ulaya.

Kiswahili ndio lugha ambayo imekuwa ikiwatambulisha Watanzania popote pale wanapokwenda, ndio lugha inayotambulisha utamaduni wa Mtanzania na hivyo inapaswa kuthaminiwa.

Ni haki Watanzania kujivunia lugha hiyo ambayo inawaunganisha Watanzania ikizingatiwa kuna makabila zaidi ya 120 Tanzania, kama isingekuwa Kiswahili ingewawia vigumu kuwasiliana.

Hata hivyo, lugha hii imekuwa ikipewa kisogo na baadhi ya Watanzania ambao wanathamini zaidi lugha za kigeni badala ya Kiswahili chao.

Hali pia imeonyesha kumkera Makamu wa Rais Dk. Ali Mohammed Shein ambaye alishangazwa na udhalilishaji wa Kiswahili unaofanywa na baadhi ya watu, hasa Watanzania ambao ndio watumiaji wazuri wa Kiswahili, lakini badala yake wamekuwa wakitumia Kiingereza katika mikutano na semina na kudidimiza lugha yao.

Shein alieleza kukerwa na kushangazwa hasa Watanzania wenyewe wanapokutana hata na wadau wanaokifahamu vizuri Kiswahili, lakini huona fahari kuzungumza Kiingereza na kuongeza kuwa haki hiyo sio sawa.


Hoja ya Makamu wa Rais inapaswa kutazamwa kwa umakini kwani kweli kuna makundi ya Waswahili ambao wao kwao kuzungumza Kiingereza kwenye kadamnasi ya watu ndio usomi na kufahamu mambo.

Hii kasumba ya kuona kuzungumza Kiswahili ni kutokujua na Kiingereza ndio ujuaji inapaswa kupigwa vita kwa nguvu zote kama kweli tunataka kuitangaza na kuipa hadhi lugha yetu ya taifa.

Sio siri Watanzania wenyewe ndio wanaua Kiswahili wakati mataifa mengine kama China, Ujerumani na Waingereza wamekuwa mstari wa mbele kuitumia lugha yao na kuitangaza ipasavyo ili kuhakikisha inaenea na kujipatia umaarufu katika mataifa mengine.

Huwa ni jambo la kushangaza kuona Waswahili wenyewe kwa maringo na majivuno wanazungumza Kiingereza wanapokutana badala ya Kiswahili tena wengine hata jinsi ya kutamka maneno hayo ya Kiingereza ni matatizo matupu.

Lazima iwepo mikakati thabiti na mipango endelevu kuhakikisha lugha ya Kiswahili inapaa na kuzungumzwa katika nchi nyingine duniani ambapo hivi sasa tayari kuna watumiaji milioni 110.

Kukipigia debe Kiswahili haina maana kwamba lugha nyingine hazipaswi kutumiwa na Watanzania, la hasha! Suala la kuangalia ni kuhakikisha lugha hizo za kigeni hazipewi nafasi kubwa kuliko Kiswahili ambacho ndicho lugha ya taifa na ndio lugha sahihi inayowatambulisha Watanzania kokote kule wanapokwenda.

Kama sio Watanzania wenyewe watakaotangaza Kiswahili hakuna mtu mwingine anayeweza kusaidia kuitangaza, hivyo kuna kila sababu na haja ya jamii ya Kitanzania kufanya kila linalowezekana kukiweka juu Kiswahili.

Jamii inapaswa pia kukijengea kizazi kipya uelewa na uwezo mkubwa wa kukizungumza na kukifahamu Kiswahili maana imekuwa tofauti kidogo katika baadhi ya familia ambapo Kiingereza imeonekana kuchukua nafasi zaidi kuliko Kiswahili.

Hii haina maana Kiingereza kisitumike, kwani shule nyingi siku hizi zinatumia ufundishaji wa lugha hiyo, suala la kuzingatia ni kuhakikisha watoto pamoja na kusoma Kiingereza lakini wafahamu lugha ya kwao ni Kiswahili na inapaswa kuheshimiwa.

Vyombo vya habari navyo viwe mstari wa mbele kukizungumza Kiswahili na kuendesha programu mbalimbali za Kiswahili ili kuhakikisha Watanzania na watu wengine nje ya Tanzania wanajifunza lugha hii na kuithamini.

Basi ni wajibu wa kila Mtanzania kuhakikisha Kiswahili kinapewa nafasi na hadhi inayostahili na kuacha kasumba ya kuendekeza na kujivunia kuzungumza lugha za watu wengine.



1 comment:

Anonymous said...

hiii ni kweli kabisaaa watanzania wana ujinga mwingi sana wakizani kuongea kingereza ni maendeleo lugha yetu ni kiswahili bwana tunatakiwa tukiongee hicho sana tukiwa pamoja