Wednesday, November 21, 2007


Samson Mwigamba.

NAOMBA nianze kwa kuwashukuru sana wasomaji wangu wote waliopata kunitumia ujumbe kutokana na makala zangu mbili zilizopita na wale ambao hawakupata nafasi ya kuwasiliana nami pia.

Na leo natoa salamu za pekee makundi mawili ya wasomaji wangu. Kundi la kwanza ni la wasomaji wanaoishi mijini na ambao wamekuwa wakinipongeza sana kwa makala zangu, lakini wakionyesha wasiwasi kama kweli ujumbe unaopatikana kwenye makala tunazoandika mimi pamoja na waandishi wengine wenye uchungu na nchi hii, unafika vijijini ili kuwa chachu ya mabadiliko.

Kwa maoni yao mabadiliko yanahitajika, lakini kwa kuwa wananchi wa vijijini hawapati habari hizi, watakwamisha mabadiliko kwa kuendelea kukumbatia mambo ya kale. Nitalizungumzia zaidi hili kwenye makala ya wiki ijayo.

Kundi la pili ni la wananchi wanaoishi vijijini ambao wanajiona wamesahaulika, wanadharaulika na kutumiwa na vigogo ili kupata tu madaraka. Wamekata tamaa na hawana matumaini tena. Wanajiona kwamba wao ni wa kuishi katika umaskini tu maisha yao yote. Hawa nitawazungumzia leo na kumalizia juma lijalo.

Rafiki yangu mmoja alipata ufadhili wa raia wa kigeni akaenda kusoma katika chuo kikuu cha Kimarekani kilichoko jijini Nairobi kiitwacho United States International University (USIU). Alipofika pale alikutana na Watanzania wachache wanaosoma kwenye chuo hicho ghali kuliko vyote jijini Nairobi. Anasema wengi walikuwa ni watoto wa vigogo, hasa mawaziri na alikuwepo mama mmoja mke wa waziri.

Watoto hao wa vigogo walikuwa wakiishi na magari ya kifahari chuoni na kwa ujumla anasema maisha yao yalikuwa ya ‘kutanua’ sana.

Mwishoni mwa juma na siku za sikukuu, waliweza kusafiri hadi Dar es salaam na kurudi kwa ndege hata kama ni sikukuu ya siku moja tu.

Mara nyingi wanafunzi wa mataifa mengine walimsumbua kwa swali lile lile kwamba: “Hivi wewe ni Mtanzania kweli? Mbona maisha yako ni duni sana ukilinganisha na Watanzania wenzako tunaosoma nao hapa?”

Mara zote rafiki yangu huyu anasema alikuwa akiwaeleza kwamba Watanzania wenye maisha ya ukwasi kama ule ni wachache mno ukilinganisha na wananchi wenye hali duni kama yeye na hata chini kuliko yeye mara kumi. Na hapo walikuwa wakiongeza swali kwamba sasa kuna Tanzania ngapi?

Msomaji unaweza kujibu swali hilo? Kuna Tanzania ngapi? Je, umewahi kujiuliza pia swali hili? Ukipita mitaa ya Osyterbay, Masaki, Mbezi Beach, n.k, kisha ukaenda Manzese, Tandale kwa Mfuga Mbwa, Uwanja wa Fisi, Tandale kwa Tumbo, n.k, unapata picha gani? Unaweza kuamini kwamba Tanzania ni moja na wananchi wake wote ni sawa?

Kabla hatujaendelea, tukubaliane kimsingi kwamba haitatokea Watanzania wote wakawa sawa kiuchumi na katika hali zote.

Lakini kilichokuwa kinawashangaza wanafunzi wale wa USIU ni ile tofauti kubwa ya kiuchumi iliyokuwepo kati ya yule rafiki yangu na wale watoto wa vigogo. Kinachotufanya tujihoji leo kuna Tanzania ngapi, ni ile tofauti kubwa iliyopo kati ya maisha ya ‘walalaheri’ na ‘walalahoi’.

Huenda wasomaji wengi waliozaliwa mijini wakakulia mijini wakaishi maisha ya mijini tangu utotoni hadi leo wanaweza wasielewe kile tunachokizungumza hapa.

Nitawasimulia aina ya maisha niliyoishi kijijini kwetu na ambayo Watanzania wengi wanayaishi hata leo na ndipo unaweza kujiuliza vizuri kama kweli Tanzania ni ileile.

Nilizaliwa mwaka 1975, nikakulia Kitongoji cha Nansuruli, Kijiji cha Nakatuba, Kata ya Kibara, katika Jimbo la Mwibara wilayani Bunda, Mkoa wa Mara. Umbali baina ya Nansuruli (nyumbani) na Nakatuba ni kama kilometa 15. Na huko ndiko tulilazimika kupata huduma zote muhimu, ikiwa ni pamoja na shule, gulio la pamba (zao letu la biashara), soko (la samaki tu) na usafiri (wa msimu).

Ili tuwahi shule saa 12:30 asubuhi, ilitulazimu tuondoke nyumbani saa 11 alfajiri. Tulichapa mguu hadi shuleni, hapakuwa hata na baikeli na gari si tu kwamba halikuwepo bali hapakuwa hata na njia ya kulipitisha. Tulisoma hadi saa 6:10 mchana na wenzetu walienda nyumbani kwa chakula cha mchana hadi saa 8 mchana.

Sisi tulilazimika kukaa shuleni bila kwenda kula kwa sababu tunatoka mbali. Hata hivyo wenzetu waliporudi tuliendelea na vipindi kama kawaida hadi saa 9:30 mchana tulipoanza wakati wa kazi.

Wakati wa kazi ulikuwa ni kwa ajili ya kazi kama kulima au kupalilia mashamba ya walimu waliyojigawia kuzunguka shule.

Wengine walifanya kazi nyingine kama kufyeka, kupanda au kumwagilia maua, kupanga mawe, kuzungushia uzio kwenye nyumba za walimu, na wengine hasa wasichana walikwenda kufanya kazi za nyumbani kwenye nyumba za walimu kama vile kuosha vyombo, kudeki, kuchota maji, n.k. Tulioshinda njaa hatukupewa upendeleo, tulishiriki kazi zote hizo kama wenzetu waliokuwa wamekula.

Tulitawanyika saa 10:30 jioni na tukafika nyumbani saa 12 jioni. Tulikuta wazazi wakiwa wametuwekea ugali wa mhogo uliopikwa mchana. Ulikuwa umepoa na kuwa kiporo kigumu ambacho tulilazimika kukila kwa sababu ya njaa.

Baada ya kula tulikwenda kufuatilia mifugo kutoka machungani na kuwarejesha nyumbani na kufanya kazi kama kukamua maziwa, kuandaa moto wa kuota usiku na wazee wakati tukisubiri chakula cha usiku.

Wasichana waliporudi kutoka shule walikabiliwa na kazi kama kuchota maji, kuokota kuni na kuandaa chakula cha usiku.

Muda wa kulala ulipowadia tulitafuta ngozi za ng’ombe ambazo ndizo zilikuwa vitanda. Ngozi ambazo mchana zilitumika kwa shughuli nyingine kama kukausha nafaka, usiku tulizikung’uta mavumbi na kuzitandika chini na kulalia, tena wakati mwingine bila shuka la kutandika, na la kujifunika likiwa limechanika chanika.

Shuka lililonunuliwa likiwa jeupe ilifika mahali huwezi kutambua rangi yake maana hatukufua kwa sabuni bali mara nyingi tuliponda ponda majani ya mipapai na kutengeneza povu kidogo na kulitumia hilo kufua.

Hatukuwa na viatu. Katika shule ya wanafunzi 400 ungeweza kukuta ni wanafunzi wasiozidi 10 waliokuwa na viatu, wengi wao wakiwa ni watoto wa walimu na wazazi wachache wenye uwezo kijijini.

Tulitembea umbali wote wa kutoka nyumbani hadi shule bila viatu. Tulitembea madarasani na nje ya madarasa bila viatu, tuliingia chooni bila viatu na tulitembea sehemu zenye miiba na zisizo na miiba, bila viatu.

Siku za wikendi zilikuwa ni siku za kutafuta pesa kidogo kwa ajili ya mahitaji ya lazima kama kununua penseli/kalamu, chumvi (ile ya mabongemabonge), mafuata ya dizeli (siyo ya taa), n.k. Pesa hiyo tuliipata kwa kubeba mizigo ya kuni kwenda kuuza mjini umbali wa zaidi ya kilometa 20.

Nakumbuka mimi nilikuwa nikiuza mzigo wangu kwa sh 10 na dada na shangazi wao waliuza sh 30 kila mmoja. Mizigo ya kuni ya watoto watatu au wanne wakati mwingine, yote ilibebwa kwenye kichwa kimoja tu cha mama yangu kutoka mlimani na kuleta nyumbani.

Hivi leo mojawapo ya majukumu niliyonayo ni kushughulikia matibabu ya mama ambaye anasumbuliwa sana na kifua. Madaktari wamethibitisha kwamba kiliharibiwa na mizigo mizito aliyokuwa akiibeba zamani.

Hospitali iliyoko karibu zaidi na kwetu ni ya mission ambayo iko umbali wa kilometa kama 25 hivi kutoka nyumbani. Mama yangu alipoumwa uchungu wa mtoto wa sita alisindikizwa kwa mguu kwenda hospitali.

Kwa sababu ya kutembea na uchungu ukiwa umeanza, alizidiwa na kukimbilia kwenye kichaka kilichokuwa karibu na njia na akajifungua mtoto wa kike akiwa nusu ya safari ya kutoka nyumbani kwenda hospitali.

Msomaji, hii si hadithi ya kubuni. Nimekusimulia maisha halisi ambayo mimi mwenyewe nimeyaishi nikiwa kijijini. Na si kwamba nimesimulia kila kitu bali mengine nimeyaacha kwa sababu ya nafasi niliyonayo kwenye gazeti haitatosha.

Na nikukumbushe kwamba haya si tu maisha ya miaka ya 70 bali ni maisha wanayoishi ndugu zetu hata sasa. Mwezi Desemba mwaka jana nilikwenda kijijini kuhudhuria mazishi ya babu yangu. Na hakuna kilichobadilika sana, isipokuwa tu wananchi sasa wameamua kujenga shule ya msingi pale Nansuruli kitongojini. Hata hivyo, ile shule ina walimu wawili tu.

Hayo ndiyo maisha ya baadhi ya Watanzania. Chukua maisha hayo yalinganishe na maisha ya mawaziri, makatibu wakuu, wakuu wa wilaya na mikoa, wafanyabiashara wakubwa, na vigogo wengineo, halafu ujibu swali: Tanzania ziko ngapi? Ni lini hawa wananchi wa vijijini nao wataiona Tanzania ya akina Lowassa na Kikwete inayopaa kiuchumi?

Juma lijalo, tutaangalia kwa kinagaubaga tumaini gani lingalipo kwa wananchi hawa ambao wengine katika ujumbe walionitumia walionekana dhahiri walikuwa wanalia wakati wakiniandikia. Nitawaandikia waraka maalum vijana wa Tanzania nzima tutafakari nini kifanyike. Usikose kuusoma.

smwigamba@yahoo.com
0784 815 499 au 0712 012 514

No comments: