Friday, January 18, 2008


Alimojificha Ballali

Na Waandishi Wetu
WAKATI mahali alipo aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Dk. Daudi Ballali pakifanywa siri kubwa na Serikali, timu ya upelelezi ya gazeti hili imebaini mahali ‘alipojificha’

Uchunguzi wa kina ulioendeshwa na gazeti hili kwa kuhusisha watu mbalimbali wa ndani na nje ya nchi, ulibaini jina la hospitali alikolazwa ambalo kwa muda mrefu lilikuwa siri kubwa.

Katika uchunguzi wetu wa kina, umebaini kuwa Ballali, ambaye juzi (Jumatano) alifutiwa viza yake na Ubalozi wa Marekani nchini, ambao pia unadai haujui yuko eneo gani, amelazwa katika Hospitali ya Permina, iliyopo ‘ndani ndani’ ya mji wa Boston katika Jimbo la Massachusetts, Marekani.

Chanzo chetu cha habari kilizidi kupasha kuwa hospitali hiyo ndiyo aliyopelekwa Ballali kwa uchunguzi wa afya yake wakati akiwa Gavana wa BoT.

Awali timu ya uchunguzi ya gazeti hili iliamua kusaka jina la Ballali katika hospitali zote zilizopo katika mji wa Boston, ili kujua wapi alikolazwa lakini iliambulia patupu.

Hospitali ‘zenye kueleweka’ ndani ya Boston ni, Arbour, Beth Israel Deaconess, Boston, Brigham and Women’s, Carney, Children’s Hospital Boston, Dana-Farber Cancer Institute, Faulkner na Franciscan Children’s Hospital & Rehab Center. Nyingine ni Kindred, Vencor, Hebrew Rehab Center, Jewish Memorial, Joslin Diabetes Center, Lemuel Shattuck, Erich Lindemann Mental Health Center, Mass. Eye & Ear Infirmary, Massachusetts, Mass. Mental Health Center na Mattapan Community.

Zipo pia New England Baptist, Solomon Mental, St. Elizabeth’s, St. Margaret’s Center for Women & Infants, Shriner’s, Spaulding Rehab, Tufts-New England na VA Hospital Jamaica Plain.

Alipokosekana katika hospitali hizo, timu ya uchunguzi iliamua kupeleleza jina la Ballali kama limo katika hospitali nyingine zilizopo kwenye Jimbo la Massachusetts, huko nako ilimkosa.
Massachusetts lina miji mingine 87 inayounda jimbo hilo, lakini katika miji yote hiyo Boston ndiyo jiji maarufu na mashuhuri zaidi.

Lakini uchunguzi wetu wa kina ulibaini baadaye kuwa Ballali, alilazwa katika Hospitali ya Permina. Kabla ya hapo timu yetu ilikuwa na ‘hofu’ huenda Ballali, amelazwa Permian Regional Medical Center, ambayo inatoa zaidi huduma kwa wakazi wa maeneo ya Andrews County, pamoja na jamii inayozunguka eneo la Texas na New Mexico, lakini chanzo chetu kilituhakikishia yupo katika Hospitali ya Permina (tazama picha ya jengo mbele).

Ballali kwa sasa yupo katika hospitali hiyo kwenye Jimbo la Massachusetts moja kati ya majimbo yanayounda Marekani, akipata matibabu lakini yaliyo ya siri zaidi.

Lakini pia uchunguzi wetu umebaini kufutiwa viza kwa Ballali, huenda ikawa ‘geresha’ kwani mkewe, Anna Muganda ana uraia wa Marekani na makazi yake yapo katika mji wa Boston.

Ballali mmoja kati ya watu waliokuwa wakiheshimika duniani kutokana na kuzisaidia nchi nyingi zikiwemo Kenya na Lesotho, kabla ya kufanya kazi Umoja wa Mataifa (UN), ‘alilazimishwa’ na Rais mstaafu Benjamin Mkapa kurejea nyumbani ili kuiongoza BoT, ingawa kuna madai alikuwa hataki kurudi nchini.

Alipoulizwa na gazeti hili jana (Alhamisi) kuhusu hatua ambayo Serikali itachukua kwa sasa, Waziri wa Usalama wa Raia, Harith Bakari Mwapachu alitaka mwandishi amuulize Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali Said Mwema. IGP Mwema alipopigiwa hakupatikana, huku msaidizi wake akisema kuwa bosi wake alikuwa mkutanoni.

Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Robert Manumba naye alipopigiwa simu yake ilikuwa ikiita bila kupokelewa.

Hivi sasa BoT haikaliki kwa wafanyakazi wengi, kwani wengi kati yao wamejikuta wakiitwa kila mara katika ofisi za Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), ili kutoa maelezo kutokana na ufisadi uliotendeka ndani ya chombo hicho muhimu kwa Taifa.

No comments: