Sunday, January 20, 2008

Ballali aja

na Charles Mullinda



KASHFA ya ubadhirifu wa fedha za Benki Kuu ya Tanzania (BoT), imeanza kuchukua sura mpya, baada ya aliyekuwa gavana wa benki hiyo, Daudi Ballali, kuanza maandalizi ya kurejea nchini huku akiwa na vielelezo nyeti na muhimu vya sakata hilo zima.

Habari za uhakika ambazo Tanzania Daima Jumapili imezipata, zinaeleza kuwa Ballali anajiandaa kurejea nchini akiwa na vielelezo vinavyowaonyesha wahusika wakuu wa ubadhirifu huo, wakiwemo viongozi wa juu serikalini.

Mmoja wa viongozi wa juu wastaafu wa serikali ambaye amekuwa akiwasiliana na Ballali katika siku za karibuni, amelieleza gazeti hili kuwa alizungumza naye Alhamisi usiku wiki hii na kumhakikishia kwamba anajiandaa kurejea nchini akiwa na ushahidi wa wahusika wakuu wa sakata hilo.

Kiongozi huyo ambaye jina lake tunalihifadhi, alisema kwamba kwa siku kadhaa sasa tangu uteuzi wa wadhifa wake katika BoT ulipotenguliwa na Rais Jakaya Kikwete, amekuwa akiwasiliana na watu kadhaa mashuhuri wanaoheshimika hapa nchini pamoja na wanasheria.

Alisema Ballali ambaye sasa yuko nyumbani kwake nchini Marekani baada ya kutoka hospitalini, hali yake inaendelea vizuri na amekuwa akiongoza jitihada za kukabiliana na tuhuma zinazomkabili yeye mwenyewe, huku akisaidiwa na watu walio karibu naye.

Kiongozi huyo alimkariri Ballali akieleza kuwa alisikitika sana kuona sakata zima la kashfa hiyo likimwangukia yeye, wakati baadhi ya viongozi wakuu serikalini wakiwa wanafahamu fika kuwa alichokuwa akikifanya ni utekelezaji wa amri za wakubwa.

Katika kile kinachoonyesha kuunga mkono hoja hiyo ya Ballali, baadhi ya wataalamu waliobobea katika nyanja za uchumi na fedha, walilieleza gazeti hili kuwa kwa kawaida, gavana wa Benki Kuu hana mamlaka ya kuidhinisha utoaji wa fedha kwa ajili ya kuilipa kampuni au mtu fulani, ama kutolipwa mtu au kampuni fulani.

Mabingwa hao wa uchumi walieleza kuwa maelekezo ya kutolewa fedha za serikali kwa malipo ya aina yoyote, hutolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha.

Habari zaidi kutoka kwa watu walio karibu na Ballali, zinaeleza kuwa chanzo cha ugunduzi wa kashfa ya BoT ni malipo ya zaidi ya sh bilioni 30 yaliyofanywa kwa Kampuni ya Kagoda Agriculture Ltd, fedha hizo zililipwa kwa kampuni hiyo ikiwa haijafanya kazi yoyote inayostahili kulipwa kiasi hicho cha fedha.

Hata hivyo, ilielezwa kuwa Ballali hakuhusika na uidhinishaji wa malipo hayo, bali yalifanywa kwa maelekezo ya kiongozi mmoja wa juu katika Serikali ya Awamu ya Tatu ambaye Ballali ana nakala yake ya kutoa maagizo maalumu ya maandishi ya kufanya malipo hayo.

Hili linaonyesha kuwa maelezo ya hivi karibuni yaliyotolewa na Waziri wa Fedha, Zakia Meghji, yakieleza kwamba Ballali alimshauri kuidhinisha malipo hayo kwa ajili ya kazi maalumu za serikali si sahihi, bali Ballali alitumiwa kama mjumbe wa kutolewa kwa fedha hizo.

Inaelezwa zaidi kwamba sehemu ya fedha zilizochukuliwa katika Akaunti ya Malipo ya Nje (EPA) na kulipwa kwa Kampuni ya Kagoda Agriculture Ltd, ziliingizwa isivyo halali katika kampeni ya Uchaguzi Mkuu mwaka 2005, zikikinufaisha moja ya vyama vya siasa, kilichoshiriki uchaguzi huo.

Hata hivyo Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Yusuph Makamba jana alilieleza gazeti hili kupitia simu yake ya kiganjani kuwa chama chake hakihusiki na kupatiwa fedha hizo.

"Kwanza, siijui kabisa kampuni hiyo ya Kagoda, na chama changu huwa hakipokei fedha kutoka kwenye makampuni, zikija za msamaria mwema kama wewe, nazipokea na ninatoa risiti…hesebu zetu ziko wazi, zimekaguliwa na juzi tu tumezipeleka kwa Msajili wa Vyama," alisema Makamba.

Lakini Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Dk. Willbrod Slaa, alipoulizwa kupitia simu yake ya kiganjani, alisema ushahidi wa mazingira unaonyesha kuwepo kwa uwezekano mkubwa wa fedha zilizochotwa BoT kutumika katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005.

Kwamba ushahidi huo unaonyesha kuwepo kwa uwezekano wa fedha hizo kutumiwa na CCM katika kusaka ushindi.

"Ukiangalia mwenendo wa uchotaji wa fedha hizo, utaona kuwa zilianza kuchotwa Agosti 1, 2005, wakati huo CCM ilikuwa katika mchakato wa kuwapata wagombea ubunge wa chama hicho.

"Ziliendelea kuchotwa hadi Oktoba 27, wakati aliyekuwa mgombea mwenza wa wadhifa wa urais kupitia CHADEMA alipofariki dunia, ndipo uchotaji huo ukakoma.

"Makamba anapaswa aeleze ni kina nani walioichangia CCM kutengeneza fulana na vifaa vingine, ilivyotumia katika kampeni za uchaguzi huo," alisema Dk. Slaa.

Wakati hayo yakiendelea, kwa wiki nzima sasa baadhi ya viongozi wakuu wastaafu wa serikali na watu wengine mashuhuri wamekuwa wakitafakari kwa kina suala hili la kashfa ya ubadhirifu katika akaunti ya EPA.

Tanzania Daima imethibitishiwa na watu walio karibu na viongozi hao kuwa mmoja wa viongozi hao ametahadharisha wenzake katika moja ya vikao vyao kuwa iwapo suala hilo litafuatiliwa kwa usahihi, baadhi ya viongozi wa juu waliopo madarakani sasa na baadhi ya waliokuwa madarakani katika Serikali ya Awamu ya Tatu ambao majina yao tunayo, wanaweza kupoteza nyadhifa zao, heshima zao, ama kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria kujibu tuhuma za ubadhirifu wa fedha za umma.

Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa mbali na mfanyabiashara, Jayantkumar Chandubhai Patel, ambaye jina lake linaonekana katika kumbukumbu zilizoko kwa wakala wa utoaji wa leseni za biashara (BRELA), za orodha ya kampuni 22 zilizotajwa kuhusika na upotevu wa fedha katika akaunti ya EPA, baadhi ya watu wengine mashuhuri wanaotajwatajwa kuwemo katika suala hili majina yao hayaonekani, ingawa ushahidi wa mazingira unawahusisha moja kwa moja katika kadhia hii.

Taarifa nyingine zilizolifikia gazeti hili hivi karibuni zinaeleza kuwa mwanasheria mmoja maarufu ambaye taasisi yake imetajwa kuhusika katika suala hilo la EPA ameanza kuchukua hatua za kisheria kusafisha jina lake na kampuni yake, akiamini kuwa hakuhusika kwa namna yoyote kuliibia taifa.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, tangu uamuzi wa Rais Kikwete wa kutaka kufanyika uchunguzi dhidi ya kampuni zilizotajwa kuhusika katika kashfa hiyo, ikiwemo kampuni ya mwanasheria huyo, wateja kadhaa aliokuwa akiwawakilisha kisheria wamejiondoa kwake, hivyo kumsababishia hasara ya mamilioni ya shilingi.


Kutoka Tanzania Daima.

No comments: