Sunday, January 13, 2008

JK Eleven ivunjwe yote

Ansbert Ngurumo

WIKI hii imekuwa ya watu wawili maarufu na muhimu kwa taifa letu. Hata kama hatutaki, hatuwezi kuacha kuwajadili Rais Jakaya Kikwete na Mbunge wa Karatu, Dk. Wilbroad Slaa.

Rais Kikwete amejitokeza katika matukio mawili makubwa. Kwanza, alikwenda hospitalini Muhimbili kumjulia hali ’mgonjwa wetu’ - mmoja wa waandishi wawili walioshambuliwa na kuumizwa wakiwa ofisini. Kufika kwake na kauli yake ni mambo muhimu ambayo hatuna budi kuyajadili na kuyatolea kauli nyingine.

Ni kweli, hatukuzoea kuwaona marais wakiwatembelea wagonjwa ‘wadogo wadogo.’ Lakini Rais Kikwete amejijengea sifa hiyo, na imekuwa tabia yake nzuri; si kama Rais bali kama binadamu.

Hii ni sehemu ya sifa tunazompa, anazostahili bila kushinikiza. Kimsingi, hatumpi sifa hiyo kwa kuwa anayo. Wasifu wake wa kisiasa unaonyesha kuwa Kikwete ni mtu wa wasanii, wachezaji, waandishi, kina mama, wafungwa, watoto, wachuuzi; na makundi mengine madogo madogo.

Kwa hiyo, wanaomsifu kwa hili hawakosei; wala hawana wanachomwongezea. Ndivyo alivyo. Ni sifa yake asilia.

Baadhi yetu tunamjua kuwa hapendi kufungwa na kuta za ofisi yake ya Ikulu. Ni mtu wa matembezi. Ndiyo maana inasemekana kwamba katika siku yake ya pili akiwa Ikulu, Desemba 22, 2005, alitaka kutoka kidogo kuwaona ’rafiki zake,’ hasa wale waliokuwa Mtaa wa Mindu.

Bahati mbaya kwake, wasaidizi wake (wakitambua kuwa ni mgeni wao) walimkatalia, wakaanza kumpa tuisheni ya kukaa Ikulu, kufanya kazi na kupumzika kwa amri yao, si kwa hiari yake. Hakwenda.

Naamini kwamba atakapokuwa anaandika kumbukumbu za maisha yake ya Ikulu, ataliweka tukio hili kama changamoto yake kuu katika siku za mwanzo za urais wake.

Kwa hiyo, hata tunapomlaumu kwa safari zisizoisha na zisizo za lazima ambazo zingeweza kufanywa na wateule wake nje ya nchi; tunapokuwa tunamlalamikia kwa kutokaa ofisini; kuna jambo tunakuwa tunalisahau - ‘karama’ yake hii.

Lakini huyo ndiye Kikwete. Kwa sababu hiyo, hili la kumtembelea mgonjwa wetu ni kofi moja ninalompigia Rais Kikwete katika wiki hii.

Akiwa hospitalini, alitoa kauli kwamba waandishi wasitishike, lakini wafanye kazi kwa tahadhari. Hii ni kauli tata. Tutaendelea kuijadili.

Najua maana ya kuchukua tahadhari kazini, lakini si pale kauli hiyo inaposisitizwa na Rais. Hapa ndipo maswali ya baadhi yetu yanapoanzia. Ndipo tunapoanza hata kutilia shaka hata ziara yake kwa mgonjwa wetu. Anamaanisha nini?

Kimsingi, ziara ya Rais ilidhihirisha kwamba anajua hisia za wananchi dhidi ya serikali yake. Anajua kwamba wananchi, hata sasa, wanahisi kwamba waliowashambulia na kuwaumiza Saed Kubenea na Ndimara Tegambwage si vibaka, bali vibaraka.

Ipo dhana kwamba vibaraka hao walitumwa na watu wake, kuwakomesha na kuwafunga midomo. Gazeti lao limesifika na limelalamikiwa na serikali mara kadhaa kwa kuiandika ‘vibaya’ serikali, hasa Rais Kikwete na Waziri Mkuu Edward Lowassa. Vielelezo vya malalamiko ya serikali dhidi yao, kwamba wanaandikwa vibaya, ni vingi.

Hata hivyo, wapo waliodhani vibaka hawawezi ‘kutumwa’ wawaumize watu wanaoipinga au kuikosoa serikali na viongozi wake. Lakini kumbukumbu zinaonyesha kwamba katika serikali hii ya awamu ya nne hili si jambo la ajabu.

Wala si lazima lifanywe na serikali kama serikali, bali wapambe, mashabiki na watetezi wa matendo na hali za wakubwa serikalini. Upo mfano mmoja wa haraka.

Dk. Slaa alipoibua kashfa za ufisadi na kutaja majina, wenye pesa zao walizitembeza hadi kwa waigizaji kwenye runinga ili wamuumbue Dk. Slaa kwa maigizo ya kitoto! Yapo na mengine tunayoyajua ambayo wakati wake kuanikwa haujatimia, lakini yaliwahusisha wasanii hao na yalikuwa yanasukumwa na kundi la watu wanaotetea au wanaofaidika na ufisadi serikalini.

Sasa ‘serikali’ hii inayowatumia waigizaji baada ya kushindwa kujibu hoja nzito za wapinzani, itashindwaje kuwatumia vibaka kuwanyamazisha waandishi wanaoikosoa?

Mtu mmoja ametania akisema: ‘Mtaji upo. Ni njaa ya vibaka na pesa za kina Deep Green! Hii ndiyo sifa mbaya ambayo ziara ya rais ililenga kusafisha.

Hoja ambayo jamii inapaswa imweleze Rais Kikwete ni kuwa serikali yake inawabagua waandishi wa magazeti binafsi wasiomimina sifa kwake na mawaziri wake.

Wanatengwa kwa njia nyingi. Usalama wao haulindwi, unahatarishwa na wanaopaswa kuulinda. Wanabaguliwa na idara na wizara za serikali yake, kwa njama rasmi na zisizo rasmi. Silaha kubwa inayotumiwa ni kuvinyima matangazo vyombo vyao ili ‘vishike adabu’ na hata ikibidi ‘vinyauke.’

Hata Ikulu inahusishwa katika kuwatenga. Imedhihirika pia kwamba hata wale wanaoalikwa kusafiri naye nje ya nchi ni wale wanaoweza kumwaga sifa kwake na mawaziri wake.

Si hao tu. Wasadizi wake wana orodha ya baadhi ya waandishi (Watanzania) wasioruhusiwa kukutana na Rais hata akiwa nje ya nchi. Mifano ipo.

Ndiyo, Kikwete anaitwa na anajionyesha kuwa rafiki wa waandishi, lakini katika ukosefu huu wa usalama wa waandishi, huu si urafiki wa mashaka?

Juzi mtu mwingine alinishangaza aliponieleza kwamba katika mkutano ulioitishwa na wahariri kulaani hujuma dhidi ya waandishi hao, wahariri wa vyombo kadhaa vyenye uhusiano wa moja kwa moja au wa mbali na serikali hawakushiriki kabisa – walijitenga!

Ndiyo, serikali ina wizara ya usalama wa raia, lakini ukweli unabaki kwamba usalama wa waandishi wanaoikosoa upo hatarini kutokana na ‘wahuni’ wanaojipendekeza au wanaotumwa kuitetea serikali yake.

Kumjulia hali Kubenea na kumlipia matibabu ni jambo jema, lakini haitoshi. Rais awaonye mashabiki na wapambe wake. Wanatuhumiwa kumdhuru Kubenea.

Kasi ya kwenda Muhimbili inaonyesha kwamba anatambua hisia za wananchi kuhusu tukio hili. Inaonyesha kwamba anajua baadhi ya wasaidizi wake wanatuhumiwa. Inaonyesha kwamba anataka kuonyesha kwamba anatofautiana nao, na kwamba wanajipendekeza kwake kwa njia zisizokubalika.

Awakemee na hao, awaonye kwa kauli na vitendo, hata kama ni kwa siri. Wanataka kutumaliza kwa kumtetea yeye au wasaidizi wake. Awaambie kwamba yeye ni kiongozi mkuu wa taifa, lakini ni mdogo kuliko taifa.

Zaidi ya hayo, awaambie kwamba hawawezi kutumaliza. Wataua mmoja mmoja miongoni mwetu, lakini hawataua hoja zetu. Kama ilivyo ada katika harakati za ukombozi, damu yetu itakuwa ndiyo rutubisho la hoja hizo. Zitaendelezwa na wengine wenye nguvu zaidi yetu. Na yawezekana hawatatoka kwetu, bali miongoni mwa hao wanaotetea leo, maana wakati wao utakuwa umepita.

Rais akiwakemea hao, nitampigia kofi la pili.

Kwa leo, makofi yangu mawili yatakwenda kwa Dk. Slaa na wapambanaji wenzake katika kambi ya ushindani kwa kuibua hoja nzito zilizoifanya serikali itumie muda mrefu kutafuta majibu.

Hatimaye, Rais Kikwete ametengua uteuzi wa aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu, Daudi Ballali, ambaye awali alitetewa, alijitetea kwamba hana doa.

Dk. Slaa aliitwa mwongo, Spika wa Bunge, Samuel Sitta, akasema nyaraka za Dk. Slaa ni za kughushi; baadhi ya watuhumiwa wakatishia kumshitaki. Hadi leo hakuna aliyemshitaki Dk. Slaa. Badala yake, mafisadi wameanza kudondoka.

Tukubali. Katika kipindi hiki, wapinzani wametawala siasa za Tanzania. Wanaibua maswali, serikali inahangaika kuficha; kuwatimua; kutishia kuwashitaki; mara hawashitaki; inapobanwa na wananchi inatoa sehemu ya majibu.

Hili la BoT ni sehemu ya majibu. Wala hatuna haja ya kuwashukuru wapinzani. Ni kazi yao. La msingi, tuitambue kazi yao nzuri. Na katika hili, kinara wao ni Dk. Slaa.

Wakati nikitambua hatua mwafaka aliyochukua Rais Kikwete baada ya matokeo ya uchuguzi nusu katika BoT, nasema shujaa wa sakata hili si Rais bali Dk. Slaa. Huyu ndiye shujaa.

Kama alivyoandika Mwanakijiji, Kikwete hajasafisha BoT, amepangusa. Hajajibu hoja nzima ya wapinzani na Watanzania kuhusu ufisadi Benki Kuu. Kama Rais anataka kuwa shujaa wetu, basi aisafishe BoT. Ballali hakufanya kazi peke yake; na ‘hakuiba’ peke yake. Asitenguliwe peke yake. Hawezi kuwajibika peke yake.

Na wananchi wanatambua kuwa Ballali alikuwa kiungo tu katika JK Eleven iliyotangazwa na Dk. Slaa pale Mwembe Yanga, Dar es Salaam, Septemba 15, 2007. Ndiyo, yeye kapewa kadi nyekundu, lakini mechi inaendelea.

Tunachotaka ni hiki: Ili sifa za Kikwete zikamilike, JK Eleven ivunjwe yote. Baada ya hapo tutakuwa na mashujaa wawili - JK na Dk. Slaa. Hadi sasa shujaa wetu ni Dk. Slaa.

ansbertn@yahoo.com +447828696142 www.ngurumo.blogspot.com

Kutoka Tanzania Daima, Jumapili 13 Januari 2008

No comments: