Wednesday, January 23, 2008


Mohammed Raza:

'Baadhi ya wabunge CCM wanafiki'

Na Mwandishi Wetu


MFANYABIASHARA maarufu wa Zanzibar, Bw. Mohammed Raza, amesema unafiki wa baadhi ya wabunge wa CCM katika kuzungumzia mambo yenye maslahi kwa umma, unatoa nafasi kwa wapinzani wanaozungumza ukweli kung'ara katika medani ya kisiasa.

Bw. Raza ambaye pia ni kada wa CCM, amesema kashfa ya ufisadi iliyoikumba Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ni mfano mzuri ambao baadhi ya wabunge wa CCM, walitaka kuifunika, lakini wa upinzani, wakaianika.

Alisema hayo jana Dar es Salaam, alipokuwa akizungumza na Majira, kuhusu kashfa ya ufisadi wa mabilioni ya fedha, ulioikumba BoT.

"Wabunge wa CCM wafike mahali pa kuzungumza ukweli kwa mambo yanayohusu maslahi ya umma, waache unafiki unaosababisha wapinzani kung'ara kisiasa kutokana na kuzungumza ukweli na mfano ni huu wa kashfa ya ufisadi ndani ya BoT," alisema Bw. Raza.

Alisema wabunge wa CCM wana wajibu wa kumsaidia Rais Jakaya Kikwete, kwa kumweleza mambo ya ukweli yanayohusu wananchi na Taifa lao kwa jumla.

"Wanapaswa (wabunge) kujua, kwamba uongo wao kwa wananchi, unakigharimu chama chetu kwa kukimbiwa na wanachama wanaotaka kusikia ukweli," alisisitiza.

Katika mazungumzo yake, Bw. Raza alimpongeza Rais Kikwete kwa kuchukua hatua za ujasiri katika kushughulikia ufisadi ulioikumba BoT.


"Rais Kikwete amefanya kitendo cha ujasiri mkubwa mno katika kushughulikia kashfa hii ya ufisadi ndani ya BoT, kwa hakika ameirejeshea Tanzania heshima yake," alinena Bw. Raza.

Alisema kwa hatua hiyo, Rais Kikwete ameonesha jinsi Serikali yake inavyosikia vilio vya raia wake hasa katika mambo ya msingi.

Mfanyabiashara huyo alisema hata hivyo, kashfa hiyo, isielekezwe kwa Dkt. Daud Balali peke yake, kwa sababu inahusisha watu wengi.

Pia aliishauri Serikali kushughulikia matatizo ya kiuchumi, ili kuwawezesha wananchi kuishi maisha yanayoridhisha.

"Hali ya maisha ya wananchi walio wengi ni mbaya kwa kweli na hilo linatokea wakati wachache wanaishi maisha ya kifahari sana," alisema.

Kuhusu ghasia zilizoikumba Kenya, Bw. Raza alisema wakati umefika kwa Rais Mwai Kibaki, kujiuzulu ili kuirejesha nchi hiyo katika amani na utulivu.

"Kibaki anajua kuwa mshindi katika uchaguzi wa Kenya ni Raila Odinga na chama chake cha ODM, iweje yeye sasa anataka kung'ang'ania kiti kile wakati hakushinda," alisema.

Alisema litakuwa jambo la burasa kama Rais Kibaki kwa kuzingatia umri wake, ataamua kumpisha Bw. Odinga kuongoza Kenya, hatua ambayo alisema itamaliza mvutano na mauaji ya watu wasiokuwa na hatia.

No comments: