Hii ni Made in Tanzania tu!
JOHN Nolan, yule raia wa Ireland aliyejaribu kuighilibu Serikali ya Tanzania imruhusu aanzishe mashamba ya kamba (prawns) ambayo yangeiharibu kabisa Delta ya Rufiji, alipata kuliambia gazeti moja la Uingereza kwamba kati ya nchi za “ajabu” alizopata kuishi ni Tanzania.
Nolan aliliambia gazeti hilo ya kwamba Tanzania ndiyo nchi pekee duniani ambayo Mzungu anaweza kuingia akiwa na dola tano tu mfukoni na akaondoka miaka mitano baadaye akiwa milionea!
Alitoa mfano wa yeye mwenyewe kwamba aliingia Tanzania akiwa hana kitu, lakini ‘akatengeneza pesa’ akiwa katika chumba chake cha hoteli kutokana na dili walizochonga na viongozi ambao walimwamini kwa kuwa tu ni Mzungu!
Lakini Nolan si mgeni pekee aliyepata kuikejeli Tanzania. Mwaka jana gazeti la Mtanzania lilipata kumnukuu mwekezaji mmoja kutoka China, anayefanya biashara ya kuuza kamba na kambakochi Mashariki ya Mbali, akiikejeli Tanzania kwamba rushwa yake ni “poa”.
Kwa mujibu wa Mchina huyo, ni katika Tanzania tu ambapo unaweza kumwita hakimu nyumbani kwako na kumpa rushwa ya Sh. 100,000 tu, na kisha kumpa maelekezo ya namna ya kutoa hukumu ya kesi ya mamilioni ya pesa inayokuhusu!
Lakini kama utashangaa na kutoziamini kauli hizo za Nolan na za Mchina huyo, utasemaje kuhusu hii ya Rais mstaafu, Benjamin Mkapa kuanzisha kampuni yake ya biashara (ANBEM) yeye na mkewe, mwaka 1999, akiwa bado Ikulu?. Kwa kufanya hivyo, Mkapa akawa Rais wa kwanza katika historia ya Tanzania kufanya biashara akiwa Ikulu. Historia bwana, nani hapendi kuweka historia ya ujasiriamali?
Lakini hakuishia hapo. Mwaka mmoja kabla ya kuondoka madarakani; yaani Desemba 29, 2004, Mkapa huyo huyo akashirikiana na aliyekuwa Waziri wake wa Fedha na baadaye Nishati na Madini, Daniel Yona, kusajili kampuni nyingine binafsi iitwayo Tanpower Resources Company, na akaisimamia kununua asilimia 85 ya uliokuwa mradi wa umma wa makaa ya mawe wa Kiwira mkoani Mbeya.
Lakini pia hakuishia hapo. Akautumia wadhifa wake wa urais kuhakikisha kampuni yake hiyo mpya – wakurugenzi wakiwa ni pamoja na mkewe na mtoto wake, kuingia mkataba wa kuiuzia Tanesco megawati 200 za umeme katika gridi ya taifa.
Raia wema waliohoji iwapo hakuna mgongano wa maslahi kwa Rais kufanya biashara akiwa bado Ikulu; huku akinunua kampuni ya umma (Kiwira) na kuingia mkataba wa kibiashara na kampuni nyingine ya umma (Tanesco), walinyamazishwa haraka kwa kuambiwa Mkapa ni “mjasiriamali”, na kwamba anaonyesha “ujasiriamali” kwa vitendo akiwa Ikulu! Upo hapo?
Kama hiyo haitoshi kukuthibitishia vioja vya Tanzania, utaielezeaje hii ya Jeetu Patel kufanikiwa kughushi na kuchota Sh. bilioni 90 kutoka Benki Kuu kwa kutumia makampuni manane tofauti aliyoyasajili?
Ilikuja ya kwanza ikachota, ikaja ya pili ikachota, ikaja ya tatu ikachota, na vivyo hivyo mpaka kampuni ya nane! Na bado Watanzania tunatakiwa tuamini kwamba hakuna aliyejua kuwa hati zilizotumiwa na makampuni hayo ni za kughushi, hadi majuzi ripoti ya ukaguzi ya Ernest & Young ilipotua mezani kwa Rais Kikwete!
Lakini kama hilo halikushangazi au kukushtua, hebu tafakari na hili jingine: Watanzania masikini wanapandishiwa umeme kwa asilimia 21 kwa sababu Tanesco iko hoi kifedha. Kwa nini iko hoi? Kwa sababu vigogo serikalini wameiingiza katika mikataba mibovu ya Richmond, IPTL na Songas.
Kwa sababu ya mikataba hiyo mibovu, Tanesco inailipa IPTL Sh. bilioni 3.3 kila mwezi, Songas Sh. bilioni 5.8 na Richmond Sh. bilioni 4.7. Kwa viwango hivvyo vya malipo, unahitaji kuwa na kampuni yenye utajiri wa Microsoft ya Bill Gates, kutotetereka kifedha. Na hivyo Tanesco ilitetereka. Ili isife, ikaamua kuongeza umeme kwa asilimia 21!
Hiyo maana yake ni nini? Hiyo maana yake ni kwamba Watanzania masikini na walalahoi wa nchi hii ndiyo “wanaobebeshwa” zigo hilo la Tanesco la kufidia gharama zilizosababishwa na vigogo serikalini za mikataba ya IPTL, Richmond na Songas. Cha kushangaza zaidi, vigogo hao waliotubebesha zigo hilo kwa kuingia mikataba hiyo mibovu, bado wanadunda mpaka leo serikalini!
Na bado wameona hiyo haitoshi. Sasa Serikali inajiandaa kuwasilisha bungeni muswada wa sheria kuziruhusu kampuni binafsi kufanya biashara ya kuuza umeme nchini. Yaani; Serikali inakuwa mstari wa mbele kulitafutia shirika lake (Tanesco) wapinzani wa kuliua kibiashara, tena inafanya hivyo ikiwa yenyewe tayari imeshalikamua hadi kuwa hoi bin taaban!
Na Tanesco ikifa na biashara hiyo ikashikwa na makampuni binafsi ya nje, (ambayo bila shaka baadhi ya vigogo nchini watakuwa na hisa), nani atayazuia yasipange bei ya pamoja ya kuuzia umeme (cartel) ili yanufaike zaidi kwa kuwakamua zaidi Watanzania? Na bado tunaambiwa kuna vita inayoendelea nchini ya kuwakomboa masikini.
Biashara ya chakula ipo mikononi mwa watu binafsi, nishati nayo sasa inawekwa mikononi mwa watu binafsi, maji nayo yataelekea huko huko …mwishowe sekta zote nyeti zinazohusu usalama wa taifa zitakuwa mikononi mwa watu binafsi hususan wageni. Tusisahau Nyerere alitabiri: “Mtabinafsisha hata Magereza.”
Lakini yawezekanaje mambo yote haya yatokee nchini na umma wa Watanzania ukae kimya tu? Jibu ni kwamba ni kwa sababu Tanzania ni nchi ‘poa’, nchi ya amani. Watanzania ni watu wasiotaka makuu, na ndiyo maana kina Nolan wanaamini kwamba duniani hakuna nchi kama Tanzania. Hayo aliyoyaona Nolan akiwa Tanzania ni Made in Tanzania tu. Huwezi kuyakuta kwingineko duniani!
Kutoka Raia Mwema wiki hii.
No comments:
Post a Comment