Thursday, January 31, 2008



Tanzania yapokea toka Ghana

uenyekiti mpya Umoja wa Afrika


Na Dennis Msacky, Addis Ababa, Ethiopia

RAIS wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete jana jioni alichaguliwa kuwa Mwenyekiti mpya wa Umoja wa Afrika (AU).

Rais Kikwete anampokea Rais John Kufour wa Ghana ambaye amemaliza muda na atashika uongozi huo kwa mwaka mmoja.

Mara baada ya kuchaguliwa, Rais Kikwete alisema atatumia uwezo wake wote kuhakikisha kuwa hali ya amani inarejea katika nchi za Kenya, Somalia, Sudani (Darfur), Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Akisema changamoto yake ya kwanza ni kuona hali ya amani inarejea nchini Kenya.

Alisema kuwa mgogoro unaoendelea nchini Kenya utaigawa vipande vipande nchi hiyo iliyokuwa tajiri katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Alisema mauaji yanayoendelea Kenya hayakubaliki na kutaka Baraza la Usalama la Umoja wa Afrika liimarishwe na kuwa na nguvu katika kukabiliana na mgogoro wa Kenya na mingine.

Hata hivyo, Mwenyekiti huyo mpya wa AU alisema hayo yatawezekana tu iwapo kutakuwa na mshikamano wa pamoja baina ya viongozi hao na kutumia busara na hekima za viongozi waliomtangulia kushika wadhifa huo wa juu barani Afrika.

Alisema ni aibu kusikia kila mara taarifa za migogoro katika Afrika na kutaka bara hilo liwe la usalama, amani na utulivu.

"Mimi ni mtu wa matumaini siku zote na naamini hakuna kisichowezekana, kazi kubwa iko mbele yetu, tujipange, tujizatiti, katika kujenga mshikamano wetu," alisema.

Alisema utengamano wa kisiasa ukirejea barani Afrika lazima maendeleo nayo yatakuja kwa kasi kwa sababu Afrika ni tajiri wa rasilimali lakini maskini sana hali ambayo ni changamoto kwa Afrika.

Kuhusu uchumi, alisema ni vizuri mazungumzo ya maendeleo ya kiuchumi ya Doha yakafufuliwa kwani muda mwingi umepotezwa na Waafrika kutumia muda wao mwingi kujadili siasa na migogoro inayowasumbua.

Alisema baada ya kujadili uchumi, basi mkutano ujao wa viongozi wa Afrika uelekeze nguvu zake katika kujadili miundombinu kwani ni muhimu katika kuwaunganisha Waafrika.

Aliahidi pia kuendeleza mapambano dhidi ya Ukimwi na malaria katika Afrika akisema kuwa hivyo ni vikwazo vikuu katika ukuaji wa uchumi wa bara hilo.



No comments: