Saturday, January 26, 2008

Udaku

Fideline Iranga anasakwa na polisi

Na Issa Mnally


Mwanamitindo wa siku nyingi nchini, Fideline Iranga anasakwa na polisi baada ya kudaiwa kumfanyia kitu mbaya mzungu mmoja ndani ya chumba cha ‘mtasha’ huyo mjini Zanzibar, Risasi limedokezwa....

Kwa mujibu wa chanzo chetu cha habari cha kuaminika, tukio hilo limetokea hivi karibuni wakati Fide alipokaribishwa kulala katika chumba cha mzungu huyo ambaye alikuwa safarini.

Habari zinasema kuwa mwanamitindo huyo alikwenda Zanzibar akiwa ameongozana na rafiki yake na kufikia kwa dada wa rafiki huyo ambako Fide alipewa chumba cha kulala, naye kwenda kulala sehemu nyingine.

“Chumba ambacho Fide alipewa kulala, kilikuwa kinatumiwa na mzungu huyo ambaye ni mume wa dada wa rafiki wa mwanamitindo huyo ambapo wenyeji hao walikuwa safarini nje ya Zanzibar,” alisema mtoa habari huyo.


Ilidaiwa kuwa katika chumba ambacho mrembo huyo alikaribishwa kulala, kulikuwa na kabati ambalo lilikuwa na dola za Kimarekani 1800 sawa na shilingi za kitanzania 2,156,400 ambazo zilichukuliwa na mrembo huyo.

Aidha, imedaiwa kuwa kulikuwa na shilingi 300,000 tasilimu za Kitanzania ambapo Fide nazo alizichukua usiku huo.

Mtoa habari huyo alisema kuwa mwenyeji wao huyo hakugutuka juu ya upotevu huo wa pesa hadi asubuhi wakati Fide na rafiki yake huyo walipoondoka kurejea jijini Dar es Salaam.

“Mke wa mzungu huyo aligutuka mchana alipokwenda kuweka sawa chumba alicholala Fide, ambapo alikutana na mabadiliko ikiwa ni pamoja na kulikuta kabati la nguo likiwa wazi na ndipo alipobaini kuwa fedha za mumewe zilibiwa,” kilipasha chanzo hicho.

Baada ya kubaini kuibiwa alikwenda katika Kituo kikuu cha Polisi Zanzibari kutoa taarifa na msako ulianza.

Hata hivyo, habari zinasema kuwa shemeji wa mzungu huyo hivi karibuni alitua jijini Dar es Salaam na kwenda katika kituo cha Polisi Oysterbay kumsaka mwanamitindo huyo lakini hawakufanikiwa.

Mwandishi wetu alikwenda katika kituo cha Polisi Oysterbay ambapo askari mmoja (jina tunalihifadhi) alimthibitishia mwanahabari wetu kuwa mwanamke huyo kutoka Zanzibar alifika kituoni hapo kumsaka mtuhumiwa wake.

“Ni kweli huyo dada alifika hapa kituoni na akiomba msaada wa kumsaka mtuhumiwa wake, nasi tunamsaidia,” alisema askari huyo.

Mwandishi wetu jana (Ijumaa) alimpigia simu Fide na kumuuliza kuhusu madai hayo lakini alisema kuwa hafahamu habari hizo.

“Wewe ni mwandishi wa chombo gani?” Aliuza Fide, alipojibiwa alisema “Sifahamu habari hizo.”

No comments: