Friday, February 01, 2008

Air Tanzania Corp.Ltd

yakodisha dege bovu


Ni Airbus ya kampuni ya Liberia,
inayofanyiwa ukarabati El Salvador

KAMA vile kashfa ya mahujaji haikutosha, na kama vile mlolongo wa kashfa za manunuzi mengine ya asasi mbalimbali za serikali hazijaitosheleza Serikali ya CCM, Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) nalo limeanza kukumbwa na kashfa kubwa ya ukodishaji wa ndege nzee kutoka kampuni ya Liberia.

Ukodishwaji huo wa ndege kubwa aina ya Airbus 320 MSN 630 (pichani) kutoka kampuni ya Wallis Trading Inc. ya Liberia, umezua maswali mengi ndani na nje ya shirika hilo. Ndege hiyo kubwa ina uwezo wa kuchukua abiria zaidi ya 150.

Kwa mujibu wa uchunguzi wa Raia Mwema, Shirika la ATCL, mnamo Oktoba 5, 2007, liliingia mkataba wa dola milioni 30 wa kukodisha ndege hiyo ya Airbus 320 ambayo wakati mkataba huo unaingiwa ilikuwa nchini El Salvador ikizeeka na kuota kutu.

Habari zinasema ya kwamba kabla ya ATCL kukubali kuikodisha, ndege hiyo ilikuwa inatumiwa na Shirika la Ndege la Jamaica ambalo baada ya kuitumia waliiacha katika hali hiyo mbovu iliyohitaji matengenezo makubwa.

Ingawa ndege hiyo imekodiwa na Tanzania kutoka kampuni ya Liberia, mkataba wake unaongozwa na Sheria za Uingereza. Mdhamini wa ununuzi wa ndege hiyo ni Serikali ya Tanzania ambayo kwa sasa inaongozwa na Chama cha Mapinduzi.

Uchunguzi unaonesha kuwa ndege hiyo mbovu ilikuwa El Salvador ikisubiri kuuzwa au kukodishwa kwa mdau mwenye kuja na bei nzuri. Mwanzoni wakati wa kutafuta ndege ya kukodi, memo moja ya viongozi wa juu wa ATCL ilisema kuwa shirika hilo linahitaji ndege ambayo itakapoletwa nchini “lazima watu wageuze vichwa vyao” kuiangalia inavyoruka.

Kwa mujibu wa vyanzo vya habari ndani ya shirika hilo, ambavyo kwa sababu ya wazi vimekataa kutajwa, ndege hiyo ilitakiwa iingizwe nchini Desemba 18 mwaka jana na kuanza safari zake tarehe Desemba 28. Ndege hiyo - A320-214 MSN 630 ndiyo inatarajiwa kufanya safari zake kati ya Dar-es-Salaam na Johannesburg, Afrika ya Kusini.

Habari zinasema, hata hivyo, kwamba kutokana na lile sakata la mahujaji na zaidi kutokana na matengenezo makubwa ya kuficha uchakavu wake, ndege hiyo imecheleweshwa kuingizwa nchini na sasa inatarajiwa kuingia nchini wakati wowote kuanzia sasa na kuanza safari zake katikati ya mwezi ujao.

Ndege hiyo imehitaji kufanyiwa matengenezo makubwa ambayo yamefanyika kwenye hanga ya kampuni ya Aeroman huko huko El Salvador.

Mara baada ya ATCL kukubali kuingia mkataba huo, ukaguzi ulifanyika ili kuangalia hali ya ndege yenyewe ilivyo. Uchunguzi huo ulifanywa kwa kuangalia nje na kutembea ndani ya ndege hiyo.

Taarifa ya ukaguzi huo siyo tu ilishtua vigogo wa ATCL bali pia ilionesha ni kwa kiasi gani ndege hiyo ilikuwa inahitaji matengenezo makubwa kinyume na mkataba na Wellis Trading Limited ulivyosema, lakini hawakuwa na cha kufanya kwani mkataba ulikuwa umeshaingiwa kati ya ATCL na kampuni hiyo yenye makazi yake huko Monrovia, Liberia.

Taarifa zinasema uchunguzi ulionesha kuwa ndege hiyo ilikuwa na matatizo mengi ambayo yanahitaji matengenezo makubwa. Kwa kuangalia taarifa hiyo kuna mambo hamsini (50) ambayo yanahitaji uangalizi wa karibu na matengenezo ya haraka kabla ya ndege hiyo kuweza kuruhusiwa kuruka.

Baadhi ya matatizo hayo ni pamoja na uchakavu wa vitu mbalimbali ambavyo imebidi ATCL iingie gharama ya kuvibadilisha kwani mkataba wao na Wellis Trading Inc. unasema wazi kuwa ndege inakodishwa kama “ilivyo” ukiondoa yale mambo ambayo yanasimamiwa na mtengenezaji wa ndege hiyo; yaani Airbus au mambo menginee yanayotajwa wazi.

Baadhi ya vitu ambavyo vilikuwa na uchakavu mkubwa ni pamoja na vyoo, milango, sehemu ya kuwekea mizigo, mazuria na chumba cha marubani. Hata hivyo, sehemu kubwa ambayo ilihitaji matengenezo makubwa ni uchakavu usiokifani wa viti vya abiria ambavyo licha ya kuchakaa karibu vyote vilikuwa vimenyofoka nyofoka na vilikuwa vimelegea na kutoa sauti kila mtu anapokalia.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya ukaguzi, viti vya marubani navyo ni vivyo hivyo huku chumba chenyewe cha marubani kikiwa ni kichafu ambacho mchunguzi mmoja aliyeangalia kwa karibu alisema “viti vyake vinatoa vumbi”.

Tatizo la viti kwa kiasi kikubwa limechangia ucheleweshaji wa ndege hiyo hasa kutokana na ukweli kuwa viti hivyo ni maalum na ilihitajika kuweka viti vipya kabisa kwenye ndege hiyo, gharama ambayo mwanzoni ATCL haikuwa tayari kuingia wakidai Wallis “haikuwaambia” kuhusu kiasi cha uchakavu huo.

Mmoja waliohusika na ukodishaji wa ndege hiyo alisema kuwa “Wallis hawakuweka kila kitu wazi kuhusu hali ya ndege”. Hata hivyo, haijajulikana kama viti vyote vimebadilishwa na kuwekwa vipya au ndio vimepakwa rangi tu na kufunikwa na vitambaa vipya tu.

Pamoja na hali hiyo chakavu, ATCL imeshaanza kulipia ndege hiyo na hadi hivi sasa tayari imeshalipia karibu dola milioni moja kwa Wallis na kwa kampuni ya Aeroman (mafundi) na kampuni ya Storm Aviation (wasafirishaji) ambapo marubani na wahandisi wanaoongozana na ndege hiyo pia watalipwa na ATCL.

Mapema mwezi huu, Ofisi ya Fedha ya ATCL iliidhinisha malipo hayo ya mwanzo, lakini baadaye ikabidi yasitishwe kwa sababu ya matatizo ya mahujaji. Hadi wiki iliyopita, kampuni ya ATCL ilikuwa imechelewa kufanya malipo mengine ya dola 370,000 kwa mwezi na hivyo kuadhibiwa faini ya dola 60,000 kwa mwezi.

Uamuzii wa kukodi ndege ya Airbus badala ya Boeing ulikuja baada ya kukataa ofa ya kampuni ya Boeing ambayo ilimtuma mwakilishi wake, Bw. Robert Faye, Septemba 29, 2007 kuja nchini kufanya majadiliano na ATCL.

Bw. Faye alikuja na mapendekezo ya kulisaidia shirika hilo katika kukodisha ndege kwa masharti kwamba ATCL pia iangalie uwezekano wa kununua ndege mpya kutoka kwao.



WAZIRI wa Miundo mbinu, Andrew Cheng

Afisa mmoja wa ATCL aliyeulizwa kwa nini waliamua kununua ndege hiyo ya Airbus badala ya Boeing, alisema kuwa ndege aina ya Airbus 320 ina matumizi madogo sana ya mafuta ukilinganisha na mshindani wake Boeing 737-200.

“Tunapoelekea kwenye bei ya mafuta kufika na kupita dola 100 kwa pipa, kwa kampuni kama ya kwetu ni lazima tutafute njia mbadala ya kutusaidia kuokoa mafuta na hivyo kupunguza gharama, na hivyo kuliokolea Taifa fedha nyingi”, alisema ofisa huyo aliyekataa kutajwa jina lake kwa kuwa si msemaji wa shirika hilo lakini, mwenye kulielewa kwa undani suala hilo.

Ukiondoa matatizo hayo ya kiufundi, hadi wiki iliyopita Serikali ya Tanzania, ambayo ndiyo mdhamini wa ununuzi wa ndege hiyo, ilikuwa haijatoa “guarantee” kwa shirika hilo la Wallis kwa mujibu wa kipengele cha mkataba huo.

Kwa mujibu wa mkataba huo ambao mwandishi wa Raia Mwema aliuona, guarantee ya serikali ilihitajika ipatikane ndani ya “siku tatu na si zaidi ya Oktoba 10, 2007”. Ni kukosekana kwa guarantee hiyo ndiko kumesababisha shirika hilo kudaiwa faini ya dola 60,000 kwa mwezi.

Hadi hivi sasa haijajulikana ni kwa nini serikali imeshindwa kutoa guarantee hiyo licha ya kuwaahidi mara kadhaa watu wa ATCL kuwa itafanya hivyo.

Hali hiyo inaonekana kuuchelewesha mpango mwingine wa kampuni hiyo wa kununua ndege mpya ya Airbus toka kwa watengenezaji; mpango ambao unatarajiwa kushuhudiwa na Rais Jakaya Kikwete kwenye ziara yake inayotarajiwa kufanywa nchini Ujerumani katikati ya mwezi ujao.

Wiki iliyopita kampuni ya utengenezaji wa ndege ya Airbus iliwaandikia ATCL barua yenye kumbukumbu namba CSD/ATC/2 ambayo ndani yake imewataka ATCL kukamilisha malipo ya awali ya ununuzi wa ndege hiyo mpya vinginevyo “maandalizi ya ziara ya Rais hayatawezekana bila kukamilika malipo hayo”.

Barua hiyo iliendelea kusema kuwa “kuchelewesha huku siyo tu kunachelewesha jitihada za kuifufua ATCL bali pia inaongeza gharama kubwa kwa kampuni yenu”.

Chanzo chetu cha habari karibu na kampuni ya Airbus, mjini Hamburg, Ujerumani, kimesema kuwa Airbus inafuatilia mkataba kati ya ATCL na Wallis kwani wao kama watengenezaji wa ndege za aina hiyo wana majukumu kadhaa ambayo wanatakiwa kuyatimiza kwenye mkataba huo, na hivyo ucheleweshaji wa kutoa guarantee na hatimaye kuiingiza ndege hiyo katika utendaji, unawahusu “sana”.

Ndege hiyo ambayo inatarajiwa kuingizwa nchini na marubani na mafundi wa Storm Aviation haijajulikana wazi kama taratibu zote za manunuzi ya serikali zilifuatwa na maswali kadhaa bado yanahitaji kujibiwa.

Baadhi ya maswali hayo ni pamoja na ni jinsi gani Waziri wa Miundo Mbinu, Andrew Chenge na watendaji wake walishughulikia mkataba huo wa ukodishaji dege hilo bovu ikizingatiwa kuwa Wizara hiyo tayari imeshawahi kujikuta na kashfa nyingine kadhaa huko nyuma kuhusiana na manunuzi ya ndege.

Si Chenge wala Mkurugenzi Mkuu wa ATCL, David Mattaka waliopatikana jana kuzungumzia suala hilo.


Kutoka gazeti la Raia Mwema wiki hii


No comments: