Friday, February 01, 2008

HOTUBA YA MHESHIMIWA,

JAKAYA MRISHO KIKWETE,

RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO

WA TANZANIA, KWA WANANCHI,

31 JANUARI, 2008



Ndugu Wananchi;

Ninayo furaha kwa mara nyingine tena kuzungumza nanyi kupitia utaratibu huu mzuri wa mawasiliano baina ya Rais na wananchi wa nchi yetu.

Jambo la kwanza ninalopenda kulizungumzia linahusu uzingatiaji wa sheria na taratibu za uhamiaji na kuishi nchini.

Ndugu Wananchi;
Tarehe 23 mwezi huu, nilimaliza ziara ya siku kumi Mkoani Kagera. Jambo moja nililoliona kwenye ziara hiyo ambalo sikufurahishwa nalo, ni ukiukwaji wa sheria na taratibu za uhamiaji na uingizaji mifugo nchini.

Kwa muda sasa, raia wa nchi jirani zinazopakana na Mkoa wa Kagera wamekuwa wakiingia na kuishi nchini mwetu kwa vibali vya viongozi na watendaji wa vijiji na kata. Baadhi ya watu hao pia wamekuwa wakiingiza mifugo kwa vibali vya viongozi hao hao.

Wageni hao wamekuwa wanaingia na kuishi nchini isivyo halali. Sheria na taratibu za uhamiaji zinatoa mamlaka hayo kwa Maafisa Uhamiaji tu na si vinginevyo. Viongozi na watendaji wa vijiji na kata hawana mamlaka hayo. Hivyo basi, vibali vyote walivyotoa viongozi hao si halali na havitambuliki. Napenda kurudia kauli yangu niliyoitoa Mkoani Kagera kwamba ni marufuku kwa kiongozi au mtendaji wa ngazi yoyote ile nchini kutoa kibali cha mgeni kuingia au kuishi nchini kama siyo Afisa wa Uhamiaji.

Ndugu wananchi;
Wageni wanaoishi nchini kwa kutumia vibali ambavyo havikutolewa na Idara ya Uhamiaji wanaishi isivyo halali. Wenzetu hawa wanatakiwa kufanya yafuatayo. Kwanza wajitokeze na kutoa taarifa kwa Maofisa Uhamiaji, Wilayani au katika vituo vya mpakani. Pili, iwapo watachagua kuishi nchini, wafuate taratibu zilizowekwa kuomba kibali cha kuishi nchini. Idara ya Uhamiaji ndiyo itakayoamua. Tunawapa siku sitini za kufanya hivyo. Baada ya hapo, hatua zipasazo za kisheria zitachukuliwa kwa wale ambao watakuwa hawakufanya hivyo. Nilipokuwa Mkoani Kagera niliwaagiza Mkuu wa Mkoa na Wakuu wa Wilaya kufuatilia utoaji wa vibali unaofanywa na viongozi na watendaji wa vijiji na kata katika maeneo yao. Nimewataka wawachukulie hatua zipasazo za kinidhamu watumishi hao wa umma pamoja na kuwabana wahamiaji haramu kufuata sheria za uhamiaji za nchi yetu au warudi makwao. Napenda kusema kuwa maagizo hayo ni kwa Wakuu wote wa Mikoa na Wilaya nchini kwani inawezekana matatizo haya yanaweza kuwepo katika mikoa mingine.

Najua kwamba kuna Watanzania wenzetu wanaohifadhi wahamiaji haramu kwa kuwa wananufaika kwa kuwafanya vibarua au wafanyakazi wao. Ukweli unabaki pale pale kwamba wanatakiwa waingie na kuishi nchini kwa kufuata taratibu zinazotambulika kisheria. Sheria za nchi, na sio manufaa ya mtu au watu binafsi, ni lazima zizingatiwe.

Ndugu Wananchi;
Jambo lingine baya linalofanyika katika mpaka wetu na nchi jirani Mkoani Kagera ni kuruhusu mifugo kuingia nchini holela. Hiki ni kitendo ambacho kinakiuka taratibu zinazotawala uingizaji wa mifugo kutoka nchi za nje. Pia ni kitendo cha hatari kwani kinaweza kupelekea mifugo yenye maradhi kuingia nchini bila kudhibitiwa na kusababisha maafa makubwa nchini. Kanuni na taratibu zimewekwa kisheria kutawala mifugo kuvuka mipaka na kuepusha hatari za namna hiyo zisitokee.

Jambo linalonishangaza ni kwa nini viongozi wetu hawa hawajifunzi kutoka kwa majirani zetu. Wakati wote tulipofanya zoezi la kurudisha makwao wakimbizi au wahamiaji wasiokuwa halali na mifugo yao wenzetu waliweka sharti la mifugo hiyo hiyo iliyotoka kwao ichanjwe kwanza kabla ya kuvuka mpaka hata kama mifugo hiyo ilitokea nchini kwao na kuja kwetu. Nilidhani hili lingekuwa fundisho kwa viongozi wetu hawa kuwa thabiti kuhakikisha kuwa mifugo kutoka nchi jirani inachanjwa kabla ya kuvuka mpaka kuja Tanzania. Lakini, hawajali kufanya hivyo. Mkuu wa Mkoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi Watendaji wa Wilaya na viongozi na watendaji wa vijiji na kata kuhakikisha kuwa hakuna mifugo inayoingia nchini holela. Lazima sheria na kanuni husika zizingatiwe.

Aidha, nimeelezwa juu ya kufahamika kuwepo vivuko haramu kadhaa mpakani. Nimesema nilipokuwa Kagera na narudia tena leo kwamba, maadamu vivuko hivyo vimejulikana lazima tuvidhibiti. Kadhalika tuanzishe vituo mpakani vya kupokelea mifugo na kila anayeingia na mifugo lazima apitie hapo na kupata idhini husika. Nimetaka viongozi wenzetu hao wasimuonee haya mtu yeyote anayeingiza mifugo nchini kinyume cha sheria na taratibu zilizopo. Kadhalika viongozi na watendaji wanaozembea wachukuliwe hatua kali za kinidhamu mara inapobainika kuwa mifugo imeingia kinyume na taratibu katika maeneo yao.

Kama ilivyo kwa uhamiaji usio halali, tatizo la kuingiza mifugo kinyume na utaratibu linaweza kuwepo mikoa mingine nchini. Hivyo, maagizo haya ni kwa mikoa yote na wilaya zote nchini. Pia yanaihusu Wizara ya Maendeleo ya Mifugo. Lazima Wizara itoe uongozi katika jambo hili muhimu kwa usalama na maendeleo ya mifugo yetu nchini. Napenda kuwakumbusha Watanzania wenzangu kuwa hakuna nchi yoyote duniani inayoruhusu mifugo kuingia holela. Si vizuri Tanzania kuwa ndiyo nchi pekee inayofanya hivyo. Wenzetu na hata hao majirani zetu wanatustaajabu.

Ndugu Wananchi;
Jambo la pili ninalopenda kulizungumzia ni matatizo yanayoukabili uchumi wa dunia hivi sasa. Bado bei ya mafuta iko juu sana na kuathiri uchumi wa nchi zote duniani tajiri na maskini ingawaje nchi maskini zinaathirika zaidi. Hili si jambo geni kwetu. Napenda kurudia kauli zangu za siku za nyuma kwamba, hatuna uwezo mkubwa wa kujikinga na athari za bei za mafuta. Hata hivyo, hatuna budi tuendelee kuwa waangalifu na hasa wabanifu katika matumizi ya mafuta. Tuepuke matumizi yasiyo ya lazima.

Wakati huo huo tunaendelea na juhudi za kuzalisha nishati mbadala kutokana na mimea hususan miwa, mawese na mbono-kaburi (jatropha). Juhudi hizo zikifanikiwa zitatusaidia kupunguza mzigo wa mafuta tunayoyaagiza kutoka nje. Nafurahi kwamba juhudi zetu zina muelekeo mzuri na katika miaka michache ijayo tutaanza kunufaika na matunda yake. Pamoja na hayo tunaendelea na juhudi za utafutaji wa mafuta na gesi asilia hapa nchini. Mpaka sasa leseni 22 za utafutaji mafuta na gesi asilia zimetolewa na kazi inaendelea katika hatua mbalimbali. Tuzidi kumuomba Mwenyezi Mungu atujaalie rehema zake na sisi tujaaliwe kugundua mafuta mengi hapa nchini yatakayotosheleza mahitaji yetu na ziada ya kuuza nje.

Ndugu Wananchi,
Tatizo lingine kubwa linaloukabili uchumi wa dunia sasa linatokana na matatizo yanayoukabili uchumi wa Marekani. Uchumi wa taifa hilo ambao ndiyo mkubwa kuliko wowote duniani umekuwa unapita kwenye misukosuko kwa miezi kadhaa na katika wiki chache zilizopita hali ikawa ngumu zaidi. Kasi ya ukuaji wa uchumi imepungua na thamani ya dola imeshuka. Serikali ya nchi hiyo imeanza kuchukua hatua za kukabiliana na matatizo hayo. Lakini, kwa kuwa uchumi wa Marekani ndiyo uchumi mkubwa kuliko wowote duniani na uchumi wa nchi nyingi duniani una uhusiano nao, matatizo ya uchumi wa nchi hiyo huathiri nchi nyingi. Na sisi Tanzania hivyo hivyo.

Nimeelekeza wachumi wetu wafanye uchambuzi wa kina juu ya athari hizo na kushauri hatua za kuchukua kupunguza makali yake. Moja ya jambo ambalo liko wazi ni lile la kushuka kwa thamani ya dola ya Kimarekani. Sisi tunaweka sehemu kubwa ya akiba yetu ya fedha za kigeni katika dola za Kimarekani. Ni dhahiri kwamba kushuka kwa thamani ya dola za Kimarekani kunatupunguzia uwezo wetu wa kuagiza bidhaa nchi za nje.

Uchunguzi wa Akaunti ya EPA

Ndugu Wananchi;
Jambo la tatu ambalo nimepanga kuliongelea leo ni hili suala la ukaguzi wa Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje na hatua zinazoendelea kuchukuliwa baada ya taarifa ya ukaguzi kutolewa.

Ndugu Watanzania wenzangu;
Kwa mara nyingine tena nawapongeza na kuwashukuru wakaguzi wa Kampuni ya Ernst and Young kwa kazi nzuri waliyoifanya na kutoa taarifa ya kina kuhusu matatizo yahusuyo matumizi ya fedha za Akaunti hiyo. Nawashukuru pia Watanzania wenzangu kwa kuunga mkono hatua tulizochukua na tunazoendelea kuchukua kuhusu suala la Benki Kuu. Hata hivyo, nasikitishwa na taarifa ninazozipata kuhusu kuwepo uvumi mwingi unaoenezwa na baadhi yetu kuhusu suala hili. Baadhi ya uvumi huo umekuwa unapotosha ukweli na kuwachanganya wananchi. Napenda kutumia nafasi hii kuwaomba wanaoeneza uvumi na uongo kuacha kufanya hivyo. Aidha, nawasihi wananchi wawe watulivu na wavumilivu.

Napenda kuwahakikishia kuwa, Serikali inayo dhamira ya dhati ya kulifuatilia suala hili mpaka mwisho wake ujulikane. Mwisho ambao utakuwa na maslahi kwa taifa letu. Pamoja na yote yatakayofanywa, tunataka kuhakikisha kuwa fedha zilizolipwa kinyume cha utaratibu zinarudishwa. Mwanasheria Mkuu wa Serikali na wenzake, yaani Mkuu wa Jeshi la Polisi na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU wameanza kuchukua hatua. Nimewataka watoe taarifa kwa wananchi mara kwa mara kadri inavyowezekana pamoja na haja ya kuwa waangalifu kutokutoa mengi yahusuyo uchunguzi wanaoufanya ili ushahidi usiharibike.

Nawaomba Watanzania wenzangu tuwe na subira. Naamini kazi hii itakamilika ndani ya kipindi cha miezi sita tuliyowapa. Napenda kurudia ombi la Serikali kwa wananchi wenye taarifa zitakazosaidia katika uchunguzi na hatua katika suala hili waisaidie kamati yetu hiyo.

Ujio wa Rais Bush

Ndugu Wananchi;
Natumai mmesoma na kusikia taarifa katika vyombo vya habari kuhusu ziara ya Rais George W. Bush wa Marekani katika nchi yetu kunako katikati ya mwezi Februari, 2008. Tunaendelea kukamilisha ratiba na itakapokuwa tayari tutawapeni taarifa. Hilo ndilo jambo langu la nne leo.

Napenda kutumia nafasi hii kuwaomba Watanzania tumpokee mgeni wetu huyu kwa mujibu wa mazoea na desturi za ukarimu wa Kitanzania. Huu ni ugeni mkubwa na wa heshima kubwa kwa nchi yetu. Rais Gerorge Bush ameipa heshima kubwa nchi yetu kwa kuamua kutumia sehemu kubwa ya ziara yake ya Bara la Afrika hapa kwetu. Ameonyesha upendo mkubwa kwetu nasi tumuonyeshe hivyo hivyo. Nawaomba Watanzania tujitokeze kwa wingi siku hiyo kumpokea mgeni wetu huyo mashuhuri.

Ziara hii ni uthibitisho wa kuimarika kwa mahusiano kati ya Marekani na Tanzania. Mahusiano hayo mazuri yameinufaisha nchi yetu. Marekani sasa ni moja ya nchi zinazoongoza kwa kutoa misaada ya maendeleo kwa Tanzania. Tangu mwaka 2003 kwa mfano, imekuwa inatoa msaada mkubwa ambao umetusaidia sana katika mapambano yetu dhidi ya maradhi ya UKIMWI nchini Tanzania. Kadhalika, Marekani imetusaidia sana katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa malaria nchini.

Ndugu Wananchi,
Wakati wa ziara yake hapa nchini, Serikali ya Marekani inatarajia kutiliana sahihi msaada mkubwa wa maendeleo unaoelekezwa katika kuboresha miundo mbinu ya barabara, umeme na maji. Kwa msaada huo utakaotolewa kupitia Programu ya Mfuko wa Changamoto ya Millenia utatusaidia kutatua baadhi ya matatizo yaliyoonekana sugu katika baadhi ya maeneo hapa nchini.

Pamoja na hayo, ziara ya Rais George Bush nchini mwetu itasaidia kuitangaza nchi yetu na kuinufaisha sana utalii na uwekezaji hasa kwa soko la Marekani na marafiki zake. Tayari katika miaka miwili hii tumeshuhudia ongezeko kubwa la watalii wa Kimarekani kutembelea nchi yetu. Hivi sasa Wamarekani ndiyo wanaoongoza kwa idadi ya watalii wanaotembelea hifadhi za Ngorongoro na Serengeti. Naamini baada ya ziara ya Rais wao watalii wengi zaidi wa Kimarekani watakuja. Hali kadhalika, wawekezaji wengi wa kutoka Amerika watajenga imani ya kuja kuwekeza nchini.

Ndugu Wananchi,
Wapo watu miongoni mwetu na hata nje wanajaribu kueneza uvumi wa uongo na kuihusisha ziara hii na masuala ya Makao Makuu ya Kamandi ya Afrika ya Jeshi la Marekani. Ni uongo na uzushi mtupu. Ziara hii haihusu hayo. Masuala hayo si agenda na wala Marekani haijaiomba Tanzania kuwa mwenyeji wa Kamandi hiyo. Nawasihi Watanzania wenzangu tupunguze hii tabia ya kuzusha na kueneza uongo. Tunajitia hofu wenyewe na wenzetu bila sababu. Haina tija yoyote. Nawaomba tujitokeze kwa wingi kumpokea mgeni wetu huyu. Aondoke nchini salama na arejee kwao akiwa na kumbukumbu nzuri ya nchi yetu na watu wake.

Hali ya Kenya

Ndugu Wananchi;
Jambo la tano ninalotaka kulizungumzia ni hali ya kisiasa na kiusalama ya nchi jirani na rafiki ya Kenya. Kwa kweli inatusikitisha na kutuletea simanzi kubwa. Mioyo yetu inauma kuona na kusikia yanayotokea nchini humo. Jitihada yangu ya kuzungumza na pande zote zinazohasimiana pamoja na zile zilizofanywa na zinazoendelea kufanywa na wenzetu wengine bado hazijazaa matunda. Sisi hatutachoka na wala hatutaacha kuzungumza na pande zinazohusika kuhusu kuacha uhasama, kuacha na mapigano na kutafuta maridhiano kwa njia ya mazungumzo.

Tunaahidi kuendelea kuiunga mkono Kamati ya Mhe. Kofi Annan (Katibu Mkuu Mstaafu wa Umoja wa Mataifa), Rais Mstaafu, Mhe. Benjamin Mkapa na Mama Graca Machel. Viongozi wetu hao wanaifanya kazi hiyo kwa niaba ya Umoja wa Afrika wanastahili msaada wetu na kuungwa mkono nasi. Aidha, tutaendelea kushirikiana na viongozi wenzetu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika kusaidia juhudi za upatanishi. Napenda kutumia nafasi kurudia tena yale maombi yangu kwa viongozi wa PNU na ODM na wananchi wote wa Kenya kuyapa mazungumzo nafasi ya kumaliza tofauti zao. Mapanga, marungu na hata bunduki zisipewe nafasi, kamwe hazitasaidia.

Tutenganishe Uongozi na Biashara

Ndugu Wananchi;
Jambo la mwisho ninalotaka kulizungumzia linahusu maadili ya uongozi nchini. Hususan napenda kulizungumzia suala la viongozi wa siasa Mawaziri na Wabunge kuwa pia watu wanaojihusisha na shughuli za biashara moja kwa moja. Upo ushahidi wa kuwepo migongano ya maslahi kwa baadhi. Lakini, pia, hata pale ambapo hakuna dalili za wazi, hisia za kupata manufaa yanayotokana na nafasi zao hutawala. Matokeo ya yote hayo ni watu kupoteza imani na kutilia shaka uadilifu wa viongozi wetu.

Ndugu Wananchi;
Nchi za wenzetu hasa zile za kibepari zinazo taratibu nzuri za kushughulikia hali hizo. Wenzetu wanao utaratibu unaomtaka mtu mwenye shughuli za kibiashara anapokuwa Mbunge au Waziri kuacha kujishughulisha na biashara zake. Unakuwepo utaratibu rasmi unaotambuliwa kisheria wa wadhamini wanaoendesha hizo shughuli bila ya yeye kujihusisha nazo. Anapoacha uongozi wa siasa kama atapenda atachukua tena mali yake na kuendelea na shughuli zake.

Ni makusudio yangu kuwa utaratibu huu tuuanzishe hapa nchini. Viongozi wetu wachague kufanya jambo moja kwa wakati mmoja ama biashara au Ubunge na Uwaziri. Kwa ajili hiyo ni makusudio yangu kuanzisha mchakato wa kufanya marekebisho ya Sheria ya Maadili ya Uongozi ili tuingize utaratibu huo.

Ndugu wananchi;
Ni jambo lenye maslahi kwa nchi yetu na litasaidia sana kujenga heshima ya viongozi wa umma mbele ya macho ya wananchi. Nafurahi kwamba suala hili tumelizungumza katika kikao maalum cha Kamati Kuu ya CCM tulichofanya Dodoma juzi tarehe 29 Januari, 2008 na tumeelewana. Ni matumaini yangu kuwa sote tutaunga mkono.

Mwisho, nawatakia kila la heri kwenye shughuli zenu. Tuendelee kushirikiana kuijenga na kuiendeleza nchi yetu.

Asanteni sana kwa kunisikiliza

No comments: