Jakaya Kikwete awakuna wengi
waandishi wetu, dar, dodoma
WABUNGE, wasomi na wananchi wa kawaida, wamempongeza Rais Jakaya Kikwete kwa hotuba yake ya mwishoni mwa mwezi uliopita, hasa kwenye kipengele cha kuwataka matajiri kuchagua moja — biashara au uongozi.
Wasomi kadhaa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, wamesema maadili ya uongozi yamevurugwa kwa kiasi kikubwa na kueleza kwamba Rais Kikwete hapaswi kuongojea sheria mpya ya maadili, badala yake anapaswa kuchukua hatua sasa.
Wakizungumza na MTANZANIA katika majengo ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Mlimani, baadhi ya wasomi wa fani ya sheria walisema Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma ya mwaka 1985 haijafanyiwa kazi, hivyo hakuna haja ya maboresho ya sheria hiyo.
Mwanaharakati maarufu ambaye pia ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Mwesiga Baregu, alisema Rais Kikwete ametangaza vita ngumu, hasa pale inapoaminika kuwa mawaziri wake wengi ni wafanyabiashara.
Profesa Baregu alisema katika vita hiyo, Rais Kikwete hana mbinu nyingine za ushindi zaidi ya kuamua kung’ata jongoo na kuamua kuvunja urafiki uliopo na wasaidizi wake.
“Mimi sioni sababu kwa nini Rais asubiri sheria mpya, sheria iliyopo bado haijafanyiwa kazi— imelazwa usingizi. Ninachokiona hapa Rais ametangaza vita na marafiki zake, sasa ili ashinde vita hii, hana choice (hiari) zaidi ya kufumua Bazara lake la Mawaziri.“Suala la viongozi wetu kukiuka maadili ya uongozi limepigiwa kelele sana, huwezi kuwa wewe rais wa nchi, kisha ukafanya biashara Ikulu. Waziri wa Miundombinu ndiye anayesimamia usafiri wa anga, hapo hapo waziri huyo anashirikiana na waziri mwenzake kuanzisha shirika la ndege, kama si kutaka kuua ATC, ni nini?” Alihoji.
Profesa Baregu aliongeza: “Hawa viongozi ambao ni wafanyabiashara, wamekuwa wakijigamba kuwa rais ni wa kwao, wamemweka madarakani kwa fedha zao. Wananchi nao wanasema wao ndiyo waliomchagua rais kwa kura zao. Sasa Kikwete aamue kuwa Rais wa wafanyabiashara au Watanzania,” alisema.
Kwa upande wake, Dk. Sengondo Mvungi, msomi na mwanasheria, alisema: “Tatizo la nchi hii kuna kudharauliana, suala hili la watu kuchanganya biashara na uongozi, wapinzani wamelisema siku nyingi, lakini wamekuwa wakionekana malofa.“Mimi nafurahi Rais alivyosema kuwa suala hili wamekubaliana katika vikao vyao vya NEC, nasema hivi kwa sababu CCM ndiyo waliopuuza na kudharau maadili ya viongozi. Walipolitosa Azimio la Arusha baharini kule Zanzibar, walitupilia mbali na masharti ya maadili ya uongozi, kitu ambacho Mwalimu Nyerere alisikitika sana.
“Kama Rais kazinduka leo, tunamwambia Rais ana kazi ngumu, kama kweli ana dhamira ya dhati ya kurejesha maadili ya uongozi, afumbe macho, afute urafiki na watendaji.
“Suala la uongozi na biashara ni suala la mgongano wa maslahi, sheria ya sasa inakataza mgongano wa maslahi sasa suala la kusubiri sheria mpya halipo, unasubiri sheria ipi wakati iliyopo hujaitumia.
“Watu waliohusika na ufisadi wa BoT wanajijua wawajibike. Tatizo la mawaziri wa serikali hii, hawataki kujiuzulu wakamwachia Rais apumue. Hawataki kujiuzulu hadi wafukuzwe you have to kick their butts ndipo wajue kwamba hapa hatutakiwi,” alisema kwa sauti ya juu.Katika hatua nyingine, wananchi wameunga mkono wazo la Serikali kuanzisha mchakato utakaowazuia viongozi wa siasa kujihusisha na shughuli za kibiashara wakati wawapo kwenye utawala wa kuwatumikia wananchi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti Dar es Salaam jana, baadhi ya wananchi walisema uamuzi huo umechelewa na hauna budi kushughulikiwa na kutekelezwa mara moja
Mkazi wa Mwenge, Plasduce Kahaya, alisema hatua hiyo ni nzuri kwani itapunguza wanasiasa kuwa na tabia ya kujilimbikizia mali kama baadhi yao wanavyofanya sasa.
“Utakuta mwanasiasa anapokea mshahara na posho nyingi, na ni mfanyabiashara, kitendo kinachoziba nafasi za watu wengine,” alisema.
Mkazi mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Ester alisema hana imani kama sheria hiyo inaweza kupita endapo itapelekwa bungeni kutokana na wabunge wengi kuwa wafanyabiashara.
“Nahisi haitafika po pote maana wabunge karibu wote ni wafanyabiashara, sasa sidhani kama watakuwa tayari kujihukumu pale bungeni,” alisema Ester.
Naye, mwanasheria ambaye hakutaka jina lake litajwe, alisema hatua hiyo ni nzuri, kwani itatoa viongozi wa kweli, wawajibikaji na wenye nia ya kuwatumikia wananchi.
Akizungumza juzi katika hotuba yake ya kila mwisho wa mwezi, Rais Kikwete, alisema serikali inatarajia kuanzisha mchakato wa kufanya marekebisho ya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma ili viongozi wachague kufanya jambo moja, kati ya biashara, ubunge au uwaziri.
Kikwete alisema, upo ushahidi wa kuwapo kwa migongano ya masilahi kwa baadhi ya mawaziri au wabunge katika suala hilo. Alisema hata pale pasipokuwapo na dalili za wazi, hisia za kupata manufaa yanayotokana na nafasi zao, matokeo yake ni kupoteza imani na kutilia shaka uadilifu wa viongozi.
Mjini Dodoma, wabunge kadhaa wameipokea hotuba ya Rais Kikwete kwa hadhari.
Miongoni mwao ni Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Hamad Rashid Mohamed (CUF), ambaye pamoja na kuunga mkono, alishauri kuwapo kwa utafiti wa kina katika marekebisho hayo.
Akizungumza na MTANZANIA ofisini kwake bungeni mjini Dodoma jana, Rashid, ambaye ni Mbunge wa Wawi, alisema ni jambo zuri kwa Rais kutambua kuwa kiongozi wa kisiasa anayetumikia umma anatakiwa ashiriki kikamilifu kutimiza wajibu wake.
Alisema marekebisho hayo hayapaswi kuhusisha Sheria ya Maadili ya Viongozi pekee, bali hata sheria nyingine, akisisitiza kuwa marekebisho lazima yazingatie hatima ya kiongozi mhusika baada ya kustaafu, kwa kuwa uzoefu unabainisha kuwa viongozi wengi waadilifu huishia kuwa na hali duni kimaisha.
“Lazima kuwepo na tafsiri ya neno biashara katika marekebisho hayo kwa kuwa zamani katika miaka ya 1960 na 1970 kiongozi alikuwa hata akifuga kuku haruhusiwi, sasa tuelezwe ni biashara gani hizo?” Alihoji.
Mbunge huyo alisema sheria ya sasa si mbaya kama kungekuwapo na utashi wa kutosha wa kisiasa katika utekelezaji wake.
Akitoa mfano alisema yupo kiongozi aliyeingia madarakani akiwa hana kampuni wakati akitangaza mali zake, na akatoka katika uongozi akiwa anamiliki kampuni, tena bila kutoa maelezo ameipataje.Naye, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (CHADEMA), aliunga mkono moja kwa moja uamuzi wa Rais Kikwete.
“Najisikia furaha sana kumsikia Rais akisema hivyo. Binafsi Spika wa Bunge aliwahi kunituma Canada, katika Bunge lao upo utaratibu unaomtaka mbunge kutojihusisha na biashara. Niliporejea niliandika muswada binafsi ambao naruhusiwa- nikamkabidhi Katibu wa Bunge nikipendekeza sheria ya maadili ibadilishwe ili mawaziri wabunge waepuke kuingia katika mtego wa mgogoro wa maslahi, ilikuwa Machi 27, mwaka jana.
“Lakini Katibu wa Bunge alinijibu suala hilo haliwezi kushughulikiwa kwa sababu linahitaji mabadiliko ya Katiba. Lakini kwa sasa baada ya kumsikia Rais, wasiwasi wangu ni kwamba utekelezaji na hatimaye kukamilika kwa suala hili utachukua muda mrefu mno, mfano ni ahadi ya Rais bungeni Desemba 30, 2005, alipoahidi kufanyia kazi suala la udhibiti wa fedha za kampeni,” alisema.
Mbunge wa Busega, Dk. Raphael Chegeni (CCM), alisema hatua hiyo ya Rais kutaka marekebisho ya Sheria ya Maadili ya Viongozi ni muhimu, na akasisitiza kuwa ni lazima taifa lifike mahali liwe na viongozi wanaowajibika kwa wananchi.
“Chanzo cha sehemu kubwa ya ufisadi ni viongozi kutumia madaraka yao ya ki-uongozi kufanya maamuzi ambayo yanawanufaisha. Sasa marekebisho ni vizuri zaidi yakatazama kwa kina suala hili kwa ajili ya kudhibiti,” alisema.
Hata hivyo, alisema katika marekebisho hayo kazi ya ubunge ni lazima ikatambuliwa kuwa ni ‘kazi kamili’ yenye kipato kamili na kusisitiza kuwa mara kwa mara ubunge si kazi yenye mazingira ya kuwapo na mgongano wa maslahi.
Wakati huo huo, Marekani imempongeza Rais Jakaya Kikwete kwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU).
Akizungumza na MTANZANIA jana, Balozi wa Marekani hapa nchini, Mark Green, alisema Marekani imefurahishwa na uchaguzi huo, na ana imani katika uongozi wake kutakuwapo mabadiliko makubwa.
“Nina imani na Kikwete, ni mtu makini asiyeyumbishwa, na mwenye kufanya uamuzi wa busara, hivyo kuchaguliwa kwake kuwa Mwenyekiti wa AU kutasaidia kuleta maendeleo barani Afrika,” alisema Balozi Green na kuongeza:
“Kikwete ni mtu anayeheshimika ndani na nje ya Afrika, kwa kuwa anaheshimika inaweza kusaidia katika utatuzi wa migogoro inayoendelea ndani ya bara hili.”
Rais Kikwete alitangazwa kuwa mwenyekiti mpya wa AU juzi baada ya aliyekuwa mwenyekiti wa umoja huo, John Kufuor ambaye ni Rais wa Ghana, kumaliza muda wake.
Wakati Kikwete anaingia kwenye madaraka hayo ya kuliongoza bara la Afrika, anakabiliwa na changamoto mbalimbali yakiwamo machafuko ya kisiasa nchini Kenya na mapigano yanayoendeshwa na vikundi vya waasi katika nchi za Sudan, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC.
Mbali ya migogoro ya kisiasa, changamoto nyingine zinazomkabili Rais Kikwete ni kukuza uchumi na kupambana na magonjwa kama malaria, ukimwi, kifua kikuu na vifo vya watoto wachanga na wajawazito.
Ripoti hii imeandaliwa na waandishi Khamis Mkotya, Primtiva Pancras, Thomas William na Godfrey Dilunga.
No comments:
Post a Comment