Saturday, February 02, 2008


Ofisa Usalama wa Taifa

atumbukia ufisadi BoT


Waandishi Wetu, Dodoma


KAMPUNI mbili ambazo zimetumiwa kuchota mabilioni Benki Kuu (BoT) zimegundulika kuwa zinamilikiwa na Ofisa wa Idara ya Usalama wa Taifa mwenye cheo cha juu kabisa. Kampuni hizo ni Clayton Marketing Ltd na Excellent Services Ltd ambazo ni miongoni mwa kampuni 22 zilizotumiwa kuiba Sh bilioni 133 za BoT kupitia Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA).

Habari zimeeleza kuwa ofisa mmoja wa ngazi ya juu ndani ya idara hiyo ndiye anatajwa kama mmoja wa wakurugenzi. Habari za uhakika ambazo gazeti hili limezipata zinaeleza kuwa kampuni hizo zilitumiwa kuchota kiasi kikubwa cha fedha kwa kisingizio cha kazi maalumu ya kitaifa.

Kampuni ya Clayton inatajwa kuchota kwa wakati mmoja dola za Marekani 500,000 kutoka Benki Kuu. “Nyaraka tu iliandikwa kwenda Benki Kuu kwamba tafadhali lipa hizo pesa kwa kazi maalumu, unajua wakati huo hatukujua hizo fedha zinakwenda wapi, sasa tunafahamu,” kilidokeza chanzo kimoja cha habari.

Kampuni hizo mbili ni miongoni mwa kampuni zilizolipwa Sh bilioni 42.9 na hakuna nyaraka yoyote iliyowasilishwa kuthibitisha malipo hayo. Kampuni zingine katika kundi hilo ni G&T International Ltd, Mibale Farm, Liquidity Service Ltd, M/S Rashtas (T) Ltd, Kiloloma and Brothers, Karnel Ltd na Malegesi Law Chambers (Advocates) inayomilikiwa na Bedery Malegesi.

Pia gazeti hili limebaini kuwa ofisa huyo kutokana na nafasi yake, ni miongoni mwa watu ambao idara yake imehusishwa katika kuundwa kwa tume maalumu iliyoundwa na Rais Jakaya Kikwete kuchunguza tuhuma hizo. “Kwa kazi yake yeye ni mtu mkubwa katika kamati ile kwani ndiye anayeshughulikia masuala yote ya kigaidi, kiuhalifu wa kimataifa ndani ya Idara ya Usalama wa Taifa,” kilidokeza chanzo chetu cha habari.

Mwenyekiti wa kuchunguza ufisadi huo, John Mwanyika alipofuatwa na gazeti hili mjini Dodoma aeleze uhusiano wa Ofisa huyo wa Usalama wa Ikulu na kamati yake alisema kwamba hamfahamu huyo mtu na kamati yake inahusisha watu watatu na wala haihusishi watu wa Usalama wa Taifa.

“Sina taarifa za hizo kampuni unazoniuliza na wala huyo mtu simfahamu,” alisema Mwanyika wakati akizungumza na gazeti hili ambalo lilitaka ufafanuzi kama ofisa huyo anahusika kwenye kamati yake. Tume ya kuchunguza suala hilo inaongozwa na Mwanasheria Mkuu kwa kushirikiana na Mkuu wa Polisi na Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa.

Lakini vyanzo vya habari vilithibitisha kuwa Ofisi ya Usalama wa Taifa imeombwa kuhusishwa katika kuchunguza suala hilo kama ambavyo imekuwa inashiriki katika matukio mengine ya uhalifu. Kampuni ya Excellent Service Ltd ambayo imesajiliwa kama inashughulika na masuala ya upokeaji na usafirishaji wa mizigo, wakurugenzi wake wakati huo walimiki asilimia 100 kila mmoja akiwamo Ofisa Usalama huyo.

Kampuni hiyo ofisi zake zinaelezwa kuwa ziko Mtaa wa Sokoine kitalu namba 11649. Oktoba 5, 2004 mwenzake alijiuzulu na akateuliwa mtu anayeitwa Massimo Fanneli kuwa Mkurugenzi. Hisa za Sabbas ambazo ni 100 zilihamishiwa kwa Fannel baada ya kulipwa Sh milioni 5. Kampuni hiyo hadi kufikia Desemba 19 mtaji wake uliongezeka kutoka 500,000 hadi kufikia milioni 5.

Alipotakiwa kuzungumzia kama kampuni zilizoanzishwa na Ofisa Usalama huyo zilikuwa ni kwa ajili ya shughuli za Serikali, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Philip Marmo alisema jana kuwa Serikali haijafikia hatua ya kuanzisha kampuni katika idara yake nyeti ya kama ya Usalama wa Taifa.

Alisema kutokana na hali hiyo ni wazi kuwa kampuni anazodaiwa kuanzisha ofisa huyo mwandamizi zilizotajwa katika ubadhirifu wa Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA) hazihusiani na Idara ya Usalama wa Taifa.

"Mimi sifahamu kama ana kampuni lakini kwa mujibu wa Azimio la Zanzibar, anaruhusiwa kuwa na kampuni, lakini zisiingiliane na nafasi yake kwa maana asitumie nafasi yake katika uendeshaji wa kampuni zake. Sasa hivi suala hilo la kampuni zilizohusika na ubadhirifu linashughulikiwa na vyombo vya sheria, mimi siwezi ku comment kitu hapo, tusubiri sheria ifanye kazi," alisema.


No comments: