"Bora nife mapema kuliko kuiona Tanzania hiyo, - Mbunge Simbachawene" |
Na Waandishi Wetu, Dodoma
MLOLONGO wa mambo unaendelea kumzonga Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi baada ya jana kupigwa rungu na Wabunge.
Rungu hilo lilikuja baada ya semina ya Wabunge kuhusu muswada wa Sheria za Umeme na Biashara ya Mafuta jana kuvunjika baada ya wawakilishi hao wa wananchi kukataa hoja ya Waziri Karamagi na kushinikiza kikao hicho kifungwe kwa maelezo kuwa hakina maslahi ya Taifa.
Wabunge hao walisema hawataki kujadili muswada huo hadi watakapopata ripoti kamili ya uchunguzi kuhusu Kampuni ya Richmond na kujadili kwa maelezo kuwa 'kuna mkono wa mtu' katika Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), hivyo kulifanya lifikie hatua mbaya ya kuwabebesha wananchi mzigo wa kulipa madeni kupitia bili kubwa za umeme.
Katika hali isiyokuwa ya kawaida wabunge hao bila kujali itikadi za vyama,walimkataza Karamagi na Naibu wake, William Ngeleja, kujibu lolote kuhusu mchango wao na kumtaka Mwenyekiti wa kikao hicho, Dk. Harrison Mwakyembe kufunga kikao kabla hali haijawa tete zaidi.
“Naomba tusiletewe muswada huu, wananchi watatuchinja, Mwenyekiti funga semina yako, wizara hii imepoteza sifa ya kuzungumza na wananchi," alisema Mbunge wa Vunjo, Aloyce Kimaro (CCM) na kuongeza:
"Bei ya umeme imepanda kutokana na gharama za IPTL, Net Group Solution iliyoingizwa na FFU kutumalizia TANESCO, baadaye ikaletwa Richmond tukiwepo," alisema Kimaro huku akionesha hali ya masikitiko.
Mbunge wa Hai, Fuya Kimbita (CCM), alisema: “Busara hainunuliwi, mtu unapewa na Mungu, upepo umeusoma, hali ya hewa inaeleweka, tumia busara na hekima” akimaanisha kumtaka Mwenyekiti kufunga kikao hicho kwa kuwa hawataki mjadala huo kwa sasa.
Mbunge wa Musoma mjini,Vedastus Manyinyi (CCM) alimshauri Karamagi asome hisia za Wabunge badala ya kupoteza muda.
"Waziri semina umeiona, huhitaji kufundishwa, tunahitaji Ripoti ya Richmond kwanza, kuna mambo tunataka kuyaangalia baada ya kusoma ripoti hiyo," alisema Manyinyi.
Kwa upande wa Mbunge wa Kibakwe, George Simbachawene (CCM), alitoa somo la aina yake baada ya kutoa maoni yake kwa maandishi kwa maelezo kuwa kutokana na uchungu alio nao hawezi kuzungumza akaeleweka.
"Nimeandika waraka huo kwa hisia kali, siwezi kurudia maneno niliyoyaandika kwa mdomo, naomba isomwe kwa Wabunge kama ilivyo," alisema Simbachawene na kumwomba Dk. Mwakyembe asome waraka wake kwa Wabunge.
Akisoma waraka huo, Dk. Mwakyembe alisema: " Nikipiga picha ya Tanzania inayokuja nasikitika, nachanganyikiwa, nawahurumia Watanzania, tunauza kila kitu kuanzia viwanda, vinu vya kuzalishia umeme kwa watu wengine, watakaogonganisha glasi huku serikali ikibakia kuwa House Girl (mfanyakazi wa kike wa ndani) na House Boy (Mfanyakazi wa kiume wa ndani) wa wamiliki hao.
"Bora nife mapema kuliko kuiona Tanzania hiyo," ilisema sehemu ya waraka huo wa Simbachawene ambaye aliinamisha kichwa chini wakati iliposomwa kuonesha uchungu na masikitiko yake.
Naye Mbunge wa Same Mashariki Bibi. Anne Malecela (CCM), alitoa angalizo kwa Dkt. Mwakyembe na kueleza kuwa kama wabunge watarudia kosa tena watakuwa wajinga hivyo watapoteza sifa ya kuwa wawakilishi wa wananchi.
"Ukiona mtu anaitwa Mbunge ujue ana akili nzuri kwa kuwa hiyo ni sifa ya kwanza ya Mbunge, kwa mara ya kwanza nakushangaa ndugu Mwenyekiti, tujifunze kukosea mara moja, tukikosea mara ya pili tutakuwa 'stupid' (wajinga), Mbunge hatakiwi kuwa 'stupid',” alionya Anne.
"Tumeambiwa TANESCO ipo ICU (chumba cha wagonjwa wenye
uangalizi maalumu), nani kaipeleka huko? “Huenda kuna mkono wa mtu, sisi tunataka kushughulika na huo mkono, kama Mbunge na kama Mama, nasema hata mkituweka katika semina hii kwa siku nne, hatutaujadili mswada huu !" alisisitiza Mbunge huyo.
Sakata hili limekuja baada ya kuwepo mjadala mzito bungeni ambapo Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe alitoa hoja binafsi juu ya mkataba wa madini kusainiwa nje ya nchi.
Mjadala huo ulifikia hatma kwa Zitto kusimamishwa katika kikao cha Bunge kilichopita, lakini jina la Karamagi likaendelea kuvuma vibaya mitaani.
No comments:
Post a Comment