Tuesday, February 05, 2008


Wabunge Afrika Mashariki

kufunzwa Kiswahili


Faraja Mgwabati


BUNGE la Afrika Mashariki (EALA) lipo katika mchakato wa kuanzisha Tume ya Kiswahili (KC) ambayo itaratibu masuala yote yanayohusu lugha hiyo ikiwa pamoja na kuhamasisha matumizi yake katika Bara la Afrika.

Sambamba na hilo, Bunge hilo sasa limeamua wabunge wake wote ambao hawazungumzi Kiswahili, kwenda shule kujifunza lugha hiyo kwa sababu ni muhimu kwa mawasiliano ya Bunge hilo.

Mbunge wa EALA kutoka Kenya, Safina Tsungu, aliliambia HabariLeo jijini Dar es Salam jana kuwa hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu, tayari muundo wa Tume hiyo utakuwa umekamilika tayari kwa kuanza kazi.

“Kiswahili ndiyo lugha ya Afrika hivi sasa kwa hiyo hatuna budi kuiimarisha na kuieneza kama zilivyo nyingine za kimataifa,” alisema Tsungu na kuongeza kuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki imedhamiria kukifanya Kiswahili lugha kuu barani Afrika.

Tsungu ambaye yupo katika kamati ya Kilimo, Utalii na Maliasili ya Bunge hilo alikuwa akizungumza katika semina ya wabunge wa kamati hiyo inayofanyika Dar es Salaam. Alisema tayari Zanzibar imeomba kuwa makao makuu ya Tume hiyo ya Kiswahili.

“Hii ni sehemu ya utaratibu uliopo ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, kila nchi inaweza kuomba kuwa mwenyeji wa taasisi, mfano tume ya Ziwa Victoria ipo Kisumu, Kenya,” alisema Tsungu.

Mbunge huyo alibainisha kuwa kutokana na umuhimu wa lugha hiyo katika mawasiliano ya wananchi wa Afrika Mashariki, Bunge hilo limekubaliana wabunge wote ambao hawazungumzi Kiswahili, kwenda Zanzibar kwa ajili ya kujifunza.

“Kila Mbunge lazima ajifunze Kiswahili na tunataka hadi kufikia Juni mwaka huu wabunge waende chuoni Zanzibar kujifunza Kiswahili ili kuonyesha mfano pia kwa wananchi wao na kurahisisha mawasiliano yao,” alisema.

Wakati huo huo Mwenyekiti Kamati ya Kilimo, Utalii na Maliasili, Dk. George Nangale amesema hali ya kisiasa nchini Kenya imeathiri kwa kiasi kikubwa sekta ya utalii nchini humo na nchi nyingine za Afrika Mashariki.

No comments: