WIKI ya 6, nilikuwa mkoani Tanga safari yangu ambayo ilinifikisha katika Mtaa wa Nairobi kijijini Kicheba, wilayani Muheza.
Kule nilikutana na baadhi ya wazee ambao koo zao zamani zilikuwa za viongozi wa kijadi, maarufu kama Zumbe.
Lakini, kabla ya kupata taarifa za hapa na pale, mtoto mmoja aliacha watu wakiangua kicheko baada ya kushtuka kwa kusikia mzee mmoja akiambiwa 'Mwinyi', yeye ghafla akasema huyo si 'Mwinyi' ni babu!
Kwa kumsaidia msomaji, neno Mwinyi hutajwa katika sehemu ya salamu za Wabondei, mfano Tate au Mmaa Mwinyi (Baba au Mama Mwinyi), ikimaanisha salama ambayo inatokana na athari ya mfumo wa Kikoloni wa Umwinyi uliotumiwa na Waarabu katika mwambao wa Pwani.
Mtoto huyu alifikiri babu yake ameitwa Mwinyi kama jina la mzee ruksa, Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Alli Hassan Mwinyi, kumbe ni salamu tu ambayo mzee anayeamkiwa huitikia: "Mwinyi Said...!
Wazee wakacheka kidogo, mtoto huyo naye akaenda kucheza, habari za hapa na pale zikaanza, ambazo kwa sehemu kubwa wazee hawa wakahoji taarifa mbalimbali wanazosikia ndani ya serikali na kuanza kukumbushia umuhimu wa vizazi na watu kutosahau historia.
Msisitizo wa umuhimu wa kutosahau historia ukawa mkubwa hadi nikashangaa, kumbe msingi wao umejengeka katika kuangalia mambo muhimu yanayotokea sasa katika nchi.
Kwa kuonyesha msingi huo, wazee wakaanza kuhoji matukio na taarifa ufisadi nchini, miongoni ambayo yameonekana kugusa nyoyo za wazee hawa ni pamoja na sakata la ufisadi katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na mkataba wa kifisadi wa Richmond.
Wakati nikiendelea kuwasikiliza wazee, kubwa nilililojifunza ni kwamba, watu hata wa vijijini wanajua nchi yao inakwenda vipi licha ya uhaba wa mawasiliano ikiwemo upatikanaji wa vyombo vya habari.
Katika kujadili hayo, wazee wakakumbusha historia kidogo kwamba wakati wa Serikali ya Awamu ya Kwanza chini ya Baba wa Taifa hayati Mwalimu Julius Nyerere, hata kama kulikuwa na rushwa lakini watu walikuwa wakiogopa na kuwajibika pale walipokuwa wanabainika.
Msingi wa mazungumzo ya wazee ukazidi kupanuka, mwisho wakatoa kile ambacho walikuwa wakificha kwamba, vipi historia ilimsahau Edward Lowassa, hadi akaja kupewa Uwaziri Mkuu nafasi ambayo ni nyeti katika nchi kama walijua matokeo ya ripoti ya Kamati ya Bunge.
Wazee waliamini historia haiwezi kumwondoa Lowassa kama mtu ambaye hafai kutokana na Mwalimu Nyerere, kumkataa katika kinyang'iro cha Urais mwaka 1995.
Hili la umuhimu wa kuangalia historia, ndilo jambo kuu ambalo nitajaribu kulijengea hoja juu yake.
Kimsingi, kama hujui historia ni dhahiri huwezi kujua wewe ni nani na ulitoka wapi na unaelekea wapi.
Ndiyo maana, awali kabisa nikajaribu kutoa mfano wa mtoto yule wa darasa la nne, ambaye alishtuka kusikia babu yake anaamkiwa 'Mwinyi'.
Hii ni historia, kwa kawaida somo hili lina athari na faida kutegemeana na mahitaji ya jamii kwa wakati husika.
Mfano, mila na desturi ni sehemu ya historia, ndiyo maana kuna mila kama za kurithi wajane hazikubaliki kwa wakati huu kutokana na uwezekano wa kuambukizana maradhi ya ukimwi na vuguvugu la wanaharakati wa kijinsia kulitaja kama la unyanyasaji wa mwanamke.
Historia pia ni muhimu katika suala la uongozi katika jamii na nchi kwa ujumla, kuangalia nani anapaswa kupewa nafasi ipi kwa kuangalia alikotoka na historia ya uadilifu wake.
Jambo hili la historia ya mtu anayepewa nafasi ya uongozi katika nchi ambayo inaangalia wasifu wake ikiwemo uadilifu, ndiyo kubwa ambalo Mwalimu Nyerere aliwahi kuhoji wakati Lowassa anataka kugombea nafasi ya Urais mwaka 1995.
Hili la Mwalimu kuhoji, limeangalia jambo la msingi ambalo hakutaka kuwa mnafiki bali ni kutaka maelezo ya mali ambazo Lowassa alikuwa nazo wakati ule.
Msimamo huu wa Mwalimu Nyerere mtu ambaye naamini kabisa kama mmoja wa kielelezo cha uzalendo na utaifa wa nchi hii, mara nyingi katika uhai wake na uongozi katika chama na serikali, hakuwa akikosea punde anapomtilia shaka mtu anayetaka uongozi.
Hili la Mwalimu Nyerere na kutopitishwa kwa Lowassa na chama chake mwaka 1995 kugombea urais, ni historia ambayo Rais Jakaya Kikwete, bila kujali urafiki wao alipaswa kuitambua na kumtosa Lowassa kwa kutothubutu kumpa nafasi ya Waziri Mkuu.
Bahati mbaya, Rais Kikwete hakutaka kumhukumu Lowassa kwa historia bali akatumia ubinadamu akampa nafasi, labda akifikiri ni mtu aliyekuwa kaonewa na akina Mwalimu Nyerere!
Rais Kikwete akasahau kwamba, Mwalimu Nyerere alikuwa ni mtu mwenye kuona mbali na aliyepewa kipawa tofauti na binadamu wengine badala yake akaleta Uwana-Mtandao akampa Lowassa nafasi nyeti katika nchi. Sasa amemwangusha vibaya.
Lakini kauli ya Mwalimu Nyerere na utabiri wake umetimia, baada ya matokeo ya Kamati Teule ya Bunge kummwaga Lowassa kwamba akiwa Waziri Mkuu alitumia madaraka yake kulitia taifa hasara kwa mkataba wa Sh172 bilioni kati ya Shirika la Umeme (Tanesco) na kampuni hiyo ya mfukoni, Richmond!
Hapa ikathibitika kwamba huyu hakuwa akifaa, ndiyo maana wazee ambao wanajua maana ya uadilifu katika nchi walimkataa.
Rais Kikwete hana upeo kama marehemu Mwalimu Nyerere, hivyo nadiriki kusema alitumia vibaya madaraka yake kumpa mtu nafasi ambaye alishindwa kueleza alikopata utajiri wake mwaka 1995.
Katika nchi kama Tanzania ambayo imetoka katika mfumo wa ujamaa akatokea mtu mwenye utajiri asioweza kuulezea hafai kuongoza, ni lazima atahujumu uchumi wa nchi.
Ndiyo maana naamini kabisa, kama imani za marehemu zinafanya kazi, basi Mwalimu Nyerere hakuwa na radhi na serikali ya Rais Kikwete chini ya Waziri Mkuu Lowassa.
Hii ni dhambi ya watu kupewa nafasi nyeti katika nchi bila kuangalia historia ambayo ingeonyesha uadilifu wao ukoje, haiwezekani nchi maskini yenye matatizo mengi ya kijamii mtu uhujumu uchumi kwa kuingiza nchi kwa mkataba wa Sh172 bilioni.
Nchi haiendeshwi kitapeli au kwa amri za mtu kutumia wadhifa wake, kama ingekuwa ni hivi familia ya Mwalimu Nyerere ingekuwa na utajiri wa kupindukia.
Madaraka ya umma hayawezi kutumiwa kufanyia utapeli na kuhujumu uchumi wa nchi, kama ilivyotumiwa nafasi ya Waziri Mkuu katika mkataba wa Richmond kwa kuipa kampuni ya mfukoni kazi ya kufua umeme, huku ikiwa haina ofisi, utaalamu hata wa kuchomeka balbu .
Kibaya zaidi Waziri Naziri Karamagi ambaye ni mmoja wa watuhumiwa wa ufisadi mimi namwiita mtuhumiwa wa uhujumu uchumi, anadiriki kusema lazima Tanesco ipandishe gharama za umeme kutoka za sasa asilimia 21 hadi 61, huku ni kuua Watanzania kwa makusudi.
Hivi kweli mzigo huu wa Sh152 milioni za kila siku zinazolipwa Richmond, ndugu zangu Watanzania, hebu tujadiliane tuwafanyeje hawa waliotia taifa hasara? maana kujiuzulu haitoshi.
Huku ni kuhujumu uchumi, sawa Lowassa amejiuzulu, kinachofuata tunataka pesa zetu na kuhakikisha wote walio nyuma ya kiongozi huyu ambao katika nafasi zao walishiriki kuhujumu uchumi wanafikishwa katika vyombo vya sheria.
Tunataka kuandika historia mpya katika nchi yetu, tunataka kujenga taifa lenye watu ambao wana hofu ya kutumia madaraka ya umma katika kuhujumu uchumi.
Nchi lazima ijengeke katika msingi na amri kumi za Tanganyika African National Union (TANU) ambazo, miongoni mwao ni kuapa kutokutoa wala kupokea rushwa na kutumia vibaya madaraka au cheo vibaya kwa kuwa cheo ni dhamana.
Maadili ya uongozi yameporomoka, watu badala ya kuandika historia za uadilifu kama marehemu Mwalimu Nyerere na mwanamapinduzi mwingine Edward Moringe Sokoine, wao wanaacha historia ya ufisadi.
Viongozi hawa wasio waadilifu na mafisadi ndiyo ambao huchochea machafuko katika nchi, watu wanasahau kulinda maslahi ya taifa, kwanini wananchi wasitumie hata nguvu ya umma kuwang'oa?
Historia imejirudia kwa mlango wa nyuma, Lowassa kang'oka kwa tuhuma za ufisadi, kauli ya Mwalimu Nyerere na utabiri wake imetimia, lala salama Mwalimu Nyerere Lowasa kashang'oka!
No comments:
Post a Comment