MWANZONI mwa wiki hii Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limeandika historia mpya baada ya aliyekuwa waziri mkuu, Edward Lowassa, kujiuzulu kutokana na kashfa ya ufisadi.
Kujiuzulu kwa Lowassa, kiongozi wa ngazi ya juu kitaifa, kulitokana na taarifa ya Kamati Teule iliyongozwa na Mwenyekiti wake, Dk. Harrison Mwakyembe, iliyobani kiongozi huyo kuhusika kwa namna moja au nyingine katika kashfa hiyo.
Kuondoka kwa Lowassa madarakani kulipokelewa kwa shangwe katika sehemu mbalimbali za Tanzania.
Wananchi wengi hivi sasa wamekuwa na mawazo tofauti juu ya viongozi wakuu wa serikali kuhusu utendaji kazi wao pamoja na mamlaka zinazohusika, kwa kile wanachosema “viongozi hao wameshindwa kulitumikia taifa na badala yake wamekuwa wakijinufaisha tu.
Lakini mbali na viongozi hao, wananchi nao wanaonekana kukerwa zaidi na Taasisi ya Kuzia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), inayoonekana kupoteza mwelekeo wa majukumu iliyokabidhiwa na serikali.
Nasema hivyo kwa sababu kitendo kilichofanywa na taasisi hiyo cha kukumbatia ufisadi kiasi cha kumsafisha Lowassa mbele ya macho ya Watanzania, kimewaondolea imani kwa wananchi.
Ni wazi kwamba TAKUKURU haikuanza leo wala jana kuwakumbatia viongozi mafisadi hapa nchini, kelele nyingi zimepigwa hasa wakati wa Serikali ya Awamu ya Tatu chini ya Rais mstaafu Benjamin Mkapa.
Awamu hiyo ililamikiwa sana kwa baadhi ya viongozi kuwa wamejilimbikizia mamilioni ya shilingi, majumba (mahekalu) na magari ya kifahari, lakini TAKUKURU yenye dhamana ya kuchunguza mambo kama hayo, iliishia kunawa mikono tu.
TAKUKURU, inayolipwa fedha za wakulima, wavuja jasho na walalahoi wa nchi hii, imefikia hatua sasa ya kugeuzwa taasisi ya kulinda wakubwa na si kuzuia na kupambana na rushwa kama ilivyoainishwa wakati taasisi hii inaanzishwa.
Kitendo cha TAKUKURU kuisafisha Kampuni ya Richmond Development Company LLC na Edward Lowassa ni ushahidi tosha kwamba na wao wanahusika kwa namna moja au nyingine kwenye sakata hiyo.
Bila aibu yoyote machoni mwake, Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo, Edward Hosea, aliuhakikishia umma wa Watanzania milioni 35 kuwa Richmond na Lowassa wako safi.
Nakumbuka siku hiyo, Hosea alipotoa taarifa hiyo mbele ya waandishi wa habari, alisisitiza kwa nguvu zote kwamba LLC na Lowassa hawakuhusika kwa yoyote katika sakata zima la kutafuta zabuni ya kuzalisha umeme.
Lakini nakumbuka aliyekuwa mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Yusuf Makamba, aliwahi kusema mtu mzima akiongopa huwa hakubali bali hubaki anagunaguna tu.
Hii inatosha kuonyesha wazi kwamba Hosea, bila aibu, amebaki anagunaguna na kushindwa kuwaomba radhi Watanzania kwa kauli yake isiyo na ukweli. Kauli ya aina hiyo sasa imelisababishia taifa hili hasara ya mamilioni ambayo yangeweza kujenga shule, zahanati na hata kupeleka huduma ya maji kwa wananchi walioko vijijini ili kuepukana na matatizo yanayowakabili.
Kitendo hiki cha Hosea kimesababisha TAKUKURU iendeleze jambo lake lile lile la kukosa imani kwa wananchi - sijui ni lini wananchi watakuwa na imani kwa chombo hiki.
Nakumbuka vizuri wakati anaingia madarakan baada ya kuapishwa pale Ikulu, Dar es Salaam, na Rais Kikwete, Hosea aliwaambia waandishi wa habari kwamba wakati umefika sasa wa kushughulikia mapapa wakubwa na si dagaa.
Lakini kadiri siku zilivyozidi kwenda na Hosea kufuatwa mara kadhaa na waandishi, hasa baada ya muda aliokuwa ameuweka yaani baada ya Krismasi kuonekana kupita - aliposema kwamba rungu lake litaanza kuwashukia mafisadi, alianza kuwapiga chenga waandishi.
Krismasi kilikuja, kikapita kama mvua ya upepo, Hosea akaendelea kuwa kimya, hali kwa namna moja au nyingine iliyoonyesha alikuwa akipanga mikakati ya kuisafisha Richmond na watu wake wote akiwamo Lowassa.
Kauli hii ilitutia moyo sana na kuamini kwamba sasa chombo hiki muhimu kimepata mtu makini atakayeshughulikia mabwana wakubwa ambao wamekuwa sugu kwa utafunaji wa fedha za walipa kodi hapa nchini.
Ili kudhihirisha imani kwa wananchi, Hosea anapaswa kuwaomba radhi Watanzania kabla ya kuachia ngazi kutokana na kashfa hii ambayo, kwa mtu mzima na mwenye akili timamu, haiingi akilini mwake.
Napenda kuona kwamba Hosea asiondoke mwenye kwenye ofisi hizi, ajumuishwe na wasaidizi wake wote na washauri waliotumia muda mwingi kuwapatia Watanzania habari za uongo juu ya ripoti yao ya uchunguzi wa Richmond.
Haiingi akilini kwa mtu wenye akili timamu kwamba mikataba mibovu kama ile ya Kampuni ya Meremeta, Buzwagi na ufisadi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inaibuliwa na viongozi wa vyama vya upinzani, kwani TAKUKURU imelala usingizi wa namna gani huo?
Vichekesho vya TAKUKURU ni kwamba kila kunavyokucha itasikika kupitia vyombo vya habari imewakamata mahakimu wa Mahakama za Mwanzo au makarani tu, kwa nini hata siku moja isimkamate waziri, mkurugenzi wa manispaa, mkuu wa wilaya au wakurugenzi wa makampuni makubwa? Umefika wakati TAKUKURU kuwa mzigo usiobebeka.
Hata mzigo usiobebeka unaweza kusukumwa na ukatembea wenyewe lakini si taasisi iliyopewa dhamana na wananchi kushughulikia matatizo yao. Umefika wakati na viongozi wake wote wafanyiwe uchunguzi wa mali zao ili kubaini namna walivyozipata.
Naamini wapo vigogo ndani ya taasisi hii wanaomiliki majumba makubwa, magari ya kifahari na kusomesha watoto wao nje ya nchi kwa fedha za walipa kodi wa nchi hii.
Kitendo hiki cha TAKUKURU kinaonyesha wazi jinsi ilivyo hapo kwa manufaa yake binafsi na si Watanzania kama walivyotumwa, leo hii watatwambia nini au hadi wananchi waitishe maandamano ya kuikataa, hapa nisingependa kuona inatokea hali kama hii, lakini jisafisheni haraka.
Namalizia kwa kusema kwamba TAKUKURU someni alama za nyakati, Hosea kabidhi ofisi ili wengine nao wajaribu kuendesha chombo hiki kilichopoteza imani kwa wananchi kwa vile umevuna ulichopanda.
Simu: 0756 511845Barua pepe: karedia2005@yahoo.co.uk
Kutoka Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment