Kenya ya leo hivi,
ya kesho itakuwaje?
na Abdul Mohammed
MATUKIO ya mauaji, ubakaji, uporaji mali na kila aina ya vurugu, zinazotawala nchini Kenya kwa sasa, zinanifanya nikumbuke mwaka 2005.
Mwaka huo wa 2005, nilikuwa nikiishi Kenya, katika mji wa Kisumu, nikifanya kazi na taasisi moja binafsi, ya Vigiha Community Development Organisation (VCDO).
Kwa kuwa taasisi hiyo haikuwa na shughuli nyingi za kila siku, nikiwa katika mji huo, nilikuwa nafanya kazi katika magazeti ya Nation, katika ofisi zake za Kisumu.
Nilikuwa nikifurahia hali ya mji mdogo wa Kisumu, ulioko karibu kabisa na Ziwa Victoria, na ambao ni ngome kuu ya kiongozi wa upinzani, Raila Odinga.
Naukumbuka mji wa Kisumu ambao pia unajulikana kwa jina la Lake Side City (yaani mji ulio pembezoni mwa Ziwa), kwa namna ulivyokuwa umetulia, ukiwa hauna aina yoyote ya ghasia wala vurugu nyingi, kama ilivyo katika mji wa Nairobi, ambako habari na hisia za hofu ya wizi na vurugu nyingine, zilikuwa zikituogopesha wageni kama sisi.
Nikiendelea kuukumbuka mwaka 2005, kumbukumbu zangu nyingi bado ziko nchini Kenya, na hususan katika mji wa Kisumu.
Naikumbuka hoteli ya Kimwa, hoteli maarufu kwa wageni watumiao mabasi ya Akamba, wanaoelekea Uganda. Hiyo ilikuwa ni sehemu ya kukutana na Watanzania wenzangu, hususan wanafunzi wanaokwenda masomoni Uganda, na hata wafanyabiashara.
Kiswahili chao wakati wa kuagiza chakula, kilitosha kunifanya nibaini kwamba hawa ni Watanzania. Utawasikia wakisema: “Naomba kuku na chipsi.” Huna sababu ya kuhoji. Unajua huyo ni Mtanzania, kwa kuwa kama angekuwa Mkenya, ungemsikia akisema: “Nipe kuku na chipsi”, na kama ni Mganda, basi ungemsikia akizungumza Kiingereza.
Kimwa ni hoteli ambayo nilikuwa nimezoea kunywa kahawa, kiasi cha wahudumu wa hoteli hiyo kunizoea, na mara nyingi walikuwa wakisema: “Yule Mtz anayependa kahawa,” kila wanapotaka kunitambulisha kwa wengine.
Nakumbuka, maduka makubwa maarufu kama ‘Super Markets’ ya maeneo ya Ukwala na Nakumatt, ambayo yalikuwa yakiupendezesha mji mdogo huo wa Kisumu, na wakati mwingine nilikuwa nikiingia kwa ajili ya manunuzi.
Nikiendelea kuikumbuka Kisumu, napakumbuka Mon-Amii, sehemu ambayo tulikuwa tukikutana kwa ajili ya kuangalia mechi za soka, hususan Ligi Kuu ya England.
Naikumbuka Mon-Amii, kwa mambo mengi, kwa kuwa mbali na kuwa klabu maarufu ya usiku, kina dada nao hujazana mahali hapo kwa ajili ya biashara zao. Nawakumbuka kina dada hao, wataagiza soda na kusogea karibu na alipo mwanamume, na wakati mwingine, akitoka nje tu, watamsalimia na kumkonyeza na kadhalika.
Naikumbuka pia hoteli ya Kimwa Annex iliyopo maeneo ya Manyatta. Nakumbuka marafiki zangu walivyokuwa wakinichukua kwa ajili ya burudani ya muziki wa Ohangla, dansi maarufu la Wajaluo.
Namkumbuka Tony Nyadundo, msanii ambaye alikuwa maarufu kwa ngoma ya Ohangla, na namna alivyojizolea umaarufu katika mji wa Kisumu na nyimbo zake kusikika kila kona, na hata ndani ya mabasi ya daladala, ambayo wenyewe wanayaita matatu.
Nakumbuka nilivyoweza kupata marafiki wa makabila mbalimbali, ingawa Wajaluo ni wengi Kisumu, wako watu wa makabila mengine ambao nilizoeana nao.
Nilikuwa na marafiki wa makabila ya nje ya Kisumu, kama vile Waluhya, Wakisii, Wakikuyu na hata Wasomali, ambao hawakusita kunialika kula nao futari katika mwezi wa Ramadhan, na kunichukulia kama mwenzao.
Nikiwa Kisumu, nilijiona kama niko nyumbani. Nilikuwa nakwenda kucheza mpira na Wajaluo ambao mazungumzo yao uwanjani, yalikuwa ni Kijaluo kitupu, huku Kiswahili kikizungumzwa mara chache, lakini mpira ulitosha kuniongezea marafiki.
Haikuchukua muda, nilijiona kama mwenyeji, kwa kuwa mitaani, nilikuwa nasalimiwa mara kwa mara na watu ambao nilikuwa nacheza nao mpira.
Nawakumbuka Wasomali ambao niliwahi kucheza nao mpira, lakini pia naikumbuka timu ya Victoria FC, ambayo pia nilikuwa nakwenda kufanya nao mazoezi pale kwenye Uwanja wa Railway. Nakumbuka nilivyojionea utamaduni mpya katika timu hiyo.
Kila baada ya mazoezi, tulijikusanya pamoja na kufanya maombi tukiwa tumeshikamana. Maombi hayo yaliyokuwa yakiendeshwa kwa lugha ya Kiingereza, yalilenga kumshukuru Mwenyzi Mungu, kwa kumaliza mazoezi salama bila hata mmoja wetu kuumia.
Aidha, maombi hayo yalilenga kumuomba Mungu atuwezeshe kufika nyumbani salama na pia kufanya mazoezi salama siku inayofuata.
Ingawa yalikuwa maombi yenye mtazamo wa dini ya Kikristo, nami nikiwa Muislamu, bado nadiriki kusema kwamba yalinivutia, na nikiri hapa nilifarijika wakati wote kwa namna tulivyoonyesha kumnyenyekea Mungu.
Nakumbuka pia marafiki ambao mara zote walinifanya nikae kijiweni na kuzungumza nao hadi usiku nikiwa Kisumu, na hasa maeneo ya Railway, na kurudi nyumbani kwangu eneo la Milimani saa tatu, na wakati mwingine saa nne usiku, bila hofu.
Nilipapenda sana Kisumu. Hata siku zangu za mwisho za kutaka kuondoka zilipowadia, nilipowaambia marafiki zangu kuhusu Kisumu, waliniambia Kisumu ni rahisi kuingia, lakini kutoka tabu. Kwa hiyo, kama unaondoka, bila shaka kuna siku utarudi au unaweza usiondoke kabisa.
Nikiwa Tanzania, kwa sasa nasoma habari za kusikitisha nchini Kenya, na hasa za wanawake kubakwa, raia wasio na hatia kuuwa, nyumba na maduka kuchomwa, hali ambayo inanifanya niwasiliane na wenzangu kujua hali ikoje huko kwao.
Naanza kuambiwa kwamba hoteli ya Kimwa, niliyokuwa nimezoea kunywa kahawa, imechomwa moto, na kwamba ipo katika hali mbaya. Nikiuliza sababu, naambiwa mmiliki ni Mkikuyu.
Naambiwa Kimwa Annex, mahali palipokuwa na ukumbi wa muziki, nilipowahi kupelekwa kwa ajili ya Ohangla, nako hakufai hata kidogo, hoteli imechomwa moto. Nauliza sababu, naambiwa mmiliki ni Mkikuyu!
Naambiwa zaidi kwamba ile Super Market ya Ukwala, kwa sasa haitamaniki. Imevunjwa na watu kuingia ndani na kuondoka na bidhaa walizoweza kuzibeba.
Pale Mon-Amii, naambiwa kwa sasa hapakaliki, na hata zile shamrashamra za usiku, zimepungua na siku nyingine hazipo, watu wametawaliwa na hofu.
Mji wa Kisumu naambiwa umekuwa si ule wa 2005 niliouzoea, bali umekuwa tofauti kabisa na ile hali ya urafiki na undugu niliyoizoea haipo tena, hofu imetawala.
Wale marafiki Wakikuyu niliokuwa nao Kisumu, nakumbuka mmoja nilipenda kumtania kwa kumwambia ‘A Kikuyu in the Luo land’ (Mkikuyu katika ardhi ya Wajaluo), leo hii nikiwauliza vipi, wananiambia wamekimbia Kisumu. Kisa, Wajaluo hawawataki na wao wana hofu ya kuuwawa.
Katika kuishi kwangu Kisumu na Kenya kwa ujumla, nilitambua kuwapo kwa tatizo la ukabila, lakini niliona kama ni jambo la kawaida na si kubwa kama nilivyosikia na hali ilivyo kwa sasa.
Niliona baadhi ya watu wakisakama makabila mengine lakini si katika hali ambayo ingeweza kuzaa balaa na kuna wakati mwingine nilifurahi kuona kama ukabila ilikuwa ni sehemu ya kufanyiana dhihaka za kawaida.
Kwa mfano nakumbuka Wakikuyu walikuwa wakihusishwa na tabia ya kupenda sana fedha na hiyo ikanikumbusha namna Wachaga wanavyotaniwa hapa Tanzania.
Nilizoea sana kuwasikia Wajaluo wakizungumza lugha yao na mara chache sana Wakikuyu, nakumbuka mara yangu ya kwanza kumsikia Mkikuyu akizungumza kwenye simu nilibaki nashangaa nikamwambia nini hicho unaongea.
Nilimtania kwa kumwambia kwamba lugha yao ni ya ajabu na haifai kuzungumzwa kwenye simu, nilimwambia wanavyoongea ni kama vitu vinagonganagongana, mwenyewe alicheka akaniambia umezoea sana Kijaluo.
Leo hii Kenya nasikia kabila limekuwa ni jambo kubwa na mwanzo wa balaa kiasi cha kufikia hatua ya watu kuuana, watu kuhama makazi yao na kuwa wakimbizi ndani ya nchi yao.
Ukabila imekuwa chanzo cha wasichana kubakwa na wengine kuzikwa wakiwa hai.
Ukabila umehusishwa moja kwa moja na matokeo ya uchaguzi wa Desemba 27 mwaka jana, ambao aliyetajwa kuwa mshindi, Mwai Kibaki inaaminika kwamba hakushinda kihalali.
Badala yake wafuasi wa mshindi anayeaminika kuwa ndiye aliyeshinda kihalali, Raila Odinga hawakupewa ushindi wao na Tume ya Uchaguzi Kenya, na hivyo wameamua kupambana na Wakikuyu.
Wakikuyu nao wamechoka na kuamua kupambana na makabila mengine yaliyoungana dhidi yao, nao wanafanya uharibifu na vurugu kadri inavyowezekana.
Hadi hivi sasa zaidi ya watu 1,000 wameripotiwa kufariki dunia, idadi ambayo inaweza kuongezeka kama juhudi hazitafanyika katika kuleta amani.
Watoto na raia wengine wasio na hatia wamejikuta katika wakati mgumu kwa sababu tu wanatoka kabila Fulani, licha ya ukweli kwamba hawahusiki kwa namna yoyote na wizi wa kura unaodaiwa kufanywa.
Unasoma habari ya waumini wa dini fulani wakiwa wamechomwa moto wakiwa ndani ya Kanisa, sababu tu wanatoka kabila fulani. Baada ya hapo, unasoma habari za watu wa kabila fulani kuhamishwa chini ya ulinzi mkali wa Polisi ili tu wasidhuriwe na watu wa kabila fulani.
Unaendelea kupata habari ya kusikitisha kwamba hata kama wewe ni Mkikuyu umefunga ndoa na Mjaluo, kama mkeo anaishi eneo la Wakikuyu au Wajaluo basi atalazimika kuhama na kurudi kwao, vinginevyo atauawa na watu wa kabila lako ambao hawamtaki.
Wakati nasoma habari hizo zote naanza kufikiria mambo mengi. Nafikiria kwamba hali ya aina hiyo itaendelea hadi lini, kwa watu ambao mwaka 2005 niliwaona kama ndugu wanaoishi pamoja.
Nafikiria kwamba hali Kenya ni mbaya, lakini naamini haiwezi kuachwa ikawa hivyo na kwamba juhudi ni lazima zifanyike kukomesha mauaji haya, hususan ya raia wasio na hatia.
Naifikiria Kenya ya sasa na hali itakavyokuwa siku zijazo, najenga hisia kwamba watu hawa 800 na zaidi waliokufa na wanaoweza kuendelea kufa wanaweza kuwa mwanzo wa tatizo kubwa kwa Kenya ya miaka ijayo kuliko hivi sasa.Najaribu kufikiria namna watu wanavyokufa na kuziacha familia zao katika wakati mgumu. Nafikiria watu wanaokufa na kuacha watoto wadogo, na wake zao wakiwa katika hali ya huzuni.
Nafikiria hali ikiendelea hivi miaka 15 au 20 ijayo hali itakuwaje? Vipi mtoto ambaye leo hii ana miaka mitatu au mitano, ambaye miaka 15 au 20 ijayo, atakuwa anahangaika na maisha.
Hapa namfikiri mtoto ambaye mama yake atashindwa kumlipia ada kwa ajili ya masomo ya sekondari, mtoto ambaye atakuwa na shauku ya kusoma na kumuuliza mama, baba yangu yuko wapi.
Nafikiri kuna mama ambaye ataona tabu kumhadithia mwanaye, lakini kuna jasiri ambaye atamwambia kwamba baba yako aliuawa na Wajaluo, Wakikuyu na au Wakalenjin.
Naifikiria hali atakayokuwa nayo baada ya kuambiwa kwamba watu hao hawakuishia kumuua tu, bali walichoma moto nyumba, waliua mifugo na kuzika watu wengine wakiwa hai.
Namfikiria mtoto huyu atakavyokuwa katika hali ya unyonge na masikitiko, namfikiria namna ambavyo atakubali yaishe na kuanza kujitafutia maisha bila elimu, elimu ambayo pengine angeweza kuipata kama baba yake angekuwa hai, kwani baba yake alikuwa na mipango na malengo mazuri ya kumsomesha.
Hata hivyo ameshindwa kupata elimu kwa sababu tu Wajaluo au Wakikuyu au Wakalenjin walimuua baba yake.
Namfikiria mtoto mwingine ambaye mara baada ya kumuuliza mama yake alipo baba, mama yake akaanza kwa kumwambia baba yako aliuawa na Wakikuyu au Wajaluo au Wakalenjin, naufikiria unyonge atakaokuwa nao.
Namfikiria mama huyo ambaye hatosita kumwambia kwamba watu hao walimuua baba yako, wakawauwa na ndugu zako wote na kuwabaka ovyo wasichana na kisha kupora mali na ndio maana wametuacha katika hali ya umasikini.
Nafikiria hali itakuwaje mtoto huyu akiwa tofauti na yule wa kwanza, nafikiria huyu akiamua kusema maadui zangu toka leo ni Wajaluo au Wakikuyu au Wakalenjin.
Naendelea kufikiria hali itakuwaje miaka 15 au 20 ijayo iwapo kutakuwa na watoto wa aina hii mmoja mmoja katika familia 800 ambazo wazazi wao wameuawa kinyama.
Natafakari hali itakavyokuwa iwapo watoto hawa wote wataamua kulipa kisasi cha kuuawa kwa baba zao, mali zao kuporwa na dada zao kubakwa.
Hapa naifikiria Kenya ya kesho. Nazungumzia miaka 15 au 20 ijayo, kama vurugu hizo zinazoendelea na kuandamana na mauaji zisipokomeshwa, hali katika Kenya ya miaka hiyo itakuwaje? Je; hali haiwezi kuwa kama Rwanda? Tusubiri!
No comments:
Post a Comment