Meya Kinondoni katika
tuhuma nyingine nzito
na mwandishi wetu
MEYA wa Manispaa ya Kinondoni, Salum Londa, anatuhumiwa kula njama na kuchota zaidi ya Sh milioni 100 kupitia zabuni ya ununuzi wa matela ya kuzolea taka iliyotolewa na Manispaa hiyo.
Taarifa za uhakika ambazo MTANZANIA imezipata zimedai kuwa, Julai mwaka jana, kikao cha bajeti cha Manispaa ya Kinondoni, kilipitisha uamuzi wa kununua matela 25 ya kuzolea taka.
Matela hayo 25 yalikuwa yagharimu kiasi cha Sh milioni milioni 8 kila moja, ambapo manispaa hiyo ingelipa jumla ya Sh milioni 200.
Lakini badala yake, inadaiwa kuwa kiongozi huyo wa manispaa hiyo kwa kushirikiana na baadhi ya maofisa wasiokuwa waaminifu, waliamua kuyalipia matela hayo Sh milioni 12 kila moja, na wao kujipatia Sh milioni 100 kinyume cha sheria.
Uchunguzi zaidi umebaini kuwa, baada ya kujipatia Sh milioni 100, kiongozi huyo na wenzake, walitaka kujipatia fedha zaidi, kwa kuongeza malipo hayo kutoka Sh milioni 12 kwa kila moja, hadi milioni 15, katika ununuzi wa matela mengine 25.
Hata hivyo jaribio la pili mpango huo wa kujipatia Sh milioni 180 kwa kununua matela 25 kwa Sh milioni 15 kila moja badala ya Sh milioni 8, lilikwama baada ya kiongozi mwingine wa hapo kubaini na kufuta malipo hayo, wakati kiongozi anayetuhumiwa kuongoza genge la ubadhirifu akiwa safarini.
Kutokana na malipo hayo kufutwa, kampuni moja ya mjini Tanga (jina linahifadhiwa) ambayo ilishinda zabuni za kuiuzia Manispaa ya Kinondoni matela hayo, inakusudia kufungua kesi ya madai kutokana na kushindwa kufanyika biashara hiyo kwa mujibu wa makubaliano ya awali.
Kampuni hiyo ya Tanga imechukua hatua hiyo baada ya Manispaa ya Kinondoni kutangaza upya zabuni ya ununuzi wa matela hayo, hatua ambayo imetokana na njama za kutaka kuiba mamilioni ya fedha za manispaa.
Pamoja na kutokea kwa ubadhirifu huo wa fedha za walipa kodi wa Manispaa ya Kinondoni, hakuna hatua zozote za kinidhamu au kisheria zilizochukuliwa na uongozi wake wa manispaa.
Alipoulizwa kuhusu tuhuma hizo kwa njia ya simu jana, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, Noel Mahyenga, hakukanusha, wala kuzungumzia suala hilo kwa undani.
“Ndugu mwandishi haya si mambo ya kuzungumza kwenye simu, kwanza nitajuaje kama nazungumza na wewe? Nitafute uje na vithibitisho vya tuhuma hizo, pamoja na press card (kitambulisho cha uandishi wa Habari cha serikali) ndiyo tuzungumze,” alisema na kuongeza:
“Kesho siwezi kupatika kwa sababu nipo ziarani vijijini, nitafute baada ya siku mbili nitakuwa nimemaliza ziara yangu.” alisema.
Kwa upande wake, Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Salum Londa alipotafutwa, alisema kuwa hawezi kuzungumza kwa njia ya simu, na kutaka mahojiano yafanyike rasmi ofisini kwake, akiahidi kuonyesha nyaraka zote kuhusiana na tuhuma hizo.
Katika tuhuma nyingine za hivi karibuni, Londa, anatuhumiwa kughushi nyaraka ili kumuwezesha binti yake (mkwe) kwenda Marekani, Julai mwaka jana.
Anadaiwa kutumia vibaya madaraka yake kumjumuisha Amina Salehe Londa, katika orodha ya madiwani vijana, ili aweze kwenda Marekani.
Madiwani vijana kutoka Manispaa ya Kinondoni walikuwa wamealikwa jijini Florida, Marekani, mwezi Julai mwaka jana na Taasisi ya Sister Cities International.
Lakini jitihada za Londa kumpeleka mtoto wake, ziligonga ukuta, baada ya Ubalozi wa Marekani kumnyima kibali cha kuingia nchini humo (VISA), tarehe 11 ya mwezi huo.
Uchunguzi zaidi umebaini kuwa, kabla ya kufanyika kwa safari hiyo, mtoto huyo tayari alikuwa ameshalipwa fedha za safari kiasi cha Sh milioni 6, na manispaa hiyo.
Katika safari hiyo ambayo Alhaji Londa naye alikwenda Marekani, pia anatuhumiwa kurejea nchini na kompyuta ndongo (laptop) 20, na kuziuza kwa manispaa, ingawa katika mkutano wake na waandishi wa Habari wiki iliyopita, alikanusha kuwahi kufanya biashara hiyo.
Lakini takwimu tulizonazo zinaonyesha kuwa Meya huyo aliuza kompyuta hizo kwa Sh milioni 3 kila moja, bei ambayo inalalamikiwa kuwa ni kubwa, ikilinganishwa na bei ya soko.
Wiki iliyopita, baadhi ya madiwani katika manispaa hiyo walielezea kutokuwa na imani na kiongozi huyo kutokana na kutuhumiwa kwa vitendo mbali mbali vya ufisadi katika utekelezaji wa majukumu yake.
Maidwani hao walisema kuwa kuna mpasuko mkubwa miongoni mwao, kiasi cha kukwamisha utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Madiwani hao pia wanamtuhumu Londa kwa kujaribu kuupa sura ya udini mgogoro wa kiwanja namba 965, kilichopo Kata ya Kawe, katika manispaa hiyo.
Katika sakata hilo la kiwanja, Londa ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Kawe, anatuhumiwa kukiuka Sheria ya Ardhi Mijini ya mwaka 1999, kifungu namba 4.
Kwa mujibu wa sheria hiyo, mwekezaji yeyote kabla ya kumilikishwa eneo, anapaswa kulipa fidia kwa mujibu wa bei ya soko kwa wakati husika.
Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanyika, kiwanja hicho chenye ukubwa wa mita za mraba 36,667, kilipaswa kulipiwa fedha zisizopungua Sh milioni 200, lakini malipo hayo hayajawahi kufanyika.
Kiwanja hicho kwa sasa kinamilikiwa na Bodi ya Wadhamini ya Taasisi ya Masjid Qiblatain, na tayari kimezungushiwa ukuta, huku ujenzi wa msikiti, shule, na majengo mengine ukiendelea.
Kiwanja hicho kinapakana na kingine kilichouzwa na manispaa hiyo mwaka juzi, na kuzua tafrani kubwa kati ya wakazi wa eneo hilo, na mwekezaji aliyekusudia kujenga shule.
Katika sakata hilo la awali lililohusisha wakazi wa eneo hilo, ambapo walifikia hatua ya kuvunja ukuta uliokuwa ukijengwa na mwekezaji aliyeuziwa eneo, Meya Londa, alilaumiwa kuhusika na uuzwaji wa kiwanja hicho, ambacho ni mali ya manispaa.
No comments:
Post a Comment