MZEE CHIFUPA AMUOA
MAMA YAKE AMINA CHIFUPA
Fatma Amri na Vaileth Mushi
HII SI UTANI!, Mzee Hamis Gabriel Chifupa juzi usiku (Jumatatu), alifunga ndoa rasmi na mama yake mzazi marehemu Amina Chifupa aliyefahamika kwa jina la Katarina Mbaga........
Kwa mujibu wa chanzo chetu cha habari ambacho kilihudhuria sherehe hiyo, mzee huyo alifunga ndoa ya Kikristo kwa dhehebu la Kikatoliki nyumbani kwake Mikocheni, jijini Dar es Salaam saa 1.00 usiku.
Ndoa hiyo ambayo ilifana, ilihudhuriwa na umati mkubwa wa watu huku maharusi hao wakiwa wamependeza kupita kiasi.
Chifupa na Katarina ni wazazi wa marehemu Amina Chifupa, aliyekuwa Mbunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (CCM) aliyefariki Juni 26, mwaka jana.
Habari zinasema kuwa baada ya kufungishwa ndoa hiyo, mzee Chifupa na mkewe, walipeana mikono kama ishara ya kupongezana na pia ndugu na marafiki walikwenda kuwapongeza kwa kuchukua uamuzi huo wa busara.
Harusi hiyo iliendeshwa na waongozaji shughuli watatu (MC), Maimartha Jesse, Mtangazaji wa Kituo cha Televisheni cha East African (Channel 5), Sauda Mwilima wa Star TV na Sakina Lioka, ambaye ni Mtangazaji wa Radio Clouds ambao walifanya kazi hiyo kwa zamu.
Mtoa habari wetu alisema mara baada ya waalikwa kutoa zawadi zao kwa maharusi, waendesha shughuli (Ma MC) nao walipata nafasi kama hiyo.
Waendesha shughuli hao, walitoa kali kwani mara baada ya kuwapa zawadi, huku wakiongozwa na kibao cha Pembe la Ng’ombe kilichopigwa na kundi la Dar es Salaam Modern Taarab, walikata mauno ya kufa mtu na kuwafanya watu waliohudhuria sherehe hiyo kulipuka kwa mayowe.
Watoto wa mzee Chifupa, Aisha na Nyami nao walikuwa ni miongoni mwa watu walioonyesha furaha yao siku hiyo kwani baada ya kuitwa mbele na MC Sakina, walikwenda kuwapa zawadi wazazi wao huku wakisindikizwa na marafiki zao kama ishara ya kuwapongeza.
Habari zinasema kuwa pamoja na yote hayo, wageni waalikwa walikula, kunywa na kusaza huku wakiburudika na muziki mnene nyingi zikiwa nyimbo za Injili.
No comments:
Post a Comment