Makamu wa Rais
ni yapi?
Edson Kamukara
KATIKA Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ibara ya 47.-(1) inatamka wazi kuwa kutakuwa na Makamu wa Rais ambaye atakuwa ndiye msaidizi wa rais kuhusu mambo yote ya Jamhuri ya Muungano kwa jumla na hususan (a) Atamsaidia rais katika kufuatilia utekelezaji wa siku hata siku wa mambo ya muungano. (b) Atafanya kazi zote atakazoagizwa na rais na (c) Atafanya kazi zote za rais kama rais hayuko kazini au yuko nje ya nchi.
Nimeanza kwa kunukuu katiba ya nchi kudhihirisha jinsi serikali yetu inavyoheshimu utawala wa sheria, kwa kuifuata katiba kwani cheo hicho cha Makamu wa Rais kipo na kwa sasa Dk. Ali Mohamed Shein ndiye anakalia kiti hicho.
Makamu wa Rais, Dk. Ali Mohamed Shein akiangalia nyama katika moja ya mabucha, Buguruni, jijini baada ya kushtukia watu wanapandisha bei kiholela katika mida ya
sikukuu ya Idd. (11 October 2007).
Tunaweza kusema Dk. Shein ni Makamu wa Rais pekee katika historia ya nchi hii tangu uhuru kuweza kuwa na bahati ya kushika wadhifa huu kwa vipindi viwili na akiwa na marais wawili tofauti.
Dk. Shein aliibuka katika medani ya kisiasa na kuwashangaza wengi mwaka 2001 alipoteuliwa na Rais mstaaafu Benjamin Mkapa, akiwa anachukua nafasi ya Dk. Omar Ali Juma, aliyefariki dunia ghafla mwaka huo, aliyekuwa Makamu wa Rais.
Makamu wa Rais Dk. Ali Mohamed Shein akizindua
awamu ya pili ya programu ya kupambana na rushwa nchini
kwenye sherehe ya siku ya maadili ya kitaifa.
(10 December 2006).
Kusema kweli wengi tulikuwa hatumjui Dk. Shein pamoja na kwamba alikuwa Waziri wa Utawala Bora katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), na hili bila shaka linatokana na yeye kutokuwa mtu wa maneno mengi, zaidi ni mchapakazi kwa vitendo.
Nyota ya Dk. Shein iliendelea kung'aa hata baada ya Rais Mkapa kumaliza muda wake wa uongozi hapo Desemba 2005, kwani baada ya Rais wa sasa Jakaya Kikwete kuchaguliwa na Chama chake Cha Mapinduzi (CCM) kugombea urais bado aliona aendelee na Dk. Shein awe makamu wake.
Makamu wa Rais ni kiongozi wa ngazi ya juu na muhimu sana katika nchi yoyote ile yenye kufuata demokrasia na ndiyo sababu ya kuanza makala hii nikiwa nanukuu katiba yetu ya nchi kuonyesha wadhifa na majukumu ya kiongozi huyu.
Tukisimamia ibara hii ya katiba katika kipengele cha (c), kinatosheleza kutuelekeza nini Dk. Shein kama Makamu wetu wa Rais anatakiwa kufanya, Rais Kikwete anapokuwa hayuko kazini au yuko nje ya nchi.
Katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Tatu, Watanzania wengi mbali na kutojua katiba ya nchi inasemaje pale rais anapokuwa nje ya nchi, lakini bado waliweza kughadhabishwa na kitendo cha rais wa wakati huo kuhutubia taifa mwisho wa mwezi, akiwa nje ya nchi alikokuwa amelazwa, japokuwa ulikuwa ni utaratibu aliokuwa amejiwekea anapokuwa hapa nchini.
Waliojitokeza kuhoji katiba inasemaje kuhusu nafasi ya Makamu wa Rais kufanya kazi hiyo ya kuhutubia taifa kwa niaba ya Rais, walijibiwa kuwa Rais Mkapa aliamua kufanya hivyo ili kuwaondolea hofu Watanzania kuwa alikuwa hayuko mahututi sana kama wengi walivyodhania.
Sababu hii ilikuwa nzuri ila kikatiba aliyumba ama tunaweza kusema ni kama hakumthamini makamu wake kuwa anaweza kutekeleza kazi zake wakati yeye yuko nje ya nchi kama katiba inavyomruhusu.
Wakati tunaanza kusahau kituko hicho, mapema mwezi huu tumejikuta tunaingia kwenye kituko kingine kinachoweza kufananishwa na kile cha Rais Mkapa, maana hata Rais Kikwete Septemba 15, mwaka jana alikuwa na ziara ndefu nchini Marekani iliyomchukua hadi mwanzaoni mwa Oktoba, na kwa taarifa zilizotolewa na wasaidizi wake ni kwamba hotuba ya mwisho wa mwezi huo kwa wananchi isingekuwapo kwa kuwa rais hakuwapo nchini.
Tukio hili limenipa maswali mengi sana ambayo pengine majibu yake ni lazima kuonana na wanasheria wanifafanulie ili kuniondolea utata nilionao, maana kama kifungu cha katiba kinasema wazi lakini hakitekelezeki, maana yake nini.
Hivi ni kweli hata sisi tuamini kuwa Dk. Shein hawezi kuhutubia taifa mwisho wa mwezi kama rais yuko nje ya nchi, na kama ndivyo alipewaje nafasi hiyo kubwa? Ama tukubali kuwa anaweza, isipokuwa hotuba zenyewe rais anahutubia anachokitaka yeye wala makamu wake hausiki?
Baada ya kujiuliza maswali mengi yasiyokuwa na majibu niliamua kutumia ujanja wetu waandishi wa habari wa kuingia mtaani kujua maoni ya baadhi ya wananchi wa Mwanza kuona nao wanasemaje kuhusu kutokuwapo kwa hotuba ya rais mwisho wa mwezi kwa kuwa Rais Kikwete atakuwa ziarani bado nje ya nchi.
Kwa kweli hapa ilizuka mitazamo mingi tofauti kwani wapo walioliona kama ni jambo la kawaida na wengine walishauri kuwa ni bora angewaachia wasaidizi wake wa Ikulu ili mwisho wa mwezi waitoe kwa vyombo vya habari ichapishwe.
Lakini kadiri nilivyozunguka ndipo nikazidi kukutana na maoni tofauti, kuna aliyeniomba nimsaidie kuuliza kwa wanasheria ili ajue majukumu ya Makamu wetu wa Rais yanaishia wapi.
"Mwandishi sikiliza, katiba ya nchi inasema wazi kuwa kama rais yuko nje ya nchi, makamu wake ndiye anakaimu madaraka, sasa iweje tena kwa marais wote wawili Mkapa na Kikwete wanakuwa nje ya nchi kisha wanashindwa kumwacha Dk. Shein ahutubie taifa mwisho wa mwezi? Hivi majukumu ya Dk. Shein kama Makamu wa Rais ni yapi?" alihoji mwananchi huyo.
Pamoja na wengi kulalamikia marais wetu kuwa hawamthamini Dk. Shein, wapo waliofikia hatua ya kuhoji kuwa, kama kweli hizi hotuba za mwisho wa mwezi zina manufaa kwa Watanzania au ni za rais binafsi wala makamu wake hashirikishwi na ndiyo maana hata wanapokuwa hawapo nchini wanashindwa kumwachia makamu akawahutubia Watanzania.
"Nakumbuka hotuba ya Kikwete Julai mwaka jana mjini Dodoma alipowahutubia wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, sasa hiyo nayo tuseme ni hotuba kwa Watanzania? Hivi kama nchi ni ya vyama vingi lakini rais anachagua kuwahutubia wanachama wa chama chake tu na tunaambiwa kuwa ni hotuba ya rais kwa Watanzania wote, hivi kweli hata wewe unaweza kusema hizi hotuba zina maana yoyote?"
" Si unaona rais akisafiri kwenda nje ya nchi na hotuba hakuna mwisho wa mwezi, hotuba kama ni za kitaifa na za msingi, iweje asiachiwe makamu wake, kama Kaimu Rais kwa muda wote anapokuwa hayupo?" alihoji mwananchi mwingine.
Waliendelea kuhoji ni lini itatokea rais akawaita na wajumbe wa vyama vya upinzani kama vile DP au TADEA n.k awahutubie na hiyo iwe ni hotuba yake ya mwisho wa mwezi kwa taifa?
Katiba ni chombo kilichowekwa kwa ajili ya kutuongoza na ni sharti kila mtu akafanya kazi zake kwa kuzingatia katiba hiyo, hata rais na viongozi wengine nao wameapa kuilinda na kuitetea katiba ya nchi.
Wote tunaamini kuwa Dk. Shein ni msomi na ni mchapakazi ndiyo maana akapewa wadhifa huu alionao, hivyo basi, hana budi kutendewa haki yake kikatiba pale rais wetu anapokuwa nje ya nchi, ni bora makamu wake akaachiwa atekeleze kazi zote, ikiwemo hata kuhutubia taifa mwisho wa mwezi kwani tunamwamini kuwa anaweza.
Na kama itakuwa utaratibu huu wa watawala wetu kusafiri nje ya nchi na kushindwa kuwaamini wasaidizi wao wanaowaachia madaraka, ni bora katiba ikafanyiwa marekebisho mapema ili tujue tu kuwa rais anapokuwa hayupo kila kazi inayomhusu inasimama mpaka arudi na kwa maana hiyo nafasi ya makamu itakuwa haina maana yoyote ile kuwapo.
Mwandishi wa makala hii ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mt. Augustine, Mwanza. Anapatikana kwa barua pepe; edkamukara@yahoo.com; simu 0755-2727351.
No comments:
Post a Comment