Wednesday, February 06, 2008


Shule ina mwalimu mmoja tu


na eliasa ally, iringa


SHULE ya Msingi Ugele, Kata ya Ugele Manyigu, mkoani Iringa, ina mwalimu mmoja tu ambaye anafundisha madarasa yote shuleni hapo kwa muda mrefu sasa, kutokana na kutokuwapo kwa walimu wengine.

Kibaya zaidi, Mtanzania ilibaini kuwa wanafunzi wa darasa la saba, wamekuwa wakiwafundisha wanafunzi wa madarasa ya chini wakati mwalimu huyo anaposafiri kikazi au kufuata mshahara wake mjini Iringa.

Kutokana na hali hiyo, hadi sasa wanafunzi wa darasa la saba hawajasoma masomo mengine mbali na somo la sayansi, ambalo ndilo linalofundishwa na mwalimu huyo mmoja. Mwanafunzi anatakiwa kusoma masomo zaidi ya tisa ili aweze kufanya mtihani wa darasa la saba.

Shule hiyo ina wanafunzi 128 chini ya Mwalimu Mkuu, Rasir Mdeme, ambaye amesomea masomo ya sayansi alipokuwa katika mafunzo ya ualimu.

Lakini pamoja na matatizo hayo, bado shule hiyo iliweza kufaulisha wanafunzi wawili kwenda kidato cha kwanza mwaka jana.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Ugele, Jamrus Mwisaka, amedai kuwa hali mbaya ya kimaendeleo katika eneo hilo ndiyo inayowakimbiza walimu wanaopangiwa kufundisha katika shule hiyo.

“Hatuna maji safi, tunapata maambukizo ya magonjwa ya tumbo na ngozi, maji tunayokunywa yana chumvi nyingi, hivi nani kweli anayeweza kuja hapa kuishi?” alilalamika Mwenyekiti huyo.

Mwenyekiti huyo na wakazi wengine wameiomba serikali na Mbunge wao, Monica Mbega, kutembelea eneo hilo na kutafuta njia ya kupambana na tatizo hilo ambalo wanasema linazidi kudunisha maendeleo katika kijiji chao.

Ofisa Elimu Taaluma Mkoa wa Iringa, Euzebios Mtavangu, alisema yeye na wenzake hawana la kufanya, kwa kuwa kila wakiwapeleka walimu katika shule hiyo wanakimbia.

“Hiyo yote ni kweli inatokana na ugumu wa hali ya maisha ya eneo hilo, kwa hiyo sisi hatuna la kufanya,” alisema.


No comments: