Sunday, July 06, 2008

Ajali ya ndege yaua

wawili


NDEGE ndogo, mali ya Wizara ya Maliasili na Utalii, imeanguka wilayani Monduli mkoani Arusha, na kusababisha vifo vya watu wawili waliokuwa wakisafiri na ndege hiyo.

Kamanda wa Polisi mkoani Arusha, Basilio Matei, aliwataja waliofariki dunia kuwa ni pamoja na Mkurugenzi Msaidizi wa Wanyamapori, Mariam Zacharia na rubani wa ndege hiyo aliyemtaja kwa jina moja la Kapteni Pius.

Kamanda Matei, alisema ndege hiyo namba 5H AWF, mali ya Wizara ya Maliasili na Utalii, iliyokuwa ikisafiri kutoka jijini Dar es Salaam kwenda Loliondo wilayani Ngorongoro, ilianguka juzi katika eneo hilo.

Alisema ndege hiyo ilipotoka Dar es Salaam, ilitua katika Uwanja wa Ndege wa Kilimoanga wa Arusha kwa ajili ya kujaza mafuta na kisha kuendelea na safari yake ya kwenda Loliondo.

Kamanda Matei alisema ndege hiyo iliondoka Uwanja wa Ndege wa Arusha, juzi saa 6.00 mchana kwenda Loliondo, lakini ilisubiriwa hadi jioni bila mafanikio, ndipo maofisa wa wanyama pori Loliondo, walipoamua kutoa taarifa polisi.

“Wasiwasi ulitanda baada ya kukatika ghafla kwa mawasiliano baina ya rubani wa ndege hiyo na muongoza ndege wa Arusha, na pia kutokuwa na taarifa za kutua kwa ndege hiyo,” alisema Kamanda Matei.

Alisema baada ya muda kupita, maofisa waliokuwa Loliondo wakiwasubiri uwanjani, walipiga simu kutaka kufahamu kama ndege hiyo imeishaondoka.

Kwa mujibu wa Kamanda Matei, mabaki ya ndege hiyo yalipatikana jana wilayani Monduli baada ya juhudi za wananchi, polisi na wataalamu mbalimbali wa serikali.

Hii ni ndege ya pili kupata ajali mkoani hapa, baada ya helkopta ya Jeshi la Wananchi (JWTZ) kuanguka maeneo ya Ziwa Natron, ambako watu kadhaa walikufa.


Kutoka Tanzania Daima

No comments: