Kiingereza shuleni
NIMEKUWA nikifuatilia mjadala usio rasmi kuhusu matumizi ya lugha ya Kiingereza katika kufundishia katika shule za msingi, sekondari au hata vyuo vya elimu ya juu.
Katika mjadala huu yamejikita makundi makubwa mawili - maoni kuwa Kiingereza shuleni kwa faida ya nani? (mfano, Irene Mark, Tanzania Daima, Jumatano Julai 8, 2008).
Kundi hili halioni umuhimu wa kutumia Kiingereza ambacho kimeonekana kuwa kigumu kueleweka na kutumika na Watanzania walio wengi.
Kundi la pili ambalo najiunga nalo bado linaona kuwa kuna umuhimu mkubwa wa kutumia lugha ya Kiingereza.

2 comments:
Sipingi umuhimu wa Kiingereza kwenye dunia ya sasa ya utandawazi na TEKNOHAMA inayokwenda kasi kama mionzi ya jua!
Sio kama hatuoni umuhimu wa kujua Kiingereza kwa sisi tulio kwenye kundi la tunaotaka Kiswahili kifundishwe tokea chekechea hadi vyuo vikuu, kama ambavyo kundi linalotaka Kiingereza kifundishwe toka chekechea hadi vyuo vikuu linavyotufikiria.
Lugha zote zote kuu duniani zisingeweza kuendelea kama zingebaki kuwa lugha tu za taifa na kuzungumzwa, halafu lugha ingine toka nje ya nchi iwe lugha ya kufundishia mashuleni hadi vyuo vikuu. Hakuna!!!
Lugha zote hizo kubwa zimefikia hapo zilipo kwa sababu zimetumika kufundishia toka chekechea nadi vyuo vikuu. Lugha inapokuwa ya kufundishia, msamiati wake unaongezeka na kukua kila siku sambamba na maendeleo yaliyopo ya wakati.
Nikichukua mfano wa Kinorwejiani (Nimesoma, naishi na nafanya kazi ya kufundisha hapa Norway kwa Kinorwejiani) na TEKNOHAMA. Hii nyanja haikuanza muda mrefu. Na ilipoanza ilikuwa kwa lugha ya Kiingereza. Wanorwejiani (Waskandinavia na WaNordic) hawakuwa nyuma. Wakaichukua kama ilivyo kwa Kiingereza na kuanza kuitumia. Wakati inaanza nilikuwa Norway, nimeona jinsi ilivyopokelewa kwa Kiingereza na hadi sasa iko kwenye Kinorwejiani kwa asilimia 90. Bado wanaendelea na kuikuza kwa Kinorwejiani. Na ndivyo ilivyokuwa kwa lugha zote kubwa duniani. Sasa TEKNOHAMA inatumika kwenye lugha zao.
Hivi majuzi tu Waziri wa Utamaduni wa Norway, Bw. Trond Giske amepeleka muswada wa kukiimarisha Kinorwejiani toka mashuleni hadi chuo kikuu na kuhakikisha hakipitwi na wakati. Lengo ni kukifanya kiende sambamba na haraka ya utandawazi na TEKNOHAMA.
Kwenye soko la utandawazi, wenye kuuza bidhaa nao si wajinga. Kwenye soko watatangaza na kuuza bidhaa kwa lugha ambayo wanaona bidhaa zao zitauzika kwa wingi. Tunaona Microsoft, Google na Wikipedia walivyoanza. Wanajaribu kwa Kiswahili. Wanafanya hivyo kwa sababu wanaona watu milioni 50 wanaozungumza Kiswahili ni soko kubwa, wasingependa kuona soko hilo linawapita pembeni kwa sababu tu hao milioni 50 hawajui Kiingereza kwa ufasaha!
Kutumia Kiswahili pekee au Kutumia Kiingereza pekee hakumfanyi mtu kuwa na akili. Kuwa na akili sana ni hulka ya mtu binafsi aliyopewa na Mungu au kwa jitihada zake mwenyewe. Na jitihada hizo zinaweza kuwa kwa lugha yoyote ile ikiwemo Kiswahili.
Mwalimu Nyerere alisema ”Kiingereza ni Kiswahili cha dunia na Kiswahili ni Kiingereza cha Afrika”
Hakukosea hata kidogo. Sehemu kubwa ya utamaduni wa taifa uko kwenye lugha. Taifa ambalo halina lugha yake ya taifa ya Kiafrika, hata utamaduni wake nao si wa Kiafrika. Utamaduni wake unayumbayumba! Tunaona mifano kwenye nchi zetu za Kiafrika. Ndio maana hata baba wa taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alisema ”Kiswahili ni Kiingereza cha Afrika” alikuwa na maana hiyo ya kuwa mataifa mengi ya Afrika yanayotumia lugha za kigeni kama lugha zao za taifa na za kufundishia, kina kitu kinakosekana kwenye hizo nchi. Wananchi wengi wa mataifa, wanashindwa kuwalewa viongozi wao kwa sababu nchi haina lugha ya taifa ya Kiafrika, badala yake inatumia lugha ya kigeni. Hilo halituhusu sisi Watanzania.
Lugha ya taifa tunayo, cha muhimu ni kufanya mikakati ya kuikuza ili iende sambamba na utandawazi, TEKNOHAMA na mengineyo. Hiyo haiwezekani na haitawezekana kama lugha haifundishwi mashuleni hadi vyuo vikuu. Lugha inapofundishwa kwenye hizo nyanja ndivyo inavyokuwa! Msamiati wa lugha haiwezi kutungwa tu na ”BAKITA” halafu ukakaa kwenye vitabu ambavyo navyo vitakaa tu kwenya maktaba, bila ya kutumikia na kutegemea kuwa watu waujua huo msamiati mpya unaotungwa!
Wangapi Watanzania wanaojua misamiati inayotungwa kila mara na BAKITA? Ukondoa miachache tu ya maneno ya kawaida ya kila siku ya Kiswahili? BAKITA ikishirikiana na TUKI imetunga misamiati mingi ambayo kama ingekuwa inatumika pale inapopaswa, Watanzania tusingesema kuwa Kiswahili hakina misamiati hivyo tusubiri mpaka kiwe na misamiati ndipo kifundishwe! Ili lugha ikue, inabidi ifundishwe mashuleni na vyuoni. Wanaisimu na wanazuoni wengi wanakubaliana na hilo. Kama walivyofanya wenzetu wa Skandinavia, Nordic na nchi zingine inawezekana. Maendeleo ya nchi hayapatikani kwa sababu nchi inatumia au watu wengi wa nchi fulani wanatumia Kiingereza. Vigezo vingi vinatumika ili nchi iendelee. Nchi za Skandinavia (na za Nordic) hazikuendelea kwa sababu watu wake au nchi kijumla inatumia Kiingereza, la hasha. Ni kuchapa kazi na mikakati na vigezo vingine ndivyo vilivyofanya hizi nchi za Kaskazini zimeendelea. Hivyo hivyo tukichukulia Ujerumani, Ufaransa, Hispania, Urusi, Ujapani, Korea ya Kusini (na zingine hazikuendelea kwa sababu Kiingereza kinafundishwa toka chekechea hadi vyuo vikuu). Zimeendelea kwa lugha zao na bado wanaweza kuzungumza Kiingereza. Tuna madaktari wengi, wataalamu wengi wa nyanja mbali mbali waliosomea enzi hizo, Urusi na nchi za Kikomunisti. Wamejifunza taaluma zao kwa lugha za nchi hizo. Na bado wanazungumza Kiingereza na wanakubalika kwenye fani zao.
Ndiyo, Warusi wengi. Wachina wengi, Wajapani wengi (na wengine) wanataka kujifunza Kiingereza (na wengine). Kuharakisha kujifunza kwao Kiingereza hakuamanishi kuwa nchi zao, zinataka kutumia Kiingereza kama lugha ya kufundishia kutoka chekechea nadi vyuo vikuu, la hasha. Watu wanaweza kujifunza lugha yoyote ya kigeni, wakaielewa na kuizungumza kama wenyeji wa nchi hiyo bila ya nchi zao kupoteza sehemu kubwa ya utamaduni wa nchi, yaani lugha ya taifa. Kwa Watanzania ni Kiswahili!
Juzi juzi Rais wa Ufaransa Nikolai Sarkozy amependekeza kuwa dola lichukue mamlaka ya kuhodhi shirika la utangazaji na habari la Ufaransa. Dola lichague hata mkurugenzi mkuu (alikuwa anachaguliwa na bodi). Lengo ni kuhakikisha kuwa Kifaransa kinapewa kipa umbele kwenye nyanja zote za maendeleo ya taifa.
Ngoja nitoe mifano midogo tu ya umuhimu wa Kiswahili kama sehemu kubwa ya utamaduni wa Mtanzania ambayo inapaswa kulindwa kwa uvumba na ubani.
Ze Comedy wametingisha fani ya uchekeshaji kwenye luninga huko nyumbani kwa sababu wanazungumza lugha inayoeleweka na kuzungumzwa na watu wengi yaani Kiswahili. Mazingira tuliyonayo Watanzania, yanaeleweka kwa wengi kwa lugha ya Kiswahili. Ndiyo maana kipindi cha Ze Comedy kimekuwa maarufu kwa kiasi chake. Sidhani kama kipindi hicho kingekuwa kwa Kiingereza kingekuwa maarufu kiasi hicho.
Mziki wa kizazi kipya (Bongo Flava) usingepata umaarufu wa kuvuka mipaka nje ya nchi kama ungekuwa kwa Kiingereza. Nakumbuka vijana wa kizazi kipya walipoanza na mziki wa ngonjera (Nauita wa ngonjera kwa sababu unafanana sana na ngojera kwa sisi tulioimba ngonjera enzi zetu! Mwulizeni Naibu Waziri wa elimu, Bi. Mwatumu Mahiza, tulikuwa tukimwita Mwalimu Mwatumu Bakari enzi hizo!) Walipoanza kuimba ”Hip Hip, Rap na R.n.B” kwa Kiingereza hawakufika kokote. Ghafla bin vuu...walipoanza kuimba kwa Kiswahili, mziki huo ukapata umaarufu na upepo ukavuma kutoka nje ya mipaka. Wamefanya hata nchi kama Rwanda, Burundi, Uganda wanaimba kwa lugha zao na Kiswahili aina ya mziki huo, badala ya Kiingereza!
Dr. Asha Rose Migiro na Profesa Anna Tibaijuka hawakufika hapo walipo kwa sababu tu wanazungumza Kiingereza kwa ufasaha. Wamefikia hapo kwa sababu za akili zao. Na kwa sababu akili zao zimefanya kazi ya ziada, wangefika hapo walipo hata kama wangekuwa wanazungumza Kiswahili na Kiingereza cha wastani. Katibu Mkuu mwenyewe wa Umoja wa mataifa, Bw. Kim Ba Moon Kiingereza chake si cha kumfanya Malkia Elizabeth kukaa chini na kufurahia, lakini Malkia Elizabeth anamsikiliza Kim Ba Moon kwa kinachotoka mdomoni. Na kinachotoka mdomoni kinaweza kuwa kwa lugha yoyote! Dr. Boutos Boutros Ghali alichaguliwa kuwa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa si kwa kwa sababu ya Kiingereza chake cha Kiarabu. Alichaguliwa kwa sababu ya uwezo wake na alikuwa anazungumza vizuri Kifaransa kuliko Kiingereza.
Mimi hapa Norway, niliajiriwa kufundisha si kwa sababu najua kuzungumza Kiingereza kama Mwingereza, hapana. Niliajiriwa kwa sababu ya makaratasi yangu yalimridhisha mwajiri wangu. Na makaratasi yangu niliyapata kwa Kiswahili. Kwa jinsi makaratasi yangu yalivyo na Kiingereza changu cha wastani, nilipata kazi ya kufundisha Uingereza, lakini nikaamua kubaki Norway.
Microsoft, Wikipedia na Google wanaona umuhimu wa hilo la soko kwa lugha za kigeni, ndio maana wako kwenye mikakati ya kutumia Kiswahili kwenye huduma zao. Watu milioni zaidi ya 50 wanaotumia Kiswahili ni soko kubwa kiasi ambacho hawawezi kuliacha likapita tu kwa sababu watu hao milioni 50 hawajui Kiingereza kwa ufasaha. Palipo na soko, wenye mali zao wako tayari kutumia lugha yoyote ile.
Ninachotaka kusema kwa kifupi ni kuwa Tanzania tunaweza kutumia Kiswahili kuanzia chekechea hadi vyuo vikuu, bila kupoteza umuhimu wa Kiingereza. Tunachopaswa kufanya Watanzania ni kukipa umuhimu Kiingereza kama lugha ya kigeni. Walimu waliopo wa Kiingereza wapigwe misasa kila wakati ya jinsi ya kufundisha lugha za kigeni, badala ya mbinu wanazotumia waalimu wengi wa Kiingereza tulio nao nchini (Sisemi wote, narudia wengi wao). Wabobee kwenye Kiingereza, kaisi ambacho watakapofundisha matunda yake yatakuwa mazuri kwa vijana watakaofundishwa, wataweza kuzungumza Kiingereza kwa ufasaha.
Halafu tatizo si kumfundisha mtu lugha tu halafu utegemee mtu huyo ataweza kuizungumza lugha ya kigeni kwa ufasaha. Hizo ni ndoto za Alinacha. Sidhani kama ningejifunza Kinorwejiani darasani nikiwa Dar es Salaam halafu mtu ategemee ningebobea kwa kuzungumza Kinorwejiani, bila ya kuwa kuzungumza Kinorwejiani kila siku kwenye maisha ya kawaida, wanaofikiria hivyo wanaishi kwenye nchi ya kufikirika ya Shabani Robert!
Lugha inaenda na matumizi. Ili Watanzania wawe wanazungumza Kiingereza kama Waingereza, Wakenya, Waganda na wengine mabingwa wa ”Kiingereza” inabidi Kiingereza kiwe lugha ya matumizi ya kila siku kwa Watanzania. Kifupi ni sawa na kusema, Watanzania tuache kutumia Kiswahili kwenye matumizi yetu ya kila siku na tutumie Kiingereza. Hivi jamani mmesikia Wakikuyu au Wajaluo wakizungumza Kiingereza? Mnaweza kusema kweli kuwa wanazungumza Kiingereza fasaha?
Profesa Emiratus Mama Birgit –Brock Utne (Chuo Kikuu Oslo, anazungumza Kiswahili fasaha) aliwahi kufundisha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na ameandika vitabu na makala kadhaa juu ya athari za kufundisha Kiingereza kama lugha ya kufundishia na kuwa na lugha ingine ya taifa inayozungumzwa kila siku na wananchi. Tatizo kubwa alilloliona ni:
Wanafunzi wa chuo kikuu wanafundishwa kwa Kiingereza, inapofikia kujadili mada darasani, wanafunzi wanaanza kujadili kwa Kiswahili!!!!
Heko mwana Semboja heko!!!!
Post a Comment