Kroner milioni 5,7 zaibiwa
toka DnB NOR zilikuwa
zitumike TANROADS
Kroner milioni 5,7 (T.shs. 1,350,121,868) zilizokuwa zitumike kwenye mradi wa barabara Marangu mkoani Kilimanjaro zimeibiwa kutoka kwenye benki ya ”DnB NOR” mwaka 2005. Kesi inaendelea mjini Dar es Salaam. Watu watatu ambao si wafanyakazi wa TANROADS wanashutumiwa kwa kuhusika na wizi huo. Mmoja kati ya watuhumiwa hao hajulikani yuko wapi inasadikiwa amekimbia na yuko nje ya nchi. Na wawili wako nje kwa dhamana.
Gazeti la kila siku la Aftenposten la leo ( Julai Mosi) linaandika kuwa Mkurugenzi Mkuu wa TANROADS, Epream Mrema anadai kwa vile watu hao si wafanyakazi wa kampuni, hivyo kampuni haipaswi kudaiwa au kudhulumiwa kwa opotevu wa pesa hizo. Na TANROADS inaidai DnB NOR pesa hizo, kwani zimeibiwa zikiwa chini ya uangalizi wa benki hiyo kwa watu hao kutumia saini batili.
Uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa kuna mtu ndani ya TANROADS aliyewatonya mafisadi hao na kuwapa siri za jinsi ya kuziiba hizo pesa. Mkurugenzi wa habari wa DnB NOR, Morten Skauge amesema kuwa wao hawawezi kuzilipa pesa hizo, huku kesi ikiwa bado iko mahakamani. Bw. Skauge anasema kuwa haiwezekani wizi huo ufanyike bila ya mamlaka ya barabara nchini (TANROADS) kugundua.
Polisi wa Norway nao wameamua kuchunguza wizi wa pesa hizo, kwa kuwapa msaada wenzao wa Tanzania kwa vielelezo vya ushahidi.
Wakati TANROADS wakidai walipwe pesa hizo na DnB NOR, serikali ya Norway inadai TANROADS iwalipe pesa hizo kwa vile hazikutumika kama makubaliano yaliyofikiwa kati ya serikali ya Norway na mamlaka ya barabara Tanzania (TANROADS).
Chanzo: gazeti la Aftenposten.
No comments:
Post a Comment