KESI inayowahusu baadhi ya wake wa vigogo nchini, wanaotuhumiwa kwa utapeli wa sh milioni 43 kupitia mchezo wa upatu, maarufu kwa jina la Dola Jet, ilianza kusikilizwa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam.
Wanawake hao ni pamoja na Evelyn Warioba ambaye ni mke wa Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba, Rose Rupia ambaye ni mke wa Paul Rupia, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Rais wakati wa utawala wa Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi na Rose Mwapachu ambaye ni mke wa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Juma Mwapachu.
Kwa mujibu wa hati hiyo ya mashtaka, wengine ni Rukia Shamte, Regina Chonjo, Saada Chande, Mwanamvua Chonjo, Mwanaidi Mussa, Zainabu Kanji, Shamsa Diwani, Mwajuma Kingwande, Halima Kinabo, Fauzia Kigwe, Halima Shamte, Jokha Mbega na Zulekha Salum.
Kesi hiyo ilifunguliwa na wanawake wanne ambao ni Bhalo Abdulhaman, Asia Amaka, Feroza Kubaga na Tina Shah kwa niaba ya wenzao 22, dhidi ya wanawake wadaiwa 17, wengi wao wakiwa ni wake wa vigogo.
Kesi hiyo ilifunguliwa mwaka 2003 baada ya wanawake hao wa vigogo kudaiwa kuwatapeli akina mama zaidi ya 22 kupitia mchezo wa upatu.
Wadaiwa katika kesi hiyo ni Zarina Madabida na wenzake 16. Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, Madabida anatajwa kuwa ndiye aliyekuwa mhamasishaji mkuu wa mradi huo kupitia kikundi cha akina mama maarufu kama Women Empowering Trust Fund.
Hata hivyo, Rose Mwapachu ambaye hapo awali alikiri kuwa mwanzilishi wa upatu huo, aliamua kurudisha fedha hizo kwa wahusika na kutangaza hatua hiyo kwenye vyombo vya habari.
Kesi hiyo, ilianza kwa kumsikiliza shahidi wa kwanza, Bhalo Abdulhaman ambaye aliieleza mahakama kuwa katika kundi lao, yeye aliwasilisha sh milioni sita wakati fedha zake zilikuwa sh milioni moja na zingine zilikuwa za wanawake wengine watano katika kundi lao.
Walalamikaji katika kesi hiyo, wanadai sh milioni 43, ambazo walizichanga katika mchezo wa upatu na kila mwanachama alitakiwa kuchanga sh milioni moja ili aweze kupata milioni nane ndani ya siku moja.
Wadaiwa katika kesi hiyo wanatetewa na mawakili wa kujitegemea watano ambao ni Profesa Mgongo Fimbo, Amida Sheikh, Jerome Msemwa, Kassim Nyangarika na Richard Rweyongeza.
Kutoka Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment