Monday, November 03, 2008


HOTUBA YA JK KWA WANANCHI

MWISHO WA MWEZI OKTOBA
HOTUBA YA MWISHO WA MWEZI

YA RAIS WA JAMHURI YA

MUUNGANO WA TANZANIA,

MHESHIMIWA

JAKAYA MRISHO KIKWETE,

KWA WANANCHI
TAREHE 31 OKTOBA, 2008


Ndugu Wananchi;
Tuanze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia rehema zake tunapata fursa ya kuzungumza mwisho wa mwezi huu Oktoba kwa mujibu wa utaratibu wetu mzuri. Mwisho wa mwezi uliopita sikuweza kuzungumza nanyi kwa sababu ya kubanwa na shughuli nyingine muhimu zaidi kwa taifa letu.

Suala la OIC
Ndugu Wananchi;
Hivi karibuni kumekuwepo na mjadala usiofurahisha kuhusu suala la Jumuiya ya Kiislamu (OIC) kufuatia taarifa iliyotolewa Bungeni na kwenye vyombo vya habari na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mheshimiwa Bernard Membe.

Nasema isiyofurahisha kwa sababu mjadala huo unaelekea kuchukua sura ya malumbano baina ya waumini wa dini zetu kuu na kupandikiza chuki baina ya serikali na wafuasi wa dini hizo. Ni mjadala unaosikitisha sana jambo ambalo napenda kuwasihi Watanzania wenzangu tusiuendeleze na wala tusiuendekeze. Unaweza kulipeleka taifa letu mahali pabaya tukaanza kupigana wenyewe kwa wenyewe.

Napenda kukumbusha kuwa mwaka 1993 Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ilitakiwa kujiondoa kutoka kwenye jumuiya ya OIC baada ya kujiunga kwa hoja kwamba hilo ni shirika la kimataifa ambalo wanachama wake ni mataifa, hivyo kwa hapa nchini kama kungekuwepo na kujiunga iliyostahili kufanya hivyo ni Serikali ya Muungano. Hayo ndiyo matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hivyo basi Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilijiondoa kwenye OIC na kuiachia Serikali ya Muungano kushughulikia jambo hilo na kuamua ipasavyo.

Tangu wakati huo Zanzibar wamekuwa wanasubiri uamuzi wa Serikali ya Muungano. Kila wakati wenzetu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wamekuwa wanaliuzia suala hilo. Hivi sasa jambo hilo limekuwa mojawapo ya kero kubwa za Muungano zinazoshughulikiwa na Kamati ya pamoja ya Waziri Mkuu na Waziri Kiongozi. Kwa mujibu wa muundo wa Serikali ya Muungano kila kero ya Muungano ina Wizara yake inayohusika nayo kushughulikia. Hivyo serikali, kupitia wizara hiyo, inalishughulikia swala hili kupitiaa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa. Serikali imeamua kufanya utafiti wa jambo lenyewe na ukishakamilika, serikali zetu mbili zitatoa uamuzi.

Ndugu Wananchi;
Nijuavyo mimi, Serikali haijakamilisha kazi yake ya utafiti huo. Kwa sababu hiyo basi Serikali haijafanya uamuzi wowote kuhusu suala la OIC kwa vile hatujui la kufanya bado. Hatujamaliza kazi ya utafiti. Katika hali hii, nawaomba Watanzania wenzangu tuwe na subira. Mtuachie tufanye kazi yetu kwa utulivu ili tuweze kutoa maamuzi kwa hekima na busara.

Aidha, napenda kuwaomba pia hapo tutakapokamilisha kazi hii (sijui lini), mtuache tuitafakari kwa utulivu ili tufanye uamuzi wa hekima utakaojenga na kulihakikishia taifa letu umoja, amani, utulivu na upendo miongoni mwa raia wa nchi yetu.

Ndugu zangu;
Napenda kuwahakikishia Watanzania wenzangu kuwa siku zote mimi na wenzangu wote Serikalini tunatambua unyeti wa suala la OIC. Aidha, tunatambua dhamana yetu ya kuwa makini katika kufikia uamuzi na kwa uamuzi wenyewe tutakaoufanya kuhusu suala hili. Kamwe hatutafanya uamuzi ambao utavuruga mambo na kuhatarisha amani, umoja na mshikamano wa nchi yetu, Serikali zetu na watu wake.

Hivyo narudia kuwasihi Watanzania wenzangu tuiache Serikali ilifanyie kazi kwa ukamilifu suala hili. Tujiepushe na vitendo au kauli ambazo zitawatia watu hofu na kujenga chuki miongoni mwa raia wa nchi yetu wanaopendana na kujenga chuki na kutoaminiana baina ya raia na Serikali yao inayowapenda na kuwathamini.

Madai ya Malimbikizo ya Walimu
Ndugu Watanzania wenzangu;
Jambo la pili ninalotaka kulizungumzia leo, linahusu madai ya malipo ya walimu kuhusu malimbikizo ya mishahara, nauli za likizo na posho za uhamisho na kujikimu. Kama sote tujuavyo Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kiliiarifu Serikali nia yake ya kuitisha mgomo wa walimu wote nchini iwapo madai ya walimu yapatayo shilingi bilioni 16.4 (bilioni 12.2 kwa ajili ya walimu wa shule za msingi na bilioni 4.2 kwa walimu wa shule za sekondari na vyuo vya walimu) yatakuwa hayajalipwa yote ifikapo tarehe 15 Oktoba, 2008.

Baaada ya kupata taarifa hiyo Serikali iliwasiliana na uongozi wa juu wa CWT kwa nia ya kufanya mazungumzo nao kuhusu madai yao. Bahati nzuri uongozi wa CWT ulikubali, hivyo mazungumzo yakafanyika baina ya Serikali na CWT. Upande wa Serikali uliwakilishwa na wajumbe 12 kutoka Wizara za Utumishi, Fedha na Mipango, TAMISEMI na Elimu na Mafunzo ya Ufundi na upande wa CWT uliwakilishwa na wajumbe saba (7).
Kiongozi kwa upande wa Serikali alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Mheshimiwa Hawa Ghasia na upande wa CWT kiongozi alikuwa Ndugu Yahaya Msulwa ambaye ndiye Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu, Tanzania.

Katika mazungumzo hayo ukiacha suala la madai ya malipo yalikuwepo pia masuala mengine matano yafuatayo:
1. Kupandishwa madaraja (vyeo).
2 CWT kushirikishwa katika uhakiki wa madai ya walimu.
3. Kuundwa kwa Baraza la Majadiliano ya Pamoja katika Sekta ya Elimu (Teachers Joint Staff Council).
4. Kuandaliwa kwa Taratibu za Uendeshaji wa Utumishi wa Walimu (Teachers Service Scheme) na
5. Kuwarudisha kwenye Orodha ya Malipo (Payroll) walimu waliofutwa kwenye orodha hiyo.
Baada ya siku 15 za mazungumzo muafaka ukafikiwa juu ya masuala yote sita na makubaliano hayo ya pamoja kutiwa saini na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Mheshimiwa Profesa Jumanne Maghembe kwa niaba ya Serikali na Katibu Mkuu wa CWT, Ndugu Yahaya Msulwa kwa niaba ya Walimu.

Jambo lililotushangaza na kutusikitisha sote ni kauli ya Rais wa CWT, Ndugu Gratian Mkoba tarehe 08 Oktoba, 2008 kwamba mgomo unaendelea.
Tena akasisitiza kuwa mgomo huo hauna muda maalum mpaka mwalimu wa mwisho atakapokuwa amelipwa. Nilimuagiza Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi kuwa, wawatafute viongozi wa CWT kuzungumza nao kuwasihi waache kuendelea na mgomo, lakini juhudi zote hazikuzaa matunda.
Waling’ang’ania kuendelea na mgomo na ndipo tukaitumia haki yetu kwa mujibu wa Sheria ya Kazi Na. 6 ya mwaka 2004 kuomba Mahakama kuu kitengo cha Kazi iamuru mgomo usiwepo na kuwataka viongozi wa CWT warudi kwenye mazungumzo na Serikali.

Viongozi wa CWT wanapinga uamuzi huo wa Mahakama Kuu na kutaka waendelee na mgomo. Tupo mahakamani tunasubiri uamuzi wa Mahakama kuhusu rufaa ya CWT.

Ndugu wananchi;
Najua wapo walioushangaa uamuzi wa Serikali wa kwenda mahakamani na wapo pia watu waliotukejeli kwa uamuzi wetu huo. Kwanza kabisa ni haki ya mwajiri kufanya hivyo na mahakama ndicho chombo chenye mamlaka ya kuamua. Lakini, pia, tumefanya hivyo kwa nia njema ya kunusuru janga ambalo mfumo wa elimu ungelikuta nchini kwa mgomo huo ambao ungekuwa wa aina yake.
Maana kuendelea kuwepo mpaka mdai wa mwisho atakapolipwa wakati inawezekana baadhi ya wadai wanaweza kuwa na vithibitisho ambavyo vinaweza kukataliwa na mlipaji kwa kutokuwa halali ni sawa na kuwa na mgomo wa kuchukua muda mrefu sana. Unaweza usiwe na ukomo kwani ubishi kuhusu uhalali wa stakabadhi ya mdai unaweza kuchukua muda mrefu. Vinginevyo ichukuliwe kuwa, kila anachodai mwalimu ni sahihi kilipwe na Serikali. Hilo nalo ni gumu kwani upo ushahidi wa kuwepo kwa stakabadhi za kughushi.

Ndiyo maana sisi katika Serikali tumeyaafiki makubaliano ya kufanya uhakiki wa pamoja utakaoshirikisha CWT na Serikali.
Nilipokuwa Tabora hivi karibuni nilielekeza kuwa uhakiki huo ufanywe shule kwa shule na mwalimu kwa mwalimu; usifanywe kwa kukagua mafaili tu katika maofisi ya Maafisa Elimu na Utumishi. Kufanya hivyo kutatupa taarifa iliyo sahihi ya nani anadai nini. Itasaidia kung’oa mzizi wa fitina. Hakutakuwepo na kudaiana kusikokwisha.

Vilevile, itatusaidia kujua uweli wa walimu waliopo na wako wapi. Kuna minong’ono ya kuwepo walimu hewa ambao pesa zao hutolewa kila mwezi. Pia, wapo walimu waliotangulia mbele ya haki ambao bado wamo kwenye orodha ya utumishi na mishahara yao huendelea kutumwa na hairejeshwi.

Ndugu Wananchi;
Napenda kuitumia nafasi hii kuwahakikishia walimu na wananchi wote wa Tanzania, kuwa Serikali inawathamini na kuwajali walimu. Serikali ya Awamu ya Nne inaweka kipaumbele cha juu sana kwa maendeleo ya elimu, ndiyo maana bajeti ya elimu ndiyo bajeti kubwa kuliko zote. Inachukua asilimia 19.8 ya bajeti yote ya Serikali. Watanzania wote ni mashahidi wa nguvu kubwa tuliyoielekeza katika elimu ya sekondari, elimu ya juu na elimu ya ufundi. Mimi na viongozi wenzangu kuendeleza elimu ni agenda yetu kuu.

Katika juhudi hizo tunatambua nafasi na umuhimu wa Mwalimu. Hatuwezi kua watu tunaohimiza upanuzi wa elimu lakini tunampuuza mwalimu. La hasha! Mara nilipoingia madarakani, katika mkakati wa kuboresha maslahi ya watumishi, kundi tuliloanza nalo ni walimu na tumeendelea kulipa kipaumbele kila tuliposhughulikia makundi mengine.

Katika mkakati wa kuboresha maslahi ya watumishi wa umma tulitambua kuwa hatutaweza kufanya hivyo kwa watumishi wote kwa wakati mmoja. Tukaona tukienda kwa makundi tunaweza. Kundi la kwanza tuliloanza nalo ni walimu. Natambua haja ya kuendelea kuboresha maslahi ya watumishi wa umma nchini, ni nia yetu kufanya hivyo. Tumekuwa tunafanya hivyo katika miaka mitatu hii na tutaendelea kufanya hivyo miaka ijayo.

Pamoja na hayo, mwezi April, 2008, tumewalipa Walimu Shs. 7.2 bilioni, sehemu kubwa ikiwa ni madeni ya nyuma kabla sisi hatujaingia madarakani. Huu ni ushaidi kwamba tunawajali walimu. Mimi nitakuwa mtu wa mwisho kupuuza maslahi ya walimu.



Mauaji ya Maalbino
Ndugu zangu, Watanzania wenzangu;
Tarehe 19 Oktoba, 2008 nilipewa heshima ya kupokea maandamano ya kulaani na kupinga mauaji ya wenzetu wa jamii ya Maalbino. Katika maandamano hayo nilielezea kusikitishwa kwangu na matendo hayo ya kikatili na ya aibu kwa nchi yetu. Siku ile nilitoa wito kwa Watanzania wote kushiriki na kushirikiana katika mapambano haya halali ili kwa umoja wetu tuweze kukomesha mauaji ya ndugu zetu hao.

Leo nataka kuwaelezea azma ya kuwataka Watanzania kote nchini kutoa taarifa kuhusu watu wanaojihusisha na mauaji ya Albino nchini. Kwa maana ya waganga, wauaji, wauzaji na wanunuzi wa viungo vya Albino.
Nawataka Watanzania wawataje kwa siri watu hao ili Serikali ifuatilie kwa karibu nyendo zao, kuwabana ipasavyo na kuwachukulia hatua mwafaka. Utaratibu huu ulitusaidia sana katika mapambano dhidi ya majambazi, naamini utatusaidia hata katika mapambano haya halali na ya haki. Baada ya muda si mrefu tutatoa maelekezo juu ya utaratibu wa kutoa na kukusanya taarifa hizo.

Nataka kuwahakikishia wananchi kuwa Serikali yenu haitakaa kimya wakati raia wasiokuwa na hatia wanaendelea kuteswa na kuuawa. Albino ni mwanadamu kama alivyo mwanadamu mwingine yeyote. Ana haki ya kuishi na kupata hifadhi ya maisha na mali zake kutoka katika jamii. Kuwaua kwa sababu yoyote ile si haki na ni kosa kubwa.

Isitoshe kwa sababu wanazouliwa ni aibu kwa mhusika na fedheha kubwa kwa jina zuri la nchi yetu. Kila mmoja wetu anao wajibu wa kuelimisha jamii juu ya madhara ya fikra potofu zinazoenezwa na waganga wa kienyeji wenye tamaa na uchu wa kujipatia utajiri. Utajiri utapatikana kwa kufanya kazi kwa bidii na maarifa na kuwa na nidhamu katika utendaji na matumizi ya mapato yako. Sote tunawajibika kuwafichua watu hawa ambao ni hatari katika jamii yetu. Naomba ushirikiano wa kila mmoja wetu ili tuikomeshe na kuondoa aibu hii.


Fedha za EPA
Ndugu wananchi;
Jambo la mwisho, na la muhimu sana, ninalotaka kuzungumzia leo linahusu urejeshwaji wa fedha za akaunti ya madeni ya nje katika Benki Kuu inayojulikana kwa kifupi kama EPA. Wengi wenu mtakumbuka kuwa, nilipozungumza na Bunge tarehe 21 Agosti, mwaka huu, nilieleza kwa kirefu yaliyotokea, hatua tulizochukuwa na mahali tulipokuwa tumefikia katika kulishughulikia suala hili. Nisingependa kuwachosha kwa kurudia tena yale niliyoyasema.


Ndugu wananchi;
Nilielezea pia kwamba baada ya tarehe 31 Oktoba, 2008, kwa wale ambao watakuwa hawakuteleza, hatua za kisheria zichukuliwe. Leo ndiyo siku ya mwisho. Napenda kuwajulisha kuwa kiasi cha shilingi 69,326,437,650 kati ya shilingi 90,359,078,804 zimerejeshwa. Hii ni sawa na asilimia 76.7.

Pamoja na kufanya hivyo, nimekwishatoa maelekezo kamili kwa wale ambao hawakutimiza malipo, Kamati ikabidhi majalada yao kwa Mkurugenzi wa Mashtaka mara moja, kwa hatua zipasazo za kisheria.

Yapo malalamiko kwamba wale waliorudisha pia wanatakiwa kuwajibishwa. Lakini kwa kuwa serikali ilikuwa imeshawaahidi msamaha, itakuwa si sawa kuvunja ahadi yetu. Lakini tunaelewa pia kuwaachia huru itakuwa si haki. Kwa hiyo, naomba nichukue fursa hii kuomba watanzania watulazimishe kisheria kuwachukulia hatua, Kwa mfano, kutushitaki mahakamani na kuiomba mahakama itangaze kwamba msamaha wetu si halali ni jia mojawapo. Na hilo likitokea, sisi tutakuwa tayari kufuata amri ya mahakama na kuwafungulia hawa mashitaka. Hii ndio itakuwa njia rahisi kwa kila mmoja wetu.

Ndugu Watanzania wenzangu;
Kuhusu uchunguzi uliokuwa unaendelea kufanywa kuhusu yale makampuni 9, nasubiri taarifa yao mpya kuhusu maendeleo ya uchunguzi huo. Taarifa nilizonazo zinaonyesha kuwa polisi wetu bado hawajapata majibu kutoka kwa wenzao katika nchi walizoomba msaada. Hivyo, nawataka waendelee kufuatilia kwa wenzao ili hatua zipasazo ziweze kuchukuliwa.

Ndugu wananchi;
Kwa mara nyingine tena napenda kuchukua fursa hii kuipongeza Kamati ya Mwanasheria Mkuu kwa kazi nzuri iliyofanya ambayo mbali na kubaini namna ya tuhuma za uhalifu zilivyofanywa, pia ilibaini wahusika na kuwabana kiasi cha kufanikiwa kurejeshwa kwa fedha ambazo vinginevyo zingepotea kabisa. Ingawa kimantiki hii inatakiwa iwe kazi ya polisi, lakini mazingira yalilazimu tuwe na kamati makini kama hii. Na tunaona matokeo yake mazuri.

Lakini kubwa zaidi, nawashukuru wananchi kwa uvumilivu na uelewa wao wakati wote serikali ilipokuwa inalishughulikia sakata hili la aina yake katika historia ya nchi yetu. Tumefarijika sana kwa uelewa na ushirikiano wenu. Nawaomba tuzidi kushirikiana katika mambo yote yanayohusu mustakabhali wa nchi yetu.

Aidha, utaratibu wa kuzigawa fedha hizo kwa ajili ya shughuli za kilimo na miundombinu zimekamilika.

Madai ya Wastaafu Jumuiya ya Afrika Mashariki
Katika hotuba yangu ya leo, sikuweza kugusia suala la madai ya wastaafu wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa sababu Serikali inaandaa tamko rasmi litakalowasilishwa Bungeni na Waziri wa Fedha na Mambo ya Uchumi, Mheshimiwa Mustafa Mkullo wiki ijayo. Hivyo nawaomba sote tuvute subira.

Hitimisho
Kabla ya kumaliza napenda kutumia fursa hii kuwashukuru wananchi wote kwa kuendelea kuiunga mkono serikali katika mambo yote ya msingi yanayoihusu nchi yetu. Licha ya mawimbi ya hapa na pale ambayo tunapambana nayo katika safari yetu, tumeendelea kuimarisha umoja na mshikamano wetu ambao ndio nguzo na mhimili wa taifa letu.
Nawaomba tuendelee kufanya hivyo kwa kutambua kuwa hiyo ndiyo njia pekee ya kujenga nguvu ya pamoja ya kuendeleza taifa letu. Nawasihi tujiepushe na mambo yanayoweza kutugawa na kupandikiza mbegu za chuki miongoni mwetu na badala yake tuimarishe maelewano, mshikamano na umoja wa kitaifa.

Mungu Ibariki Afrika;
Mungu Ibariki Tanzania.
Asanteni kwa kunisikiliza.

Imetolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais
Ikulu.
Dar es Salaam.
31 Oktoba, 2008



No comments: