Mazungumzo ya Soko
Tanzania haijakubaliana
na mawazo ya nchi nyingine
kuhusu uhuru wa kusafiri,
mgawanyo wa ardhi,
uraia wa kudumu na
masuala ya huduma.
Faraja Mgwabati
Daily News
Mazungumzo ya kuanzishwa kwa Soko la Pamoja la Afrika Mashariki yamekwama baada ya Tanzania kugomea baadhi ya vipengele ambavyo imeona vina maslahi kwa taifa. Mazungumzo hayo ambayo yanafanyika chini ya Jumuiya ya Afrika Mashiriki (EAC) ilibidi yakamilike mwezi ujao, lakini kutokana na kushindwa kufikiwa kwa mwafaka, yamesogezwa hadi Aprili mwakani.
Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Diodorus Kamala alisema Dar es Salaam kuwa Tanzania haijakubaliana na mawazo ya nchi nyingine kuhusu uhuru wa kusafiri, mgawanyo wa ardhi, uraia wa kudumu na masuala ya huduma. Dk. Kamala alisema baadhi ya nchi zinataka soko la pamoja likianzishwa, kuwe na uhuru na haki ya kupata ardhi, kitu ambacho Tanzania inakataa kwa sababu nchi nyingine haina ardhi ambayo Watanzania wataweza kupata.
Alisema pia sheria za ardhi za nchi hizo zinatofautiana, kitu kitakacholeta mtafaruku ambao mwisho wa siku, Tanzania ndiyo itaathirika kwa nchi nyingine kuchukua ardhi kwa kuwa ina ardhi kubwa. “Tumeona suala la ardhi tusiliingize kabisa kwenye suala la soko la pamoja…ukitaka kuleta machafuko basi ingiza suala la ardhi kwenye soko la pamoja,” alisema Dk. Kamala ambaye pamoja na Kamati ya kisekta ya Mawaziri wa EAC walikutana Zanzibar wiki hii.
Kuhusu uraia wa kudumu, Dk. Kamala alisema Tanzania inapinga kuwapo kwa haki ya kupata uraia kwa wananchi waliokaa ndani ya nchi moja kwa miaka mitano, kwa sababu itailazimisha Tanzania kuwapa uraia hata wageni ambao wamekaa nchini isivyo halali. Alisema Tanzania itaendelea na utaratibu wake uleule wa kuwapa uraia wageni wenye sifa ili kuziba mianya ya wachache ambao wanaweza kutumia mgongo wa soko la pamoja kukaa nchini.
Kamala alisema Tanzania pia inapinga mawazo ya baadhi ya nchi kutaka vitambulisho vya uraia vitumike mipakani badala ya pasipoti ili kurahisisha wasafiri kuingia nchi nyingine kwa urahisi. Alisema mazungumzo hayo yataendelea tena Machi mwakani na kama hadi Aprili mwafaka hautafikiwa, basi wataongeza muda zaidi, lakini Tanzania haitakubali kwenda haraka kama itaona hakuna manufaa.
No comments:
Post a Comment