Viza ya Uingereza sasa
kuombwa kwa intaneti
Na Abdallah Bawazir
Ubalozi wa Uingereza nchini, umebadili utaratibu wa kuomba viza kwa Watanzania wanaotaka kuingia nchini humo ambapo kwa sasa waombaji watatakiwa kutuma maombi yao kupitia mtandao wa kompyuta (intaneti).
Hayo yalisemwa na Ofisa Habari wa Ubalozi wa Marekani nchini, John Bradshaw, wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana.
Alisema ubalozi huo umebadili utaratibu wa kuomba viza kwa Watanzania wanaokwenda nchini humo, ambapo sasa waombaji watatakiwa kutuma maombi yao kupitia mtandao.
Bradshaw alisema utaratibu huo mpya ni sehemu ya merekebisho yanayofanywa katika mfumo mzima wa utoaji wa viza ya nchi hiyo duniani kote unaojulikana kama `Hub & Spoke Visa Processing`, ambao lengo lake ni kupunguza nusu ya vituo vya utoaji wa huduma hiyo hadi kufikia 50 duniani kote.
``Utaratibu huu utapunguza nusu ya vituo vya utoaji viza ya Uingereza duniani hadi kufikia 50, kwa mfano kwa upande wa nchi za Kusini mwa Afrika waombaji kutoka nchi za Namibia, Botswana, Msumbiji, Lesotho, Swaziland, Malawi na Zimbabwe wanaombea Pretoria, Afrika Kusini wakati ubalozi wa Nairobi unashughulikia maombi ya nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Kenya yenyewe na ya nchi za Ulaya, Amerika na Asia huduma hiyo imeondolewa katika balozi zaidi ya 50 na kuhamishiwa katika vituo vya kikanda,`` alisema Bradshaw.
Alifafanua kuwa kwa Tanzania, kupitia utaratibu huo mpya, maombi yote ya viza sasa yatapokelewa katika ubalozi wake uliopo Dar es Salaam na kisha maombi hayo yatapekekwa katika ubalozi wake wa Nairobi nchini Kenya kwa ajili ya kushughulikiwa na kisha kurejeshwa tena nchini kwa ajili ya kupewa mhusika.
Alisema mchakato mzima tangu siku ya kwanza ya kuwasilisha ombi la kupata viza, utachukua muda wa wiki tatu.
``Utaratibu huu wa kuomba viza kupitia `intaneti` ni wa haraka na unaojulikana zaidi na wateja wetu wengi, zaidi ya asilimia 80 ya waombaji wa Tanzania wanatumia utaratibu huu kwa sasa,`` aliongeza kusema.
Hata hivyo, alisema utaratibu wa awali wa waombaji kupeleka maombi yao moja kwa moja kwenye ubalozi wa Dar es Salaam bila ya kupitia mtandao wa kompyuta utaendalea kutumika, ila maombi hayo hayatashughulikiwa haraka kama wale wakaoomba kupitia intaneti.
- SOURCE: NIPASHE
No comments:
Post a Comment